NA
MWINYIMVUA NZUKWI
Rais
mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume amewataka wananchi wa Zanzibar
kutunza na kuhifadhi miundombinu ya kiuchumi inayotengenezwa na serikali ili
kukuza uchumi wa nchi na jamii kwa ujumla.
Akihutubia
wananchi na watendaji mbali mbali wa taaisisi za serikali, binafsi na kisiasa
katika uzinduzi wa ukuta wa bahari wa mizingani Dk. Karume aliyeiongoza
serikali ya awamu ya sita, alisema kutotunzwa kwa miradi hiyo kutaisababishia
hasara serikali na wananchi kwa ujumla.
Alisema
mradi huo ambao ulibuniwa wakati wa uongozi wake, ulilenga kuondoa hatari
iliyokuwa inayoukabili ukuta wa awali amabao ulijengwa mnamo mwaka 1920,
kupunguza madhara ya maji ya mvua katika maeneo ya makaazi na kuipa haiba nzuri
miji mikuu ya Zanzibar.
“Mradi
huu umetekelezwa kwa fedha amabazo ni mkopo, hivyo msiposhiriki katika utunzaji
wake licha ya kuwa tutaendelea kupata madhara lakini mjue kuna siku sote
tutahusika katika malipo ya mkopo huu”, alitahadharisha Dk. Karume.
Aidha
aliishauri wiraza ya fedha kuandaa mradi utakaolenga kuwasaidia wamiliki wa
majengo yaliyomo ndani ya eneo la Mji Mkongwe wasio na uwezo wa kuyajenga au
kuyafanyia ukarabati majengo yao ili kuuweka mji huo katika haiba na usalama
zaidi.
“Nimefurahi
kusikia kuwa awamu ijayo ya mradi huu (uimarishaji wa huduma za miji ya
Zanzibar – ZUSP) kuwa utahusisha ukarabati wa jengo la Beit El Jaib, basi
muongee na hawa wakubwa (benki ya dunia) kuona uwezekano wa kuwasaidia wamiliki
wa majengo yaliyomo ndani ya Mji Mkongwe wawajengee uwezo wa kuyajenga upya
majengo yaliyoanguka na kuyafanyia ukarabati yaliyokonga ili kuuongezea haiba
na thamani mji huu ambao ni urithi wa kimataifa”, alisisitiza Dk. Karume.
Awali
akimkaribisha Dk. Karume, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dk. Khalid Salum
Mohammed mbali ya kuishukuru benki ya dunia kwa kufadhili mradi huo, pia
aliishukuru kwa kukubali kutoa fedha dola za marekani 55 milioni kwa ajili ya
utekelezaji wa mradi wa ZUSP awamu ya pili utakaohusisha ujenzi wa jaa la kisasa
litakalojengwa katika eneo la Kibele wilaya ya Kati Unguja.
“Miongoni
mwa kazi nyengine ni pamoja na ujenzi wa njia za waenda kwa miguu katika
barabara za Malindi – Darajani, Mkunazini – Kariakoo, uwekaji wa taa za
barabarani katika barabara ya Mwanakwerekwe – Uwanja wa ndege na ujenzi wa
mtaro mkubwa wa maji ya mvua utakaoanzia katika bwawa la Mwanakwerekwe –
Magogoni – Sebleni – Kwa Abasi Hussein – Kinazini”, alisema Dk. Khalid.
Aidha
aliishukuru benki ya dunia kwa misaada yake kwa serikali ya Zanzibar ambayo
alisema imesaidia na kuchochea kasi ya maendeleo ya Zanzibar na wananchi wake
na kuwapongeza wakandarasi na wasimamizi wa ujenzi wa ukuta huo kwa kumaliza
kazi hiyo kwa ufanisi na kwa wakati uliopangwa.
“Hakika
umahiri uliooneshwa na mjenzi, mshauri mwelekezi na msimamizi wa ujenzi wa
mradi huu wa kumaliza kazi kwa viwango na wakati uliopangwa umeongeza Imani ya
serikali kwenu na hakika mmejiwekea akiba njema katika kumbukumbu za ujenzi
hapa Zanzibar”, alieleza Dk. Khalid.
Akitoa
maelezo ya kitaalamu kuhusiana na ujenzi wa ukuta huo sambamba na utekelezaji
wa mradi wa ZUSP katibu mkuu wa wizara ya fedha na mipango Zanzibar alisema
mradi huo uliosainiwa mwaka 2009 na kuanza utekelezaji wake april 2010, kwa
kuhusisha maeneo manne makuu ya ujenzi wa ukuta huo wenye urefu wa mita 312
kuanzia bustani ya forodhani hadi mizingani.
Maeneo
mengine ya mradi huo ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa
mita 308 na upana wa mita 6, ujenzi wa njia za waenda kwa miguu, vibaraza vya
kupumzikia, uekaji wat aa za barabarani na ujenzi wa njia za maji ya mvua
kuelekea katika bahari ya hindi kazi iliyokamilika na kukabidhiwa serikalini
mwezi septemba mwaka uliopita.
“Kwa upande wa gharama za Ujenzi jumla ya
Shilingi za Kitanzania bilioni 7,636,056,400/- zilitumika. Fedha hili ni bila
ya ongezeko la thamani ambalo linakisiwa kuwa ni shilingi za Kitanzania milioni
763,605,640 na kwa upande wa malipo ya mkandarasi, malipo yote stahiki tayari
yamelipwa na malipo yaliyobakia ni ya mwisho (retention payment), malipo hayo
hufanywa baada ya kumalizika kwa muda wa uangalizi wa ubora yaani “Defect
Liability Period”, alisema na kuongeza kuwa fedha hizo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka benki ya
dunia.
Akitoa
salamu za benki ya dunia, mwakilishi wa benki hiyo nchini Tanzania Andre Bald
alisema taasisi yake imeridhishwa kufikiwa kwa viwango katika ujenzi wa ukuta
huo na utekelezaji wa mradi mzima hivyo itaendelea kuisaidia Zanzibar na
Tanzania ili kuweka viwango bora vya maisha ya watu wake.
“Benki
ya dunia kila mara huzingatia upatikanaji wa huduma bora za maisha ya watu
hivyo kila mtakapofikiria njia bora za kuimarisha maisha ya watu sisi
hatutosita kusaidia hasa pale kunapokuwa na utekelezaji unaoashiria matokeo
bora kama ilivyo katika mradi huu wa uimarishaji wa huduma za miji ya
Zanzibar”, alisema Bald.
Uzinduzi
wa ukuta huo ulifanyika katika eneo la Mizingani na bustani ya Forodhani ikiwa
ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar ambapo
mbali ya Dk. Karume viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala bora maalim
Haroun Ali Suleiman, mke wa Dk. Karume Mama Shadya Karume, Naibu Waziri wa
Ujenzi, mawasiliano na uchukuzi Mohammed Ahmada Salum, wenyeviti wa chama cha
mapinduzi (CCM) mikoa ya Mjini na Magharibi (kichama) na viongozi wa dini
akiwemo katibu wa mufti wa Zanzibar sheikh Fadhil Suleiman Soraga.
Rais
Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Aman Abeid Karume akikata
utepe kuashiria Uzinduzi wa matumizi ya eneo la Ukuta wa kuzuia maji ya bahari katika eneo la Mizingani Mjini
Zanzibar ikiwa ni shamra shamra za Maadhimisho ya kutimia Miaka 54 ya
Mapinduzi ya Zanzibar. Kulia yake ni Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Khalid Salum
Mohammed na kushoto ni Mwakilishi wa Benki ya Dunia Andre Bald.
Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Aman Abeid Karume (Kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mratibu wa Mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) Makame Ali Makame kuhusiana na ujenzi wa ukuta wa Baharini katika uzinduzi wa ukuta huo katika eneo la Mizingani Mjini Zanzibar.
Rais
Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt,Aman Abeid Karume (katikati) akitembea kwa miguu baada ya uzinduzi wa Ukuta wa Baharini
Mizingani kuelekea katika Bustani ya Forodhani Mjini Zanzibar. Wengine kutoka kulia ni Mratibu wa mradi wa ZUSP Mkame Ali Makame, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud, Waziri wa fedha na mipango Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohammed na Katibu Mkuu wizara ya fedha na mipango Khamis Mussa Khamis.
Mwakilishi
wa Benki ya Dunia Andre Bald akitoa salamu za taasisi yake juu ya utekelezaji
wa miradi mbali nchini inayofadhiliwa na beki hiyo ukiwemo ujenzi wa ukuta
wa Baharini katika eneo la Mizingani sherehe zilizofanyika katika Bustani ya
Forodhani Mjini Zanzibar.
Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Aman
Abeid Karume akisisitiza jambo alipokuwa akihutubia hadhara (haipo pichani)
wakati wa uzinduzi wa ukuta wa baharini wa Mizingani sherehe zilizofanyika katika
Bustani ya Forodhani Zanzibar. Kulia ni waziri wa fedha na mipango Zanzibar Dk.
Khalid Salum Mohammed na kushoto ni Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini Andre Bald.
1. Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya fedha na Mipango Zanzibar na wageni waalikwa waliohudhuria katika uzinduzi wa ukuta
wa baharini wa Mizingani sherehe zilizofanyika katika Bustani ya Forodhani Mjini
Zanzibar zikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 54 ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment