Sunday, February 25, 2018

WAHIMIZWA USAFI, MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA

NA MWINYIMVUA NZUKWI
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka wananchi kuwa na utamaduni ya kufanya usafi katika njia za kupitishia maji machafu na kufuata sheria za matumizi bora ya ardhi ili kuondokana na athari ya mafuriko.

Ayoub ameyasema hayo wakati aliposhiriki katika zoezi la usafi wa mazigira lililoandaliwa na kundi la ‘Safari ya CCM 2020’ na Manispaa ya wilaya ya Magharibi "A" uliofanyika  Mwera Meli sita Wilayani humo.

Alisema mvua za masika zinatarajiwa kunyesha hivi karibuni zimekuwa zikisababaisha maafa makubwa kwa watu na mali zao kila mwaka hivyo kila mwananchi anawajibu wa kuchukua tahadhari juu ya suala usafi.

“Kwa wale wanaoishi sehemu za mabondeni kuna haja ya kuchukua hatua za tahadhari kwa kuanza kuhama katika maeneo hayo na kufanya usafi wa mara kwa mara hasa katika njia za maji ili kupunguza athari”, alisema Ayoub.

Aidha aliuomba uongozi wa kundi la ‘Safari ya CCM 2020’ kuendeleza utamaduni wa kushiriki katika shughuli mbali mbali za kijamii na kisiasa ili kusaidia mabadiliko ya tabia na fikra kuhusiana na swali la usafi wa mazingira yanayowazunguka.

“Ninawapongeza kwa juhudi mnazochukua katika kusaidia mabadiliko ndani ya jamii yetu, hivyo ningewaomba kuweka mkazo wa kushajiisha mabadiliko ya fikra hasa katika maswali ya usafi wa mazingira lakini pia kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambanodhidi ya rushwa na uhujumu uchumi”, alieleza Ayoub.

Akizungumzia masuala ya rushwa na uhujumu wa uchumi afisa uchumguzi wa mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu wa uchumi Yussuf Juma aliitaka jamii kuchukia vitendo vya rushwa na kuwa tayari kuvitolea taarifa katika taasisi yake ili kudhibiti athari za uovu huo.

“Mapambano dhidi ya rushwa ni ya jamii nzima lakini kwa wanachama wa CCM (Chama cha Mapinduzi) hili ni kipaumbele namba moja kwa kuwa katiba na ilanoi ya uchaguzi ya 2015 – 2020 imeeleza wazi kuwa itazielekeza serikali zake kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi hivyo kila mmoja ahakikishe anapiga vita rushwa iwe ndani au nje ya chama”, alisema Yussuf na kuitaka jamii itwayo kuunga mkono kampeni ya FUNGUKA kwa kupiga simu namba 113 kutoa taarifa za rushwa.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Keptaini Khatib Khamis Mwadini alisema kuwa serikali ya Wilaya yake imeanzisha utaratibu maalum wa kufanya usafi kwa kila Shehia katika kila jumamosi ya mwisho wa wiki ili kuondokana na maradhi ya mripuko.

Alisema hatua ya wanakikundi hao kuamua kufanya kampeni hiyo ya usafi pamoja na kuchangia damu ni jambo jema linalopaswa kupongezwa kwa kuwa litaokoa maisha ya watu wengi bila ya kujali itikadi zao.

Mapema asubuhi makundi mbali mbali yakiwemo ya wafanyakazi wa manispaa ya magharibi ‘A’, masheha wa shehia za wilaya hiyo, wanachama wa ccm wa matawi yaliyomo wilayani huo na wananchi wa kawaida waliungana kusafisha maeneo mbali mbali ya eneo la mwera meli sita liliopo jirani na ofisi za mkuu wa wilaya hiyo na kuchagia damu. 

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud  (kushoto) akifagia wakati wa zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo ya Mwera Meli sita Wilaya ya Magharibi 'A' Unguja. Kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Kepteni Khatib Khamis Mwadini.

Wafanyakazi wa Manispaa ya Magharibi 'A' na wananchi wa wilaya ya Magharibi 'A' wakiendelea na kazi ya usafi wa mazingira  karika barabara ya Mwera Meli sita wakati wa kampeni ya usafi iliyoandaliwa na kundi la 'Safari ya CCM 2020'.

Mkuu wa Mkoa wa mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud (kushoto) akisalimiana na mmoja ya wanachama wa kundi la 'Safari ya CCM 2020' wakati kundi hilo lilipoandaa kampeni ya usafi wa mazingira katika maeneo ya Mwera Meli sita, Wialya ya MaghariBI 'A' Unguja. 


No comments:

Post a Comment