Friday, February 9, 2018

MICHE 5000 YA MIKOKO YAPANDWA KISAKASAKA

NA MWINYIMVUA NZUKWI
ZAIDI ya miche 5,000 ya miti ya mikoko imepandwa  katika  shehia  ya   Kisakasaka na bondeni wilaya ya Magharibi ‘B’ unguja ikiwa  ni sehemu mikakati ya utunzaji  wa  mazingira  katika  maeneo  mbalimbali  ya  mkoa  wa  Mjini Magharibi.

Zoezi hilo lililoendeshwa kwa ushirikiano kati ya baraza la Manispaa ya Magharibi ‘B’ na Jumuiya ya Utunzaji wa Mazingira ya Kisakasaka (JUMKISA) ambapo Mkururugenzi wa baraza  hilo Amour Ali Mussa alisema baraza lake litaendeleza ushirikiano uliopo kati yake na jumuiya za kiraia zilizomo ndani ya manispaa hiyo ili kufikia malengo yao.

Alisema ushirikiano huo utasaidia kufikiwa kwa malengo mbali mbali yaliyowekwa na baraza lake la kuweka maeneo kaika hali ya usafi na usalama sambamba na kuhifadhi mazingira kama moja ya njia za kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa wakaazi wa manispaa yake.

Alisema baraza  lake   limeandaa  mikakati  ya kuhakikisha linaweka  mazingira  mazuri  kwa  wananchi  wake  wa   hususani vijana ili kuepukana na madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza katika zoezi hilo lililoendeshwa katika fukwe ya bahari ya Kisakasaka shehia ya Kombeni  wilayani humo Naibu  Katibu wa ‘JUMKISA’  Iddi Hassn Ali  aliwaomba   wananchi wanaoishi katika maeneo hayo na viongozi  wa  kiserikali kujenga utamaduni  wa   kutembelea sehemu mbali mbali za kitalii ili  kuendeleza dhana ya utalii wa ndani.

Nae Diwani wa wadi ya Kibondeni Shabaani Mwinyi Ali Aliwataka wananchi wanaojihusisha na kilimo cha mbogamboga kuacha tabia ya kukata mikoko inayotunza mazingira ya bahari hiyo kutokana na kuwa kitendo hicho kinaviza juhudi zinazochukuliwa za kulihifadhi eneo hilo.



Sehemu ya upwa wa pwani ya Kisakasaka iliyopandwa miti ya aina ya mikoko ili kuzuia mawimbi ya bahari yasipande katika maeneo ya juu ya ardhi ikiwa ni sehemu ya mikakati ya utunzaji wa mazingira ya eneo hilo.

No comments:

Post a Comment