NA MWINYIMVUA NZUKWI
Serikali ya Zanzibar imeeleza kuwa inatambua na kuthamini
mchango unaotolewa na asasi za Kiraia (AZAKI) katika kuisaidia juhudi zake za kukabiliana
na umaskini, demokrasia na utawala bora nchini.
Akifungua kongamano la pili la asasi za kiraia Zanzibar
katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Idi alilisema shughuli zinazotekeleza na jumuiya hizo zina mchango
mkubwa katika ujenzi wa taifa na kuwataka wasimamizi wa asasi hizo kuzidisha ushirikiana
na serikali kwa lengo la kuchochea kasi ya maendeleo ya wananchi kiuchumi,
kisiasa na kijamii.
Balozi Seif alisema ili kufikia maendeleo ya kweli
na ya haraka ipo haja kwa pande mbili hizo kushirikiana na kuzingatia wajibu wa kuijenga nchi kwa
mujibu wa katiba ya nchi, sheria na katiba za jumuiya hizo.
“Pamoja na kutambua mchango wenu kwa maendeleo ya
nchi yetu, bado nawatahadharisha kuwa serikali haitokuwa tayari kuziona asasi
zenu zinafanya kazi kinyume na katiba zao au taratibu
zilizojipangia zenyewe kwani uzoefu wa majukumu ya taasisi za kiraia umetoa
mafunzo mengi na kupelekea baadhi ya taasisi kukiuka madili yao”, alisema Makamu
wa Rais.
Aidha aliwahakikishia washiriki wa kongamano hilo ambalo ni
sehemu ya mpango wa kuzisaidia asasi za kiraia Zanzibar (ZANSAP) unaotekelezwa
kwa pamoja kati ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Umoja wa Ulaya
(EU) kwamba serikali ipo tayari kuyafanyia kazi mapendekezo yote yatakayotolewa
mwisho wa kongamano hilo.
“Napenda niwahakiishie kuwa serikali ipo tayari kupokea maazimio
mtakayoyafikia mwisho wa kongamano hili kwa kuamini kuwa yatasaidia kwa kiasi
kikubwa kuimarisha utawala bora sambamba na jamii kupata nguvu za kupambana
dhidi ya umaskini kutokana na shughuli za ujasiriamali zinazotekelezwa na
baadhi ya azaki”, alisisitiza.
Mapema Mwenyekiti wa Kongamano hilo Dk. Mzuri Issa Ali
aliishukuru serikali ya Zanzibar kwa kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi
wa asasi za kiraina na kuiomba kuwa na uratibu taasisi zao iliziweze kufanya
kazi kwa pamoja na kufokiwa kwa malengo ya kuanzishwa kwao yafikiwe.
Alisema katika muungano wa azaki zinazoshiriki
kongamano hilo zipo zinazojihusisha na kazi za kufanya utafiti, kutoa elimu na
huduma za jamii ambazo ni chimbuko la mafanikio na maendeleo ya wananchi.
“Katika kongamano hili tutapata fursa ya kupokea na
kujadili mada sita muhimu zilizojikita katika utekelezaji wa majukumu yetu ya
kila siku ambazo ni zitatoa hali halisi ya taasisi zetu katika utekelezaji
wa mipango ya kitaifa kama vile mkakati wa kupunguza umaskini Zanzibar awamu ya
tatu (MKUZA III) pamoja na mpango wa kusaidia biashara zinazojitokeza kwa
Wajasiriamali”, alisema Dk. Mzuri ambae pia ni mkurugenzi wa chama cha
wanahabari wanawake Tanzania (TAMWA) ofisi ya Zanzibar.
Akimkaribisha Mgeni ulifungua Kongamano hilo Kaimu
Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Maaalim Haroun Ali Suleiman alisema serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) imeanzisha
Mradi wa kuzizaidia taasisi za kiraia nchini (ZANSAP) ili zifanye kazi zake kwa
ufanisi na kuchangia maendeleo ya jamii.
“Mradi huu wenye kutekelezwa kwa mfumo wa Mkataba
ulibuniwa kwa lengo la kuimarisha demokrasia na utawala bora, kuongeza ushiriki
wa wananchi katika shuguli zinazowahusu, ushiriki wa azaki katika utekelezaji
wa sera, sheria sambamba na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya kitaifa na
kimataifa nchini na tunatarajia hadi kukamilika kwa mradi, taasisi hizi zitakuwa
zimeimarika na kuibua maeneo mapya ya utekelezaji”, alisema Maalim Haroun ambae
pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utawala Bora na Utumishi
wa Umma.
Zaidi ya asasi za kiaraia 200 zinashiriki kongamano hilo lililoanza
januari 24 hadi 25 mwaka huu kutoka Unguja na Pemba ambalo ni la pili baada ya
lililofanyika mwaka uliopita ambalo lilitumika kuutambulisha mradi wa ZANSAP
kabla ya kuanza utekelezaji wake kwa kuzijengea uwezo asasi na makundi mbali
mbali ya kijamii.
Balozi Seif akinusa ili kuridhika na kiwango cha utengenezaji wa Mafuta ya asili ya nazi yaliyosarifiwa na wajasiriamali wa Zanzibar wakati
alipokuwa akikagua maonesho ya kazi za asasi za kiraia Zanzibar. Kushoto yake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utawala Bora na Utumishi wa Umma Haroun Ali Suleiman na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (alievaa miwani) akipata maelezo juu ya moja ya bidhaa zilizotengenezwa na Wajasiriamali wa asasi za Kiraia alipotembelea maonesho ya kazi za wajasiriamali kabla ya kufungua Kongamano la pili la Asasi za Kiraia za zanzibar linalofanyika katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini.
Balozi Seif akihutubia washiriki wa kongamano la pili la asasi za kiraia zanzibar (hawapo pichani) linalofanyika katika Ukuimbi wa Mikutano wa hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini Nje
kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi (katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya
Maandalizi ya Kongamano la asasi za Kiraia Zanzibar (waliosimama) mara baada ya kulifungua rasmi Kongamano
hilo. Wengine katika picha hiyo kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud, Mkuu wa timu ya wataalamu wa mradi wa kuziwezesha asasi za kiraia Zanzibar (ZANSAP) Fergal Ryan, Mwenyekiti wa kongamano hilo Dk. Mzuri Issa Ali, Kaimu Waziri wa Fedha na Mipango Maalim Haroun Ali Suleiman, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar Juma Khamis Reli na Kamishna wa Fedha za nje katika wizara ya fedha na mipango Zanzibar Hindi Nassor Khatib.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif (katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wawakilishi wa asasasi za kiraia zinazoshiriki Kongamano la pili la asasi za Kiraia Zanzibar (waliosimama) mara baada ya kulifungua rasmi Kongamano hilo linalofanyika katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mzizini. wa kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya watu wenye ulemavu Zanzibar Abeda Rashid mara baada ya kulingua rasmi Kongamano hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akiagana na Mwenyekiti wa Kongamano la asasi za
Kiraia mara baada ya kulifungua rasmi Kongamano hilo linalofanyika katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mzizini. anaeshuhudia ni Mkuu wa timu ya wataalam wa mradi wa kuziwezesha asasi za kiraia Zanzibar (ZANSAP) Fergal Ryan.
(PICHA KWA HISANI YA OMPR)
No comments:
Post a Comment