NA MWINYIMVUA NZUKWI
Kamati Maalum ya Halmashauri kuu ya CCM Zanzibar imefanya uteuzi wa wajumbe wa sekretarieti na kupitisha majina ya wajumbe wa kamati ya maadili itakayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein katika kikao maalum kilichofanyika katika Afisi kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui.
Kikao hicho kilichofanyika kwa mara ya kwanza toka kukamilika kwa uchaguzi wa ngazi mbali mbali za uongozi wa chama hicho, iliwateua wajumbe wa sekretarieti ya CCM ambao pia ni wakuu wa idara mbali mbali itakayodumu kwa miaka mitano ijayo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdallah Juma Sadallah ‘Mabodi’ aliwataja wajumbe wa sekretarieti hiyo kuwa ni pamoja na aliyewahi kuwa Katibu wa CCM mkoa wa Kaskazini Unguja Catherine Peter Nao alieteuliwa kuongoza idara ya Idara ya Itikadi na Uenezi nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na mjumbe wa NEC Waride Bakar Jabu.
Wajumbe wengine wa sekretarieti hiyo inayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar kikatiba ni Bakari Hamad Khamis anaekuwa Katibu wa Idara ya Oganaizesheni iliyokuwa ikishikiliwa Haji Mkema Haji, Kombo Hassan Juma anaekuwa Katibu wa Idara Siasa na Uhusiano wa Kimataifa iliyokuwa ikiongozwa na Naibu waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Masauni Hamad Masauni na Afadhali Tybu Afadhali anaekuwa Katibu wa Idara ya Fedha na Uchumi.
Kikao hicho pia kimeridhia majina ya wajumbe wa kamati maadili ya chama cha Mapinduzi Zanzibar itakayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdallah Juma Sadallah ambae ni Katibu wa kamati hiyo na Wajumbe Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi, Mjumbe wa sekretarieti Kombo Hassan Juma, Yasmin Aloo na Ramadhan Shaib Juma.
Aidha Dk. Sadallah alieleza kuwa kikao hicho kimepokea taarifa ya mwelekeo wa chama kwa kipindi cha miaka 10 ijayo na kuwahimiza wajumbe wa mkutano huo na vingozi wengine wa chama kusimamia utekelezaji wa ilani ya ccm katika maeneo yao ya utendaji.
"Aidha kikao pia kiliwataka wajumbe kuzingatia maeneo yote yaliyotiliwa mkazo katika mkakati mpya wa mabadiliko ndani ya chama na kuwataka kurudi walipo wanachama na wananchi ili kujenga uhai wa chama na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa ilani", alieleza.
Kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na wajumbe 68 kati ya 69 wanaounda kamati maalum ya halmashauri kuu ya CCM Zanzibar ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi.
Mwishoni mwa mwaka uliopita chama hicho kilikamilisha uchaguzi wake katika ngazi ya taifa ambapo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa walimchagua Dk. John Pombe Magufuli kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Zanzibar na Philp Japhet Mangula kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania bara.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein (wa pili
kulia) akiimba wimbo wa 'Chama chetu cha Mapinduzi chajenga nchi' mara
alipowasili katika ukumbi wa mikutano wa afisi kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui
kuongoza kikao cha kamati maalum ya halmashauri kuu ya CCM Zanzibar. Wengine
kutoka kushoto ni wajumbe wa kamati hiyo Balozi Seif Ali Idi Makamu wa pili wa
Rais wa Zanzibar, Samia Suluhu Hassan Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Dk. Abdalla Juma Sahallah Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha Kamati Maalum ya halmashauri kuu ya
CCM Zanzibar wakiwa katika kikao cha kwanza cha kamati hiyo kilichoongozwa na
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dk. Ali Mohamed Shein ambae pia ni Rais wa
Zanzibar.
Dk. Abdalla Juma Sadallah Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar akitoa
taarifa ya maamuzi ya kikao cha kamati maalum ya halmashauri kuu ya CCM
Zanzibar kwa waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho.
Katibu mpya wa idara ya Itikadi na Uenezi wa Kamati maalum ya
halmashauri kuu ya CCM Zanzibar Catherine Peter Nao (mbele) akifurahia jambo
kabla ya kuteuliwa kushika wadhfa huo wakati wa kikao cha kamati maalum ya
halmashauri kuu ya CCM Zanzibar kilichofanyika Februari 4, 2018 mjini Zanzibar.
No comments:
Post a Comment