NA MWINYIMVUA NZUKWI
Makamo wa pili wa Raisi Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi amewataka majaji na Mahakimu kuendesha kesi kwa haraka ili wananchi
wanufaike na haki zao za msingi juu ya mashtaka wanayoyafungua.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya
Shamrashamra za Siku ya sheria huko katika Viwanja vya Misara Mjini Unguja
Balozi Seif amesema kumekuwa na malalamiko mengi kwa wananchi juu ya
kucheweshwa kesi katika kupewa hukumu.
Amesema kutolewa hukumu kwa wakati kutawawezesha
wananchi kuendelea kuripoti kesi mbalimbali zinazotokea katika jamiii ili
kuzuia wimbi la wavunjifu wa sheria.
Hata hivyo balozi seif amewataka wananchi kutumia
vyema fursa ya maonesho hayo katika kujifunza sheria pamoja na
kupeleka malalamiko yao kwa kwa mawakili mbalimbali waliopo ili waweze
kutatuliwa matatizo ya kesi zao.
Amesema kuna wimbi kubwa la wananchi hawajui sheria
jambo ambalo linasababisha kushindwa kukata rufaa baada ya kutoridhika na
hukumu inayotolewa na mahakama juu ya mashtaka wanayofungu jambo ambalo
linapelekea kukosa haki zao pamoja na kulalamika mitaani.
Aidha balozi iddi ametowa wito kwa Mahakama kuwa na
utamaduni wa Kufungua maonesho hayo mwaka kila mwaka ili kuwawezesha wananchi
kujifunza sheria za nchi yao.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othaman
Makungu amesema lengo la kuwepo kwa Maonesho hayo kutowa elimu ya sheria kwa
wananchi ili kujua haki zao na namna ya kufuatilia mashtaka yao mahakamani.
Amesema katika kuhakikisha elimu hiyo inawafikia
walengwa Maonesho hayo pia yameshirikisha wafanya biashara mbali mbali
kujifunza elimu ya sheria pamoja na kuuza na kutanga bidhaa zao hali hiyo
inaenda sambamba na kauli mbinu ya siku ya sheria inayolengwa kuimarisha 'Utawala wa sheria kwa kukuza Uchumi wa Nchi'.
Siku ya sheria inatarajiwa kufikia kilele Februari 12
mwaka huu, ambapo kwa Zanzibar maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika
ukumbi wa zamani wa Baraza la wawakilishi Mjini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif (wa pili kushoto) akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa Maonyesho ya Siku ya Sheria Zanzibar katika Viwanja vya Maisara Suleiman Mjini Zanzibar. Wa kwanza kushoto ni Naibu waziri wa nchi ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utawala bora na Utumishi wa Umma Khamis Juma Mwalim na wa kwanza kulia ni Jaji mkuu wa Zanzibar Omar othman Makungu.
No comments:
Post a Comment