Wednesday, January 10, 2018

DK. SHEIN KUWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA MJI KISASA WA FUMBA

NA MWINYIMVUA NZUKWI
Ikiwa imesalia siku moja kabla ya kilele cha sherehe za mapinduzi ya Zanzibar,leo asubuhi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa mji wa kisasa wa Fumba itakayofanyika Nyamanzi, wilaya ya Magharibi B.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Halmashauri ya sherehe na maadhimisho ya kitaifa shughuli hiyo ambayo awali ilipangwa kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli itafanyika chini ya usimamizi wa wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar.

Mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya CPS-Lives LTD ikiwa ni sehemu ya miradi 35 iliyopangwa kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi katika kipindi cha maadhimisho hayo yanayofikia kilele chake Januari 12, 2018.

Akizungumzia tukio hilo Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya CPS-Lives Tobius Dietzold aliishukuru serikali ya Zanzibar kwa Kuuhusisha mradi huo katika maadhimisho ya sherehe za mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka huu ambayo  yanayotimiza miaka 54 toka yalipoasisiwa Januari 12, 1964.

"Toka tumeanza kutekeleza mradi wetu tumekuwa na mashirikiano ya karibu sana na serikali ya Zanzibar na viongozi wake, hii ni kwa sababu tunajenga mji huu hapa Zanzibar kwa ajili ya Wazanzibari hivyo tunaamini kuingizwa katika ratiba ya sherehe hizi kunaongeza thamani ya kile tunachokifanya na ari ya wafanyakazi wetu", alisema Tobius.

Mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa wa Fumba (Fumba Town Development) ni miongoni kwa miradi miwili mikuu ya makaazi inayotekelezwa katika ukanda wa maeneo huru ya kiuchumi ya Fumba yaliyotangazwa mnamo miaka ya 90.

Mbali na shughuli hiyo, mchana wa januari 11 Dk. Shein atatunuku nishani maalum za mapinduzi kwa watu mbali mbali waliotoa mchango na kutumikia jamii katika nyadhifa matukio mbali mbali wakati Rais mstaafu wa awamu ya sita Dk. Amani Abeid Karume atafungua kituo cha kutotolea vifaranga vya samaki huko Beit el Ras, Wilaya ya Magharibi 'A' Unguja.

Wakati wa mchana Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohammed Aboud Mohammed anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika bonanza la mashindano ya michezo mbali mbali ya miaka 54 ya mapinduzi yakakayofanyika katika viwanja vya maisara kabla ya vikosi vya ulinzi na usalama kurusha fashifashi za maadhimisho hayo itakapofika saa 6:00 usiku mkesha ambao utatawaliwa na burudani mbali mbali za ngoma asilia, muziki wa dansi na muziki wa kiizazi kipya shughuli zitakazofanyika katika viwanja vya Maisara Mjini Unguja na Gombani kisiwani Pemba.




Muonekano wa moja ya nyumba za mfano zinazojengwa katika mradi wa mji wa kisasa wa Fumba unaotekelezwa na kampuni ya CLS-Lives LTD ambae utawekewa jiwe la msingi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment