NA MWINYIMVUA NZUKWI
Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kutofumbia macho vitendo vya
ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto ili kukomesha vitendo
hivyo ndani ya jamii.
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa wito
huo katika tamasha la uchangiaji damu pamoja na uzinduzi wa jumuiya ya maendeleo ya vijana na wanawake (BIWO) katika viwanja vya Mnara wa kumbukumbu ya Mapinduzi
Michenzani na kueleza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua za kisheria.
Alisema iwapo jamii itaondoa
muhali na kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na asasi za
kiraia, tatizo hilo linaweza kukomeshwa na kustawisha maisha ya wananchi na taifa
kwa ujumla.
“Tukiwa tayari tunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa madhara ya vitendo
vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia sambamba na matumizi ya dawa za
kulevya hivyo naviagiza vyombo vinavyohusika na ufuatiliaji na usimamizi wa
sheria ni lazima vifanye kazi kwa haki na kuchukua hatua stahiki kwa watu
wanaohusika na uovu huuu”, alieleza Balozi Seif.
Aidha aliipongeza jumuiya ya BIWO kwa uamuzi wao ywa kuanzisha
kampeni ya uchangiaji damu kwa hiyari jambo alilosema linaenda sambamba na azma
ya Serikali ambayo kupitia misaada na ushirikiano na wafadhili mbalimbali imechukua juhudi za kuanzisha benki ya damu ili kuhakikisha uhakika wa damu kama moja ya njia za
kuimarisha huduma za afya ya jamii.
“Utaratibu wa kuchangia damu
ni wa duniani kote hivyo hatua hii itasaidia kupatikana kwa damu
ambayo itatumiwa katika hospitali
mbalimbali ambako mahitaji hujitokeza ikiwemo kuwasaidia kina mama wanapotaka
kujifungua kwani hupoteza damu nyingi pamoja na panapotokea majanga ya kitaifa
au ajali”, alisisitiza Balozi Seif.
Mapema akimkaribisha Mkamo wa pili wa Rais, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi
Ayoub Mohammed Mahamoud alisema serikali ya Mkoa wake imekuwa ikiunga
mkono jumuiya mbalimbali zenye lengo la kuhakikisha
utetezi wa haki, usawa na ustawi wa wananchi kwani kufanya hivyo kunaongeza
kasi ya maendeleo taifa.
“Wazo la hili linaenda sambamba na azma ya serikali ya kuimarisha
ustawi wa wananchi wetu na ndio maana ndani ya mkoa wetu tulianzisha kampeni ya
MIMI NA WEWE ili kuimarisha dhana ya uzalendo kama ilivyokuwa katika miaka ya
nyuma”, alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Uzinduzi wa Jumuiya hiyo
ulienda sambamba na kampeni ya uchangiaji wa damu kwa hiyari kwa ushirikano na
benki ya damu Zanzibar ambapo hadi majira ya saa 6:45 jumla ya chupa 375 za
damu zilikwishapatikana kati ya chupa 1000 zilizokadiriwa.
Kwa mujibu wa benki ya damu Zanzibar wastani wa chupa 75
zinakadiriwa kutumika kila siku katika hospitali mbali mbali Zanzibar kwa watu
wanaohitaji tiba ya kuongezewa damu ambapo katika kamperni kama hiyo mwaka chupa
500 za damu zilipatiakana.
Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akiwakagua
baadhi ya watu walijitokeza kuchangia damu katika tamasha la uzalendo
lililoandal;iwa kwa pamoja na jumuiya ya maendeleo ya wanawake na vijana (BIWO)
na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi. anayemfuatia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud.
No comments:
Post a Comment