Saturday, February 24, 2018

'SAND HEROES' USO KWA USO NA WA-AFRIKA KUSINI UFUKWENI KESHO

Na Mwinyimvua Nzukwi
Kocha mkuu wa Mabingwa wa mashindano ya Copa Dar es salam katika soka la ufukweni timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Sand Heroes’ Ali Sharif Adolf  ameeleza kuwa kikosi chake kipo imara kukikabili kikosi cha timu ya taifa ya afrika kusini katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaochezwa Februari 25 mwaka huu katika fukwe za Bububu nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Mchezo huo ambao ni sehemu ya maandalizi ya timu ya Afrika Kusini kwenye changamoto ya kuwania kufuzu katika mashindano ya kombe la dunia, yatatumiwa na  ‘Sand Heroes’ kama maandalizi ya tamasha la mchezo huo linalotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu kama ilivyoshauriwa na rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein alipokuwa akipokea kombe lililochukuliwa na timu ya Zanzibar mwaka uliopita.

Adolf ambae pia ni mwenyekiti wa kamati ya soka la ufukweni Zanzibar alisema lengo la tamasha hilo litakaloshirikisha nchi mbali mbali za ndani na nje ya afrika ni kuitangaza Zanzibar kupitia mchezo huo na kujiimarisha katika viwango vya FIFA.

alisema maandalizi yote yanayohusiana na mchezo huo yamekamilika na Kwamba ameridhishwa na viwango vya wachezaji wake ambao anaamini wataonesha mchezo wa urafiki kwa lengo la kukuza mahusiano kati ya nchi mbili hizo.

“Mchezo huu ni mchezo wa bahati na fursa kwa wale ambao wamekosa bahati ya kushiriki katika soka la kawaida, nadhani tukiitumia vyema fursa hii itasaidia kuitangaza nchi na wachezaji wake na ndio maana tunamtaka kila mmoja wetu aje kushuhudia mchezo huo”, alisema.

Akizungumzia mchezo huo, kocha wa afrika kusini Ntokozo Bhengu alisema wachezaji wake wapo fiti na wana ari kubwa ya mchezo huo.

 “Mbali ya kuamini kuwa tutapata ushindani wakati wa mchezo, lakini tunapaswa kujua kuwa nchi zetu ni marafiki na sisi tumekuja kujifunza utamatuni wa mchezo huu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki baada ya kuwa na uzoefu mkubwa katika mashindano ya ukanda ya COSAFA”, alisema kocha Bhengu.

Alisema amevutiwa na mwaliko waliopewa na kukutana na Zanzibar kutokana na kuwa Zanzibar inashika nafasi ya karibu na nchi yake katika viwango vya FIFA, hivyo anaamini mchezo huo utakuwa na ushindani utakaomsaidia kuimarisha kikosi chake.

Nae Mkuu wa msafara wa timu ya taifa ya Afrika Kusini Ngwenya Kwezakwakhe alielezea kufurahishwa kwa mapokezi na huduma walizopatiwa toka walipowasili na kutoa mwaliko kwa timu ya Zanzibar kufanya ziara kama hiyo nchini kwao.

“Tumehudumiwa vyema toka tulipowasili na kushuhudia sehemu kubwa ya ukarimu wenu kwa wageni na ninaamini hata kama tukipoteza mchezo huu itakuwa ni kwasababu za ushindani na sio mambo mengine”, alisema Kwezakwakhe.


Timu ya Afrika Kusini iliwasili Zanzibar Ijumaa ikiwa na wachezaji 11 na viongozi 7 kwa ajili ya mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya wenyeji wao ‘Sand Heroes’ baada ya timu ya mchezo huo ya Oman kushindwa kujibu mwaliko uliotolewa na Kamati inayosimamia mchezo huo visiwani humu.


Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Zanzibar Ali Shari ‘Adolf’ (kulia) na kocha mkuu wa timu ya taifa ya afrika kusini Ntokozo Bhengu (kushoto) wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya timu hizo utakaochezwa Jumapili Februari 25, 2018 katika ufukwe wa bahari ya Bububu, Zanzibar. 

No comments:

Post a Comment