NA MWINYIMVUA NZUKWI
Wakongwe wa soka wilaya
ya Magharibi ‘A’ Unguja timu ya Muungano Rangers ya Dole imekamilisha mzunguko
wa 6 wa ligi daraja la pili wilayani humo kwa kuwafunga wapinzani wao wa jadi
Kizzy Stars ya Kizimbani goli 1 - 0 katika mchezo mkali uliochezwa katika dimba
la Mwakaje.
Rangers iliyoteremka kutoka daraja la pili taifa msimu uliopita
ilianza harakati za kusaka ushindi huo toka katika dakika za awali za mchezo
huo na kukabiliana na upinzani wa hali ya juu kutoka kwa wachezaji wa timu ya
Kizzy ambao walifanikiwa kulifikia lango la Rangers mara kadhaa huku mashabiki
wa timu zote mbili wakiuchochea upinzani huo uliopelekea timu hizo kumaliza
dakika 45 za mwanzo zikiwa nguvu sawa.
Kama ilivyokuwa katika kipindi cha kwanza timu hizo ziliopo
kundi A zilishambuliana kwa zamu kabla ya Muungano kupata goli lake kupitia kwa
Farid Abdallah mnamo dakika ya 50 ya mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki
wengi wa soka.
Katika mchezo huo timu hizo zinazotoka katika vijiji jirani
zilifanya mabadiliko kwa wakati tofauti kwa Muungano kuwatoa Ayoub Zubeir,
Saleh Ahmada na James Charles na nafasi zao kuchukuliwa na Mohammed Hiyar,
Fadhil Ramadhan na Juma Ramadhan huku Kizzy wakiwatoa Saleh Kassim, Mussa Bakar
na Edward Mohammed ambapo nafasi zao zikachukuliwa na Feisal Mohammed, Antony
Ali na Mohammed Ali.
Matokeo mengine ya mzunguko huo kwa timu za kundi A, Scud S. C
iliibamiza bila huruma Mbuzini F C kwa kuifunga mabao 3 - 0, Kianga
International ikaifunga bila huruma Mwakaje star 5 - 2 kabla ya Blue Stars
kutoka sare ya bao 1 - 1 na Mtopepo United.
No comments:
Post a Comment