Na Mwinyimvua Nzukwi
Familia ya askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) Issa Saleh Issa aliyefariki akiwa matibabuni nchini Uganda imepatiwa msaada wa fedha taslim na vitu mbali mbali vya matumizi ya nyumbani kama kifuta machozi kutokana na msiba wa ndugu yao.
Askari huyo ni miongoni mwa askari 15 wa JWTZ waliofariki wakiwa katika shughuli za ulinzi wa amani nchini Congo mnamo mwaka uliopita alihamishiwa nchini Uganda kwa matibabu zaidi kabla ya kufariki kwake na kutimiza idadi ya askari 10 waliotokea Zanzibar.
Akikabidhi msaada huo kwa baadhi ya ndugu wa marehemu akiwemo mjane wa marehemu, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mjini Magharibi Hamida Mussa Khamis alisema msaada huo uliotolewa na kampuni ya Rom Solutions umelenga kuisaidia familia hiyo kukabiliana na changamoto mbali mbali yaliyosababishwa na kifo cha askari huyo.
Hamida alieleza kuwa kama ilivyokuwa kwa askari wengine, kampuni hiyo kupitia serikali ya mjkoa wake imeamua kutoa msaada huo ili kutambua mchango wa askari hao katika ulinzi wa taifa na kuitaka familia kuendele kuwa wamoja.
Alisema serikali kuu na ya mkoa huo itaendelea kufuatilia maendeleo ya familia hizo na kuzitaka kuwa karibu na ofisi yake iwapo kutatokea jambo linalohitaji msaada ili kupunguza ukubwa wa pengo lililoachwa na marehemu hao aliowataja kuwa ni mashujaa wa taifa.
Katika makabidhiano hayo yaliyofanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, kampuni hiyo iliwakilishwa na Mkurugenzi wa kampuni hiyo Viorica Enescu aliewataka wafiwa kuendelea kuwa na subira kwa kuwa jamii ya kimataifa inatambua kazi iliyofanywa na ndugu yao.
Mnamo Disemba 18 mwaka jana kampuni hiyo ilikabidhi msaada kama huo kwa familia kwa familia za askari 9 waliozikwa Zanzibar uliokisiwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi 10 na kuahidi kutoa ya kutoa msaada wakati wa maziko ya askari huyo.
Disemba 8 mwaka uliopita Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutterres alitangaza vifo vya askari 14 wa JWTZ waliokuwa sehemu ya jeshi la kulinda amani la umoja wa mataifa nchini Congo DR baada ya shambulizi la kushitukiza linalodaiwa kufanywa na waasi wa serikali ya nchi hiyo na kupelekea askari 44 kujeruhiwa vibaya akiwemo Issa aliefariki mwezi mmoja baadae.
Mkurugenzi wa kampuni ya ROM Solution Viorica Enescu (katikati) akimfariji mjane wa askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) Issa Saleh Issa (kushoto). Wa kwanza kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mjini Magharibi Hamida Mussa Khamis.
No comments:
Post a Comment