Monday, January 8, 2018

BALOZI SEIF AWATAKA WAKANDARASI KUZINGATIA UADILIFU

NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaomba Wakandarasi na wasimamizi wanaopata kazi za Ujenzi katika Taasisi za Serikali kufanya kazi zao kwa uadilifu wa hali ya juu kinyume chake Serikali haitokubali kukabidhiwa majengo yasiyokuwa na kiwango.

Alisema Serikali italazimika kutumia sheria za ujenzi zilizopo katika njia na Utaratibu wa  kukataa kazi yoyote ile iliyokuwa chini ya kiwango kinachokubalika kimikataba.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa ombi hilo wakati akiweka Jiwe la Msingi wa Ofisi Tatu Pacha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambazo ni za Wizara ya Kazi Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto, Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora zilizofanyika Mtaa wa Gombani Chake Chake Pemba.

Alisema haikubaliki kuona muda  mfupi tu baada ya kukamilika kwa Ujenzi na kukabidhiwa Majengo hayo yanaanza kuharibika, kuvuja, kupasuka, kupoteza haiba na hadhi inayokusudiwa.

Balozi Seif alieleza kwamba hivi sasa yapo Mjengo mengi hasa yake ya Skuli katika maeneo tofauti Nchini yaliyojengwa chini ya kiwango zimeanza kuvuja kama chungio jambo ambalo Serikali Kuu tayari imepata fundisho kutoka kwa baadhi ya Wakandarasi na hivyo hapana budi sasa kuchukuwa tahadhari.

Alieleza kuanzishwa kwa ujenzi wa majengo pacha kwa ajili ya matumizi ya Ofisi za Wizara Tatu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambao zote ni muhimu kumefungua fursa za ujenzi wa jengo jengine kwa ajili ya matumizi ya Ofisi ya Bodi ya Mapato Zanzibar litakalokuwepo Mkabala na Majengo hayo.

Balozib Seif alisema ujenzi huo utazidi kulifanya eneo hilo la Gombani kuwa na haiba nzuri zaidi na  ni matarajio ya Wananchi wanaoishi jirani na maeneo hayo wanaweza kunufaika kwa kuitumia fursa hiyo kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo.

Alisema biashara hiyo itakayosaidia kutoa ajira kwa Wananchi hao itaweza kuwahudumia Wafanyakazi wengi watakaokuwa wanapita katika maeneo yao wakati wakielekea au kutoka kazini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wananchi na Vijana wote waliokuwa wakilitumia eneo hilo kwa uamuzi wao wa kizalendo waliouonyesha  wa kuamua kuondoka wenyewe kwa hiari yao ili kupisha shughuli hizo za ujenzi wa Ofisi za Serikali.

“Kulikuwa na Vijana waliolitumia eneo hilo kibiashara, uoshaji wa Magari pamoja na Wakulima waliojishughulisha na kilimo cha mboga mboga ambao walikubali kuhama kupisha mradi wa maendeleo bila ua usumbufu”. Alisema Balozi Seif.

Alitoa wito kwa Wananchi wa maeneo mengine  Pemba na Unguja ambao wanatumia ardhi ya Serikali kwa kufanya shughuli zao binafsi wanapaswa  kujifunza kutoka kwa Wananchi wa Gombani kwa kuondoka bila ya malalamiko kupisha ujenzi wa Serikali.

Alielezea matumaini yake kwamba kukamilika kwa ujenzi wa Ofisi hizo Tatu Pacha na kuanza kutumika kwake kunatarajiwa kuimarisha huduma zinazotolewa na Wizara hizo Kisiwani Pemba.

Alisema katika kuimarishwa huduma hizo kwa Wananchi Serikali imepanga kuweka mifumo ya Kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambayo kwa kiasi kikubwa huwa inachochea utendaji kazi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Wananchi wote wa Zanzibar kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza na malengo yote ya Mapinduzi ambao ni kutoa huduma bora kwa Wananchi.

Mapema  akitoa Taarifa ya ujenzi wa Majengo pacha ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Gombani Chake chake Pemba Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar Nd. Khamis Mussa Omar alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha iliandaa Programu ya ujenzi wa Majengo ya Taasisi za Serikali Unguja na Pemba.

Nd. Mussa alisema hatua hiyo imekuja kufuatria Ofisi nyingi za Serikali kukumbwa na changamoto ya uhaba wa Ofisi jambo ambalo lilisababisha watendaji wa Taasisi hizo kusoma uwajibikaji unaotakiwa.

Alisema ujenzi wa Ofisi Tatu Pacha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Gombani Pemba umezingatia uhaba huo wa Ofisi ambapo zaidi ya Wafanyakazi 186 wa Wizara hizo walikuwa wakifanya kazi zao katika mazingira mabovu  ambayo Ofisi nyingi tayari zimechakaa.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango alieleza kwamba ujenzi wa Ofisi pacha za SMZ Gombani umeanza mara baada ya kutiwa saini Mkataba wa Mradi huo mapema mwezi Julai Mwaka 2017 na ujenzi wake kuanza rasmi Oktoba Mwaka huo.

Alisema maendeleo ya ujenzi wa Mradi huowa sasa umeshafikia asilimia 52% ambapo hatua iliyofikiwa inakwenda na mkataba wa Ujenzi. Hata hivyo alisema wakati ujenzi ukiendelea Wizara hiyo kwa kuzingatia mfumo wa uwajibikaji wa ongezeko la Ofisi ilishauri kuwepo kwa Ofisi ya Tume ya Mipango wazo lililokubaliwa na Swerikali Kuu na hatimae kuongezwa kwa Ghorofa Moja zaidi ya Majengo hayo.

Ndugu Khamis Mussa Omar kwa niaba ya Wizara ya Fedha aliwaomba radhi Wananchi ambao ndio walipa kodi Wakuu kufuatia changamoto iliyotokea ya ujenzi wa Jengo la Wizara hiyo liliopo Tibirinzi Chake chake Pemba ambalo halikuwa katika kiwango kilichokubalika cha Ujenzi.

Alisema Taratibu za kisheria dhidi ya Mkandarasi wa ujenzi wa jengo hilo zimechukuliwa na tayari ameshafikishwa kwenye vyombo vya Sheria na kuilipa fidia Serikali kutokana na uzembe huo ambao aliahidi kwamba hautatokea tena.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Majengo Pacha ya SMZ Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar  Dr. Khalid Salum Mohamed alisema Teknolojia ya Kisasa inayokwenda kwa kasi tayari imeshakuwa haioani na Majengo mengi ya Taasisi za Serikali zilizopo hivi sasa.

Dr. Khalid alisema inapendeza kuona Taasisi nyingi za Serikali hivi sasa zimeanza kuelekea kwenye mfumo wa kisasa wa majengo yanayokwenda na mfumo wa dunia wa Mawasiliano ya Habari na Teknolojia.

Aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kwa kuridhia ujenzi wa Jengo Jipya la Bodi ya Mapato Zanzibar {ZRB} jirani na Mjego Pacha ya Ofisi za Serikali yaliyopo Gombani Mpya Chake Chake Pemba.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar alisema ujenzi wa Ofisi Mpya za Serikali uliomo ndani ya Utekelezaji wa Programu maalum inayosimamiwa na Wizara ya Fedha umekuja kutokana na kuongezeka kwa Mapato ya Taifa katika kiwango kinachokubalika.

Alisema hali ya kuongezeka huo kumechangia pia ongezeko la huduma kwa Wananchi hasa katika Sekta ya Afya, Elimu Kilimo na miradi mengine inayolenga kupunguza ukali wa maisha wa Wananchi walio wengi Visiwani Zanzibar.

Ujenzi wa Majengo Pacha ya Ofisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar unaogharamiwa kwa asilimia 100% na Serikali ambao uko chini ya ujenzi na Wasimamizi Wakandarasi Wazalendo utararajiwa kugharimu zaidi ya Shilingi za Kitanzania Bilioni Saba, Milioni Mia Nane na 24.

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akifungua pazia kuashiria kuweka jiwe la msingi la jengo litakalotumiwa na ofisi mbali mbali za serikali ya Zanzibar kisiwani Pemba.



 Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akikagua ujenzi wa jengo litakalotumiwa na wizara mbali mbali za serikali ya zanzibar  mara baada ya kuweka jiwe la msingi.


baadhi ya wananchi waliohudhuria na kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi wa majengo pacha yatakayotumiwa na wizara mbali mbali za serikali ya zanzibar ujenzi ambao unasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar.


Muonekano wa majengo pacha yanayojengwa na serikali ya Zanzibar kwa ajili ya iofisi za wizara mbali mbali kisiwani Pemba. (Picha kwa hisani ya OMPR)

No comments:

Post a Comment