NA
MWINYIMVUA NZUKWI
WIZARA
ya Habari, Utamaduni, Utalii na michezo imesema kutekelezwa kwa mkataba wa utoaji
wa huduma kwa wateja utasaidia kuimarisha utendaji na utawawala bora ndani ya
wizara hiyo.
Akiwasilisha rasimu ya mkataba huo kwa wadau wa wizara hiyo, watendaji
wa idara na wakuu wa vitengo Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji na Utumishi Joseph
Kilangi alisema lengo la mkataba huo pia ni utekelezaji wa programu ya
kuimarisha utumishi wa umma yam waka 2000.
Alisema programu hiyo inazitaka taasisi za umma kuweka kwa uwazi
misingi ya huduma zinazotoa na kuweka viwango vya utoaji wa huduma na kuwataka
wadau hao kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo.
Alisema kukamilika kwa mkatàba huo kutawasaidia wadau wa wizara
hiyo kukuza kupata huduma bora na kuwa tayari kupeleka malalamiko yao kwa katibu
mkuu wa Wizara hiyo pale wanapokosa huduma wanazostahiki.
“Wapokea huduma kutoka katika taasisi zilizomo katika wizara
yetu wanatakiwa kwa mujibu wa mkataba huu kuwasilisha malalamiko yao juu ya kutoridhishwa
na huduma zinazotolewa ili kuzipatia ufumbuzi lakini pia watendaji wanatakiwa
kuutekeleza mkataba huu kikamilifu”, alieleza Kilangi.
Alisema chini ya mkataba huo, mteja atakuwa na haki ya kupatiwa
mrejesho wa malalamiko atakayoyawasilisha, kupatiwa huduma kwa haraka na katika
muda mfupi na kupatiwa huduma anayoihitaji bila ya ushawishi au kutoa rushwa na
zawadi.
Wakiichangia rasimu hiyo
wadau hao waliitaka wizara hiyo kuwa na vipimo vya muda katika majukumu
waliyojipangia kuyatekeleza ili iwe rahisi wadau kujua namna ya kupata au kudai
huduma zinazotolewa na taasisi za wizara hiyo.
Walisema pamoja na mkataba huo kuwa na maelezo ya jumla katika
majukumu ya idara na vitengo vya wizara hiyo ni vyema vitengo hivyo
vingeanishiwa majukumu mahsusi ili iwe rahisi kuwajibika juu yake.
“wizara ina majukumu makubwa na ingekuwa vyema kama kila kitengo
kingeeleza mambo yatakayoyafanya na kuwa ni ahadi ili mwisho wa siku iweze
kupimwa kutokana na mipango hiyo”, alisema usi mohammed usi kutoka wizara ya
nchi ofisi ya rais, tawala za mikoa, serikali za mitaa na idara maalum za SMZ.
Aidha wadau hao waliitaka wizara hiyo kuzingatia kwa kina
majukumu ya kila idara na kuhakikisha zinaweshwa kwa kupatiwa mafunzo na bajeti
ya kutosha ili wawe na uwezo wa kutekeleza mkataba huo kikamilifu.
Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za wajumbne wa kikao hicho
kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano ya wizara hiyo kikwajuni, afisa
utumishi kutoka tume ya utumishi Zanzibar maulid sheha alisema uanzishwaji wa
mikataba hiyo ni sehemu ya utekelezaji katika sekta ya utumishi wa umma na
kwamba maoni yaliyotolewa na wadau hao yatazingatiwa.
“Tafiti mbali mbali zimebainisha uwepo wa ufanisi katika
utumishi wa umma mahali ambapo kuna mikataba ya utoaji huduma kwa wateja kwani
watumishi wote huwa wamejifungamanisha na mikataba hiyo na wateja huwa na
nafasi ya kulalamika pale wanapoona hawajatendewa haki”, alisema ofisa huyo.
Mkurugenzi wa idara ya uendeshaji na utumishi katika wizara ya Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo Joseph Kilangi akiwasilisha rasimu ya mkataba wa
utoaji huduma kwa wateja wa wizara yake kwa wadau wa wizara hiyo.
Afisa utumishi wa idara ya utumishi serikalini Maulid Shehe akitolea
ufafanuzi baadhi ya hoja zilizotolewa na wajumbe waliohudhuria kikao cha
kupitia rasimu ya mkataba wa utoaji wa huduma kwa wateja wa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo (WHUUM).
Baadhi ya wajumbe walioshiriki kikao cha kupitia rasimu ya mkataba wa utoaji wa huduma kwa wateja wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo (WHUUM) Zanzibar.
No comments:
Post a Comment