NA MWINYIMVUA NZUKWI
JUMLA ya maswali 74 yaliyoratibiwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar
yanatarajiwa kuulizwa na kupatiwa majibu katika mkutano wa 9 wa baraza la wawakilishi Zanzibar utakaoanza Februari 7 mwaka huu.
Katibu wa baraza hilo Raya Issa Mselem amewaambia waandishi
wa habari ofisini kwake chukwani kuwa maswali hayo yameulizwa na wajumbe wa
baraza ambao watapata nafasi ya kuuliza maswali mengine ya nyongeza kwa mujibu
wa kanuni.
Amesema pamoja na maswali hayo baraza litapokea na kujadili ripoti
za kamati za kudumu za baraza kwa mwaka 2017/2018 na miswaada mitatu ya sheria
ukiwemo mswada wa kufuta sheria ya adhabu na kutunga sheria mpya ya adhabu,
kuweka masharti bora Zaidi pamoja na mambo mengine yanayohusiana nayo.
“Mswada mwengine ni mswada wa sheria ya mwenendo wa makosa ya
jinai namba 7 ya mwaka 2004 na kutunga sheria ya mwenendo wa jinai na kuweka
utaratibu bora wa upelelezi wa makossa ya jinai na usikilizaji wa kesi za jinai
na mambo mengine yanayohusiana na hayo”, alieleza katibu Raya.
Aliutaja mswada mwengine wa sheria utakaowasilishwa katika
mkutano huo kuwa ni wa kufuta sheria ya
kusimamia mwenendo wa biashara na kumlinda mtumiaji ya Zanzibar namba 2 ya 1995
na kutunga sheria mpya ya ushindani halali wa biashara na kumlinda mtumiaji,
kuweka masharti bora Zaidi pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Aidha Raya alieleza kuwa katika mkutano huo serikali itawasilisha
taarifa ya mwelekeo wa mpango wa taifa, ripoti kuhusu hoja binafsi ya mjumbe wa baraza hilo Mohammed Said
Mohammed ‘Dimwa’ kuhusu kuweka miundombinu bora kwa watu wenye ulemavu katika
maeneo ya umma na taarifa ya wajumbe wanaoliwakilisha baraza hilo katika bunge la jamhuri ya
muungano wa Tanzania.
“Pia tunatarajia serikali itatoa ripoti kuhusu maombi ya
wananchi wa Kisakasaka Zanzibar kuhusu namna wanavyoweza kufaidika kutokana na
machinjio yaliyopo kwenye maeneo yao pamoja kama yalivyowasilishwa katika
mkutano wa mwezi Disemba”, alieleza.
Katika mkutano uliofanyika Disemba mwaka uliopita, Mwakilishi wa jimbo la Mpendae Mohammed Said Mohammed aliwasilisha maombi hoja
binafsi yenye maombi ya kupatikana kwa sehemu ya mapato yanayopatikana katika
eneo la Kisakasaka ili kuyaendeleza maeneo hayo kutokana na shughuli
zinazoendeshwa katika eneo lao ambazo zimekuwa na madhara kwa mazingira na
maendeleo ya jamii.
Huu ni mkutano wa 9 toka kuzinduliwa kwa baraza la 9 la Wawakilishi Zanzibar lililopatikana baada ya uchaguzi mkuu wa zanzibar mwezi Machi 2016 baada ya kufutwa kwa uchaguzi wa awali uliofanyika Oktoba 25, 2015 na tume ya uchaguzi Zanzibar.
Huu ni mkutano wa 9 toka kuzinduliwa kwa baraza la 9 la Wawakilishi Zanzibar lililopatikana baada ya uchaguzi mkuu wa zanzibar mwezi Machi 2016 baada ya kufutwa kwa uchaguzi wa awali uliofanyika Oktoba 25, 2015 na tume ya uchaguzi Zanzibar.
No comments:
Post a Comment