Saturday, February 24, 2018

ZANZIBAR HEROES WAKABIDHIWA VIWANJA WALIVYOAHIDIWA

NA MWINYIMVUA NZUKWI
Serikali ya Zanzibar imekabidhi viwanja 33 kwa wachezaji na viongozi wa makamo bingwa wa mashindano ya chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes) ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein aliyoitoa Disemba 24 mwaka jana.

Hafla hiyo iliyoshuhudiwa na waziri wa habari, utamaduni, utalii na michezo Rashid ali juma, iliongozwa na waziri wa ardhi, maji, nishati na mazingira salama adoud talib katika eneo la Tunguu plan wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Akikabidhi hati na maeneo ya viwanja hivyo, waziri salama aliwataka wachezaji hao kuzingatia usia uliotolewa na Dk. Shein wa kuvienzi kwa kuvijenga viwanja hivyo ili kufaidi matunda ya jasho lao.

“Serikali inathamini michezo na nguvu mlizotumia wakati mnapigania heshima ya nchi yetu, hivyo nawakumbusha kuwa Rais (Dk. Ali Mohamed Shein) hatofurahi atakaposikia mmeviuza na hamkuvijenga”, alisema Waziri huyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, waziri juma alisema anashukuru kuona historia nyengine inaandikwa katika medani ya soka na kuwataka wachezaji hao kuendelea kujituma na kulinda viwango vyao katika timu zao wanazozitumikia.

“ninashukuru kuona kuwa serikali imetimiza ahadi yake kama ilivyoiweka. Sasa ni jukumu na wajibu wetu kuendelea kutumia vyema nguvu na akili zetu katika kuendeleza michezo nchini”, alisema Rashid.

Kocha mkuu wa Zanzibar heroes Hemed Suleiman ‘Morocco’ akitioa shukrani kwa niaba ya viongozi na wachezaji wa timu hiyo alimshukuru Rais Dk. Shein na viongozi wengine wa serikali kwa kutimiza ahadi hiyo na kuahidi kuendelea kuikumbuka siku hiyo miaka mingi ijayo.

“Hiki tunachokishuhudia hapa ni deni ambalo linaweza kuchukua muda mrefu kulilipa lakini tunaomba mumfikishie salam zetu za shukrani na ahadi ya kwamba tutaitunza zawadi hii na kuithamini siku zote”, alisema Morocco.


Viwanja hivyo ni zawadi ya 4 kwa wachezaji hao kutoka kwa Dk. Shein baada ya chakula cha mchana, hafla maalum katika taarab rasmi na fedha taslim shilingi milioni 3 kwa kila mmoja baada ya timu hiyo kushika nafasi ya pili katika mashindano hayo baada ya kutolewa na wenyeji Kenya kwa penalti 3 – 2 baada ya timu hizo kutoka sare ya magoli 2 – 2 ndani ya dakika 120.


Mlinda mlango wa timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ Ahmed Salula (wa pili kulia) akipokea hati ya kiwanja chake kutoka kwa Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Abod Talib (kushoto). Anaeshuhudia ni waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Rashid Ali Jumba (wa pili kushoto).

Kikosi cha timu ya Zanzibar Heroes kilichoshiriki fainali za challenji ya wakubwa ya CECAFA mwaka 2017 na kumaliza ya pili nyuma ya Harambee Stars ya Kenya.

No comments:

Post a Comment