Friday, January 26, 2018

ZATU KUKUTANA JANUARI 27 - 28, DK. SHEIN ATARIWA KUBARIKI MKUTANO MKUU FEBRUARI

NA MWINYIMVUA NZUKWI
Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU) kinatarajia kufanya mikutano mikuu ya ngazi kanda kabla ya kukutana katika ngazi ya taifa baadae mwezi Februari mwaka huu.

Katibu wa chama hicho Mussa Omar Tafurwa amewaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho Kijangwani mjini Unguja kuwa mkutano wa kanda ya Unguja utafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Uhuru Kariakoo wakati mkutano wa kanda ya Pemba utafanyika katika skuli ya sekondari Madungu.

Amesema mikutano yote hiyo uitakayokuwa ya siku mbili pamoja na kufanya kazi zake za kawaida za kupokea, kujadili na kupitisha taarifa mbali mbali zinazohusiana na chama hicho, pia itafanya uchaguzi wa kuwachagua viongozi watakaoziongoza kanda hizo, wajumbe wa mkutano mkuu na baraza kuu la taifa.

“Tunatarajia katika siku mbili hizo wajumbe wa mikutano hiyo watapata nafasi nzuri ya kujadili na kupanga mikakati ya baadae ya chama chetu ikiwa ni pamoja na kuwachagua wenyeviti wa kanda, wajumbe 6 wa baraza kuu taifa, wajumbe wawili wa kamati kuu kutoka kila wilaya na wajumbe wa mkutano mkuu taifa”, alisema Mwalimu Tafurwa.

Aidha alieleza kuwa mkutano mkuu wa taifa wa chama hicho utafanyika Februari 10 na 11 mwaka huu unaotarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali na wadau wengine wa elimu wakiwemo viongozi wa vyama vya walimu na mashirikisho ya vyama vya wafanyakazi kutoka ndani na nje ya nchi.

“Kutakuwa na waalikwa kutoka ndani na nje ya nchi katika mkutano huo ambao tunatarajia utahudhuriwa na wastani watu kati ya 180 na 200 ambapo mbali ya ajenda za kawaida pia utawachagua viongozi wa chama katika ngazi ya taifa”, alifafanua Katibu huyo.

Alizitaja nafasi zinazogombewa katika uchaguzi huo kuwa ni ya Rais, Makamo wa Rais, wajumbe 7 wa Kamati Tendaji taifa, wajumbe wa kukiwakilisha chama katika Baraza Kuu la vyama vya wafanyakazi na wajumbe wa kukiwakilisha chama katika mkutano mkuu wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi Zanzibar.

Akizungumzia ujumbe wa mkutano huo Mwalimu Tafurwa alisema mkutano huo utaendeleza ujumbe wa kimataifa wa siku ya walimu unaosema ‘uhuru katika kufundisha hujenga uwezo wa mwalimu’ na kuwataka walimu nchini kuzingatia maadili ya taaluma yao wanapokuwa kazini ili kuongeza tija na kulinda hadhi ya fani hiyo.

Mussa Omar Tafurwa, Katibu Mkuuu wa chama cha walimu Zanzibar (ZATU) akisisitiza jambo katika moja ya mikutano yake na waandishi wa habari.






No comments:

Post a Comment