Thursday, February 22, 2018

VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA - VYOMBO VYATAKIWA KUACHA UTASHI

NA MIZA KONA MAELEZO – ZANZIBAR
Wasimamizi wa sheria na vikosi vya ulinzi na usalama wametakiwa kuacha utashi na kufanya kazi kwa uzalendo ili kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Mkurugenzi mtendaji Tume ya Taifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar Kheriyangu Mgeni Khamis alitoa rai hiyo katika kikao cha pamoja kati ya taasisi hizo kilichofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkokotoni.
amewataka watendaji hao wawe waadlilifu katika ngazi zote za utendaji ili kuweza kudhibiti uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya nchini.
Kikao hicho kiliitishwa na tume hiyo kwa lengo la kujadili namna ya kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya katika mkoa huo kutokana na uwepo wa bandari ndogo ndogo zinazohusishwa kuwa njia zinazotumiwa kuingizwa kwa dawa hizo.
Alisema kuna baadhi ya ya vyombo vya kusimamia sheria havitekelezi vyema majukumu yao na kupelekea kufutwa kwa baadhi ya kesi na hivyo kurudisha nyuma juhudi za serikali za kutokomeza dawa hizo.
Alieleza kuwa wasimamizi wa sheria wakiwa makini na waadilifu pamoja na kushirikiana na jamii, wanaweza kufanya kazi bila ya migogoro na kuwafichua wahalifu wanaofanya biashara haramu ya dawa za kulevya katika mkoa huo.
Mkurugenzi huyo alieleza kwa Mkoa wa Kaskazini umekuwa ukiongoza kwa kesi za dawa za kulevya kutokana na wimbi kubwa la uingizaji na utumiaji wa dawa hizo.
“Ni vyema kuzisimamia ipasavyo sheria ili kuweza kuzuia na kudhibiti uhalifu huu usiingie nchini na kuinusuru na nguvu kazi ya taifa isiathirike na matumizi ya dawa za kulevya”, alisema na kueleza kuwa tume yake imejipanga kuimarisha mfumo utakaodhibiti uingiaji wa dawa hizo nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Vuai Mwinyi Mohammed, akizungumza katika kikao hicho alitaka kubadilishwa kwa sera na sheria zilizopo ili ziendane na mazingira ya sasa pamoja na kuondoa muhali na kudhibiti tatizo hilo nchini.
Wakichangia majadiliano hayo, washiriki wa kikao hicho wameitaka Tume hiyo kuweka maofisa katika ofisi za mikoa watakaoweza kuratibu na kushughulikia suala hilo.
Aidha walitaka hatua kali na za haraka zichukuliwa kwa wanaobainika kujihusisha na biashara hiyo ili kuepukana na usumbufu katika ufuatiliaji wa kesi hizo wanaoupata wasimamizi wa sheria.
Aidha walieleza kuwa ukosefu wa vifaa vya kisasa unapelekea kukosa taarifa za haraka na hivyo kusababisha kuongezeka kwa uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya katika mkoa huo.

No comments:

Post a Comment