Saturday, February 10, 2018

DK. SHEIN AWATAKA WALIMU, WIZARA KUSAKA MWARUBAINI WA KUSHUKA KWA ELIMU ZANZIBAR

NA MWINYIMVUA NZUKWI
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar kuanzisha utaratibu wa kukutana na chama cha walimu Zanzibar (ZATU)  mara mbili kwa mwaka ili kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoikabili sekta ya elimu na ualimu nchini.

Akifungua mkutano mkuu wa 6 wa ZATU katika ukumbi wa zamani wa baraza la wawakilishi mjini Unguja, Dk. Shein alisema katika vikao hivyo wadau hao wajadili na kupanga mikakati ya kuimarisha elimu ya Zanzibar aliyosema licha jitihada zinazochukuliwa na serikali yake imekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka.

Dk. Shein alisema ili maendeleo ya haraka yapatikane nchini wadau wa sekta hiyo hawana budi kukaa pamoja na kufikiria namna bora ya kuimarisha elimu wakati serikali kuu ikiendelea kuzitafutia changamoto mbali mbali ikiwemo ya ukosefu wa madawati na madarasa ya kusomea.

“Kwa miaka mitatu mfululizo serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya wizara ya elimu ili kukabiliana na changamoto zinazoshusha ubora wa elimu pamoja na kupunguza gharama za elimu kwa wazazi wa wanafunzi kwa kuondoa michango”, alisema Dk. Shein.

Aidha aliwapongeza walimu wa Zanzibar kwa jitihada wanazochukua katika ufundishaji licha ya kukabiliwa na changamoto mbali mbali na kueleza kuridhishwa kwake na matokeo ya mitihani ya darasa la 4, 6, kitato cha pili na kidato cha sita huku akiiagiza wizara ya elimu kukutana na walimu wakuu wa skuli sita za Zanzibar ziliopo katika orodha ya skul;i 10 zilizofanya vibaya kitaifa katika mitihani ya kidato cha nne.

Alisema matokeo ya mitihani ya kidato cha nne ya mwaka uliopita yameshuka kutoka asilimia 73.8 (2016) hadi asilimia 70.8 (2017) hivyo wizara inatakiwa kutafuta chanzo hali hiyo na namna ya kuzuia isijierejee katika kipindi kijacho.

“Hakuna mwalimu anaefurahi wanafunzi wake wanapofeli, hivyo ni vyema viongozi wa wizara mkakutana na walimu wa skuli hizi ili mjadiliane namna ya kuondokana na aibu hii ambayo haikutufurahisha sote”, alisema Rais Dk. Shein.

Akijibu maombi ya zatu kuhusu malipo ya malimbikizo ya madeni ya walimu, kuopndolewa kwa madaraja ya utumishi kwa walimu na kuundwa kwa tume ya utumishi ya walimu, Dk. Shein aliiagiza wizara ya elimu kukukaa na wizara ya fedha na mipango na kuhakikisha madeni hayo yanalipwa haraka.

“Hili la ‘scheme of service’ (mpango wa utumishi) nataka wizara katika muda mfupi ujao mkutane na Wizara ya Katiba, Sheria, Utawala bora na Utumishi wa Umma) na mlirekebishe na kuwarudishia stahiki zao kwani hili ni agizo langu nililolitoa mwaka 2012 kwa watumishi wote sasa iweje walimu wawekwe katika huo mpango kisha waondolewe?”, alihoji Dk. Shein.

Akiwataka walimu kuvuta subira kuhusu swali la uundwaji wa tume ya utumishi ya walimu ili kupisha mapitio ya sera ya elimu ya mwaka 2006 na kuwataka washirikishwe ili kutoa maoni yao ambayo alisema ni muhimu katika kuiimarisha sera hiyo ambayo inatamka kuanzishwa kwa tume hiyo, mfuko wa elimu Zanzibar na kodi ya elimu.

Mapema akisoma risala ya walimu Katibu Mkuu wa ZATU Mussa Omar Tafurwa alisema licha ya mafanikio makubwa yaliyofikiwa na chama hicho bado sekta ya elimu Zanzibar inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ya uhaba wa walimu.

Alisema utafiti uliofanywa na chama hicho mwaka mwishoni mwa uliopita kisiwa cha pemba pekee kinahitaji jumla ya walimu 800 huku mikoa ya Kaskazini na Kusini Unguja ikionesha kuathiriwa na hali hiyo na kuiomba serikali kutoa kipau mbele kwa ajira za walimu.

“Pamoja na hayo pia tunakabiliwa na uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia hivyo tunaiomba serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kulipwa kwa malimbikizo ya stahiki za muda mrefu za walimu”, alisema Tafurwa.

Nae Rais wa ZATU Mwalim Seif Mohammed Seif alimshukuru na kumpongeza Dk. Shein kwa hatua anazochukua katika kustawisha elimu ya Zanzibar na maisha ya watumishi wa umma katika kipindi chake cha utawala.

“Katika kipindi cha uongozi wako, sisi walimu tunaounda sehemu kubwa ya watumishi wa umma, tumeshuhudia uanzishwaji wa mahkama ya kazi na chombo cha majadiliano na mashauriano ya kisekta mambo ambayo yameimarisha mahusiano mema katika maeneo ya kazi”, alisema Mwalim Seif.

Akimkaribisha mgeni rasmi kuhutubia hadhara hiyo, Kaimu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo ambae pia ni Waziri wa Afya alisema msongamano wa wanafunzi katika skuli za Zanzibar linatokana na ongezeko kubwa la watu linaloikabili Zanzibar ikilinganishwa na idadi ya skuli.

Alisema serikali itaendelea na juhudi za kujenga majengo ya skuli ili kuongeza idadi ya madarasa ili kukabiliana na msongamano wa wanafunzi hususani katika elimu ya msingi.

“Hili la wingi wa watoto wanaokuwemo madarasani halitokani na uchache wa skuli bali pia na ongezeko la watu ambalo limefikia asilimia 2.8 kila mwaka wakati Zanzibar inapokea vizazi vipya 50,000 kwa mwaka, wakati wastani wa watoto 100 wanazaliwa kwa siku katika  hospitali ya Mnazi Mmoja pekee”, alieleza waziri Kombo.


Mkutano huo wa siku mbili utakaomalizika Februari 11, 2018 mbali ya walimu pia ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar akiwemo Naibu Waziri wake Mmanga Mjengo Mjawiri, wakuu wa mikoa mitatu ya Unguja, viongozi wa vyama vya walimu vya Tanzania bara, Kenya, Uganda, Denmark na viongozi wa muungano wa vyama vya wafanyakazi Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

No comments:

Post a Comment