NA
MWINYIMVUA NZUKWI
SERIKALI
ya Zanzibar imewataka wafanyabiashara na waingizaji wa bidhaa za matairi ya
magari na vyombo vingine vya moto kuzingatia utaratibu mpya utakaonzishwa na
taasisi ya viwango Zanzibar (ZBS) kuhusiana na uingizaji wa bidhaa hizo ili kukuza
uchumi wa nchi na ustawi wa jamii.
Naibu
katibu mkuu wa wizara ya biashara, viwanda na masoko ali khamis juma alitoa
wito huo alipokuwa akifungua semina ya siku moja kwa wafanyabiashara wa bidhaa hizo iliyolenga
kutoa elimu kwa kundi hilo ili kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.
Alisema
dhana ya ukuaji wa uchumi na biashara huria zinategemea uwezo wa uzalishaji na
matumizi ya bidhaa au huduma zenye ubora unaoendana na viwango vinavyotambulika
kitaifa na kimataifa ambavyo vinahakikisha afya za watumiaji na mazingira ya
nchi yanabakia salama na endelevu.
Alisema
matairi ya vyombo vya moto ni miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa na kutumika
katika shughuli nyingi za maendeleo ya kila siku kupitia huduma ya usafiri na
usafirishaji wa abiria na mizigo hivyo kuna haja kubwa ya wafanyabiashara hao
kutumia elimu waliyopatiwa kuwaelimisha watumiaji wengine wa bidhaa hizo jambo
alilodai litasaidia kupunguza ajali na uharibifu wa mazingira.
“ZBS
(Taasisi ya viwango Zanzibar) itaendelea kufanya ukaguzi kioa mara ili
kuhakikisha bidhaa zinazoingia katika soko la Zanzibar na kutumika zinazingatia
usalama, afya, mazingira na ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa
ujumla na sio chanzo cha madhara kwa jamii yetu kwa faida ya sasa na baadae”,
alisema Khamis.
Awali
akikitoa maelezo ya utangulizi katika semina hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya
viwango Zanzibar Mwadini Khatib Mwadini alieleza kuwa taasisi yake itaendeleza
mashirikiano na wafanyabiashara na waingizaji wa bidhaa mbali mbali ili
kuhakikisha malengo ya taasisi yake ya kudhibiti ubora wa bidhaa linatimia.
Alisema
katika kufikia lengo hilo taasisi hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa uma na kuandaa
viwango vya bidhaa mbali mbali zinazozalishwa au kuingizwa nchini ambapo hadi
sasa taasisi hiyo imeshaandaa viwango vya bidhaa 113 vikiwemo vya bidhaa za
mafuta.
“Mbali
ya viwango hivyo lakini pia tumefanikiwa kuwa na maabara ya kisasa inayoweza
kupima bidhaa za vifaa vya kieletroniki na mafuta aina zote na tumefanya yote
hayo ili kuhakikisha malengo yetu yanayoenda sambamba na malengo ya taifa ya
kukuza biashara na ujasiriamali, kudhibiti ubora wa bidhaa na usalama wa
watumiaji wa bidhaa hizo yanatimiake”, alisema Mwadini.
Akiwasilisha
mada katika semina hiyo Afisa Viwango wa taasisi ya viwango Zanzibar Mukhtar Chande
Muumin alieleza kuwa taasisi hiyo baada ya kuandaa viwango vya matairi na kupitishwa na bodi ya wadhamini inatarajia
kuanza ukaguzi wa matairi yanayotarajiwa kuingizwa nchini kuanzia April 1 mwaka
huu.
“Kuanzia
tarehe hiyo waingizaji na wauzaji wote wa matairi ya vyombo vya moto wanatakiwa
kufuata utaratibu na kutumia mahitaji yaliyoelekezwa katika viwango kama fursa
pekee ya kuweza kushajihisha matumizi bora na kuijengea jamii na serikali
kuepukana na athari zinazoweza kuepukika”, alisema Muumin.
Wakitoa
maoni yao katika semina hiyo baadhi ya wafanyabiashara wa matairi walioshirikia
semina hiyo waliitaka taasisi hiyo kupunguza ada ya ukauzi iliyopangwa ili
kuondoa ongezeko la gharama za uendeshaji wa biashara yao.
Aidha
waliitaka taasisi hiyo kuendeleza mashirikiano na jumuiya za wafanyabiashara
pamoja na kukaa na taasisi nyengine zinazohusika na utozaji wa kodi ili
kupunguza viwango vya tozo mbali mbali ambzo zinachangia kwa kiasi kikubwa
ukuzaji wa gharama na kudumaza biashara zao.
“Tunaamini
nchi yetu imekuwa ikihimiza ujasiriamali, na wafanyabiashara wengi tunaofanya
biashara hii ni wale wadogo wadogo hivyo ada ya shilingi 5,000 kwa kila tairi
iliyopendekezwa ni kubwa na kwamba haitosaidia kukuza biashara zetu bali
kuididimiza na kupelekea kumkandamiza mtumiaji wa mwisho wa bidhaa hizo”,
alisema waziri mbonde.
Nae
mwakilishi wa jumuiya ya wafanyabiashara, wenye viwanda na wakulima Zanzibar aliishauri
taasisi hiyo kuzingatia maoni ya wadau hao ikiwa pamoja na kusogeza muda wa
kuanza kutumika kwa utaratibu kutoka mwezi aprili hadi julai mwaka huu ili
kutoa muda kwa wafanyabiasha hao kujipanga.
“Mimi
naamini ZBS (taasisi ya viwango Zanzibar) haijaweka viwango hivi kwa ajili ya
kupata mapato hivyo ni vyema viwango vya ada vikapitiwa upya lakini pia na muda
wa kuanza kwa zoezi hili ili kuwapa muda wadau kujiandaa na kulielewa kwa kina hii
dhana ili kuwasaidia kuja kulitekeleza bila ya vikwazo”, alisema Dk. Hafidh
kutoka ZCAA
Semina
hiyo iliyolenga kutoa elimu kwa wafanyabiasha wa matairi nchini iliandaliwa na ZBS
kwa lengo kujenga uelewa wa pamoja juu ya aina na viwango vya matairi
yanayoingizwa nchini ili kupunguza ajali na athari za kimazingira
zinazochangiwa na bidhaa zilizo chini ya ubora na viwango.
Mwisho.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Ali Khamis Juma akifungua semia ya kujenga uelewa wa wafanyabiashara ya matairi ya magari na vyombo vya moto iliyoandaliwa na taasisi ya viwango Zanzibar.
Washiriki wa semina ya semia ya kujenga uelewa wa wafanyabiashara ya matairi ya magari na vyombo vya moto iliyoandaliwa na taasisi ya viwango Zanzibar (ZBS) kuhusu utaratibu wa ukaguzi wa viwango vya bidhaa hizo unaotarajiwa kuanza mwezi April mwaka huu.
No comments:
Post a Comment