Wednesday, February 28, 2018

DK. SHEIN APANGUA BARAZA LA MAPINDUZI, AONGEZA WIZARA, MANAIBU MAWAZIRI



NA MWINYIMVUA NZUKWI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amafanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mapinduzi kwa kuongeza Wizara moja zaidi na kuzibadilisha muundo na mawaziri wa baadhi ya Mawaziri. 

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais ikulu na kusambazwa katika wa vyombo vya habari, Dkt. Shein ameunda wizara mpya ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo itakayoongozwa na balozi Ali Abeid Karume na naibu wake Lulu Abdulla Khamis ambapo shughuli za Vijana zilizokuwa katika wizara ya kazi, uwezeshaji kiuchumi, vijana, wanawake na watoto zimehamishiwa katika Wizara hiyo mpya.

Aidha shughuli za mazingira zilizokuwa katika wizara ya ardhi, maji nishati na mazingira zimehamishiwa katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na shughli za Wakala wa Serikali wa Uchapaji zilizokuwa katika ofisi ya makamo wa pili wa Rais zimehamishiwa Wizara mpya ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale. 


Taarifa hiyo imeeleza kuwa Dkt. Shein amewateua Naibu Mawaziri wapya wawili na kumbadilisha Wizara Naibu Waziri mmoja na kupelekea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na Wizara 14 zenye Mawaziri na Naibu Mawaziri badala ya 13 za awali pamoja na mawaziri wawili wasiokuwa na wizara maalum.

Katika mabadiliko hayo Dkt. Shein aliwateua tena Issa Haji Ussi Gavu kuwa Wizara wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Maalim Haroun Ali Suleiman kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Naibu Waziri katika wizara hiyo Khamis Juma Mwalim. 


Katika Wizari ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri na Naibu wake Shamata Shaame Khamis wanaendelea kuitumikia wizara hiyo wakati Mohamed Aboud Mohamed anaendelea kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Naibu wake ni Mihayo Juma Nhunga.

Hamad Rashid Mohamed aliyekuwa waziri wa kilimo, maliasili, mifugo na uvuvi amehamishiwa katika wizara ya Afya itakayokuwa na naibu Waziri Harusi Said Suleiman anaendelea kama ilivyo kwa Salama Aboud Talib anaendelea kuiongoza Wiziri ya Ardhi, Nyumba, Maji na sambamba na naibu wake Juma Makungu Juma. 

Balozi Amina Salim Ali anaendelea kuhudumu katika wizara ya Biashara na Viwanda iliyopatiwa naibu waziri mpya Hassan Khamis Hafidh, walimu Riziki Pembe Juma 
na Mmanga Mjengo Mjawiri wanaendelea kuingoza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kama ilivyo kwa Dkt. Khalid Salum Mohamed aneendelea kuwa Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar.

Aliyekuwa Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo ametuliwa kuongoza Wiziri ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale wakati Choum Kombo Khamis anakuwa Naibu Waziri katika wizara hiyo ambayo kabla ya mabadiliko hayo ilijulikana kama Wizara ya habari, utamaduni, utamii na michezo.  

Katika Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico anaeendelea kuwa waziri na naibu wake ni Shadia Mohamed Suleiman, rashid ali juma aliyekuwa waziri wa habari, utamaduni, utalii na michezo amehamishiwa katika Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi atakaesaidiwa na Dkt. Makame Ali Ussi alieteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa naibu waziri katika wizara hiyo.


Aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na waziri asiekuwa na wizara Maalum Dkt. Sira Ubwa Mamboya ameteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji iliyokuwa ikiongozwa na Balozi Ali Abeid Karume ambapo Mohamed Ahmada Salum anaendelea kuwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji katika uteuzi huo unaonza Machi 1, 2018.



Monday, February 26, 2018

93 WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA ZANZIBAR


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Jeshi la polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, limewafikisha watuhumia 93 wa makossa mbali mbali ya udhalilishaji wa kijinsia katika mahkama za mkoa huo ikiwemo ya Hassan Aboud Talib maarufu ‘Kiringo’.

Kamanda wa polisi mkoani humo Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Msaidizi Kamishna Hassan Nasssir Ali aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake Mwembe madema wakati akitoa taarifa za matukio mbali mbali yaliyotokea katika wiki iliyopita na kueleza kuwa hiyo ni awamu ya tatu ya kundi la watuhumiwa hao kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Alisema jeshi hilo bado linaendelea na mkakati wake wa kupunguza makossa hayo licha ya kushindwa kuwapata watuhumiwa 39 kati yao ambao kutokana na kutowapata kwa wakati muafaka na wengine kuruka dhamana walizowapatia.

Alifahamisha kuwa jeshi la polisi litawachukulia hatua za kisheria wadhamini wa watuhumiwa hao baada ya kukiuka masharti ya dhamana kwa kushindwa kuwarudisha kituoni pale wanapohitajika.

“Polisi inapozuia dhamana dhidi ya baadhi ya watuhumiwa huonekana kama inakiuka sheria au haki za watuhumiwa lakini hapa tuna mifano ya kesi nyingi ambazo watuhumiwa hawadudi kituoni baada ya kupewa dhaman ana kupelekea kushindwa kuanza kwa wakati kwa kesi husika”, alieleza Kamanda Nassir.

Mapema asubuhi mamia ya wananchi, wanaharakati na wanahabari walifunga kambi katika viunga vya mahakama kuu ya Zanzibar kwa lengo la kumshuhudia ‘Kiringo’ akifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza baada ya kukamatwa wiki iliyopita akituhumiwa kumlawiti mtoto wa kiume wa miaka 14.

Hata hivyo kesi hiyo inayovuta hisia za watu wengi ndani na nje ya Zanzibar inayosikilizwa na hakimu Valentine Andrew imeahirishwa hadi kesho Februari 27 wakati hakimu huyo atakapotoa hukumu juu ya ombi lililotolewa na wakili wa mtuhumiwa la kupatiwa dhamana mteja wake ombi ambalo awali lilipingwa na upande wa jamhuri na kuzusha mabishano ya kisheria kati ya pande mbili hizo.


Hassan Aboud Talib 'Kiringo' mmoja ya watuhumiwa wa kesi za udhalilishaji waliofikishwa mahakamani. 


Sunday, February 25, 2018

WAHIMIZWA USAFI, MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA

NA MWINYIMVUA NZUKWI
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka wananchi kuwa na utamaduni ya kufanya usafi katika njia za kupitishia maji machafu na kufuata sheria za matumizi bora ya ardhi ili kuondokana na athari ya mafuriko.

Ayoub ameyasema hayo wakati aliposhiriki katika zoezi la usafi wa mazigira lililoandaliwa na kundi la ‘Safari ya CCM 2020’ na Manispaa ya wilaya ya Magharibi "A" uliofanyika  Mwera Meli sita Wilayani humo.

Alisema mvua za masika zinatarajiwa kunyesha hivi karibuni zimekuwa zikisababaisha maafa makubwa kwa watu na mali zao kila mwaka hivyo kila mwananchi anawajibu wa kuchukua tahadhari juu ya suala usafi.

“Kwa wale wanaoishi sehemu za mabondeni kuna haja ya kuchukua hatua za tahadhari kwa kuanza kuhama katika maeneo hayo na kufanya usafi wa mara kwa mara hasa katika njia za maji ili kupunguza athari”, alisema Ayoub.

Aidha aliuomba uongozi wa kundi la ‘Safari ya CCM 2020’ kuendeleza utamaduni wa kushiriki katika shughuli mbali mbali za kijamii na kisiasa ili kusaidia mabadiliko ya tabia na fikra kuhusiana na swali la usafi wa mazingira yanayowazunguka.

“Ninawapongeza kwa juhudi mnazochukua katika kusaidia mabadiliko ndani ya jamii yetu, hivyo ningewaomba kuweka mkazo wa kushajiisha mabadiliko ya fikra hasa katika maswali ya usafi wa mazingira lakini pia kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambanodhidi ya rushwa na uhujumu uchumi”, alieleza Ayoub.

Akizungumzia masuala ya rushwa na uhujumu wa uchumi afisa uchumguzi wa mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu wa uchumi Yussuf Juma aliitaka jamii kuchukia vitendo vya rushwa na kuwa tayari kuvitolea taarifa katika taasisi yake ili kudhibiti athari za uovu huo.

“Mapambano dhidi ya rushwa ni ya jamii nzima lakini kwa wanachama wa CCM (Chama cha Mapinduzi) hili ni kipaumbele namba moja kwa kuwa katiba na ilanoi ya uchaguzi ya 2015 – 2020 imeeleza wazi kuwa itazielekeza serikali zake kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi hivyo kila mmoja ahakikishe anapiga vita rushwa iwe ndani au nje ya chama”, alisema Yussuf na kuitaka jamii itwayo kuunga mkono kampeni ya FUNGUKA kwa kupiga simu namba 113 kutoa taarifa za rushwa.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Keptaini Khatib Khamis Mwadini alisema kuwa serikali ya Wilaya yake imeanzisha utaratibu maalum wa kufanya usafi kwa kila Shehia katika kila jumamosi ya mwisho wa wiki ili kuondokana na maradhi ya mripuko.

Alisema hatua ya wanakikundi hao kuamua kufanya kampeni hiyo ya usafi pamoja na kuchangia damu ni jambo jema linalopaswa kupongezwa kwa kuwa litaokoa maisha ya watu wengi bila ya kujali itikadi zao.

Mapema asubuhi makundi mbali mbali yakiwemo ya wafanyakazi wa manispaa ya magharibi ‘A’, masheha wa shehia za wilaya hiyo, wanachama wa ccm wa matawi yaliyomo wilayani huo na wananchi wa kawaida waliungana kusafisha maeneo mbali mbali ya eneo la mwera meli sita liliopo jirani na ofisi za mkuu wa wilaya hiyo na kuchagia damu. 

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud  (kushoto) akifagia wakati wa zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo ya Mwera Meli sita Wilaya ya Magharibi 'A' Unguja. Kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Kepteni Khatib Khamis Mwadini.

Wafanyakazi wa Manispaa ya Magharibi 'A' na wananchi wa wilaya ya Magharibi 'A' wakiendelea na kazi ya usafi wa mazingira  karika barabara ya Mwera Meli sita wakati wa kampeni ya usafi iliyoandaliwa na kundi la 'Safari ya CCM 2020'.

Mkuu wa Mkoa wa mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud (kushoto) akisalimiana na mmoja ya wanachama wa kundi la 'Safari ya CCM 2020' wakati kundi hilo lilipoandaa kampeni ya usafi wa mazingira katika maeneo ya Mwera Meli sita, Wialya ya MaghariBI 'A' Unguja. 


UDHIBITI WA VIWANGO VYA MATAIRI KUANZA APRIL ZANZIBAR

NA MWINYIMVUA NZUKWI
SERIKALI ya Zanzibar imewataka wafanyabiashara na waingizaji wa bidhaa za matairi ya magari na vyombo vingine vya moto kuzingatia utaratibu mpya utakaonzishwa na taasisi ya viwango Zanzibar (ZBS) kuhusiana na uingizaji wa bidhaa hizo ili kukuza uchumi wa nchi na ustawi wa jamii.

Naibu katibu mkuu wa wizara ya biashara, viwanda na masoko ali khamis juma alitoa wito huo alipokuwa akifungua semina ya siku moja kwa  wafanyabiashara wa bidhaa hizo iliyolenga kutoa elimu kwa kundi hilo ili kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.

Alisema dhana ya ukuaji wa uchumi na biashara huria zinategemea uwezo wa uzalishaji na matumizi ya bidhaa au huduma zenye ubora unaoendana na viwango vinavyotambulika kitaifa na kimataifa ambavyo vinahakikisha afya za watumiaji na mazingira ya nchi yanabakia salama na endelevu.

Alisema matairi ya vyombo vya moto ni miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa na kutumika katika shughuli nyingi za maendeleo ya kila siku kupitia huduma ya usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo hivyo kuna haja kubwa ya wafanyabiashara hao kutumia elimu waliyopatiwa kuwaelimisha watumiaji wengine wa bidhaa hizo jambo alilodai litasaidia kupunguza ajali na uharibifu wa mazingira.

“ZBS (Taasisi ya viwango Zanzibar) itaendelea kufanya ukaguzi kioa mara ili kuhakikisha bidhaa zinazoingia katika soko la Zanzibar na kutumika zinazingatia usalama, afya, mazingira na ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla na sio chanzo cha madhara kwa jamii yetu kwa faida ya sasa na baadae”, alisema Khamis.

Awali akikitoa maelezo ya utangulizi katika semina hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya viwango Zanzibar Mwadini Khatib Mwadini alieleza kuwa taasisi yake itaendeleza mashirikiano na wafanyabiashara na waingizaji wa bidhaa mbali mbali ili kuhakikisha malengo ya taasisi yake ya kudhibiti ubora wa bidhaa linatimia.

Alisema katika kufikia lengo hilo taasisi hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa uma na kuandaa viwango vya bidhaa mbali mbali zinazozalishwa au kuingizwa nchini ambapo hadi sasa taasisi hiyo imeshaandaa viwango vya bidhaa 113 vikiwemo vya bidhaa za mafuta.

“Mbali ya viwango hivyo lakini pia tumefanikiwa kuwa na maabara ya kisasa inayoweza kupima bidhaa za vifaa vya kieletroniki na mafuta aina zote na tumefanya yote hayo ili kuhakikisha malengo yetu yanayoenda sambamba na malengo ya taifa ya kukuza biashara na ujasiriamali, kudhibiti ubora wa bidhaa na usalama wa watumiaji wa bidhaa hizo yanatimiake”, alisema Mwadini.

Akiwasilisha mada katika semina hiyo Afisa Viwango wa taasisi ya viwango Zanzibar Mukhtar Chande Muumin alieleza kuwa taasisi hiyo baada ya kuandaa viwango vya matairi  na kupitishwa na bodi ya wadhamini inatarajia kuanza ukaguzi wa matairi yanayotarajiwa kuingizwa nchini kuanzia April 1 mwaka huu.

“Kuanzia tarehe hiyo waingizaji na wauzaji wote wa matairi ya vyombo vya moto wanatakiwa kufuata utaratibu na kutumia mahitaji yaliyoelekezwa katika viwango kama fursa pekee ya kuweza kushajihisha matumizi bora na kuijengea jamii na serikali kuepukana na athari zinazoweza kuepukika”, alisema Muumin.

Wakitoa maoni yao katika semina hiyo baadhi ya wafanyabiashara wa matairi walioshirikia semina hiyo waliitaka taasisi hiyo kupunguza ada ya ukauzi iliyopangwa ili kuondoa ongezeko la gharama za uendeshaji wa biashara yao.

Aidha waliitaka taasisi hiyo kuendeleza mashirikiano na jumuiya za wafanyabiashara pamoja na kukaa na taasisi nyengine zinazohusika na utozaji wa kodi ili kupunguza viwango vya tozo mbali mbali ambzo zinachangia kwa kiasi kikubwa ukuzaji wa gharama na kudumaza biashara zao.

“Tunaamini nchi yetu imekuwa ikihimiza ujasiriamali, na wafanyabiashara wengi tunaofanya biashara hii ni wale wadogo wadogo hivyo ada ya shilingi 5,000 kwa kila tairi iliyopendekezwa ni kubwa na kwamba haitosaidia kukuza biashara zetu bali kuididimiza na kupelekea kumkandamiza mtumiaji wa mwisho wa bidhaa hizo”, alisema waziri mbonde.

Nae mwakilishi wa jumuiya ya wafanyabiashara, wenye viwanda na wakulima Zanzibar aliishauri taasisi hiyo kuzingatia maoni ya wadau hao ikiwa pamoja na kusogeza muda wa kuanza kutumika kwa utaratibu kutoka mwezi aprili hadi julai mwaka huu ili kutoa muda kwa wafanyabiasha hao kujipanga.

“Mimi naamini ZBS (taasisi ya viwango Zanzibar) haijaweka viwango hivi kwa ajili ya kupata mapato hivyo ni vyema viwango vya ada vikapitiwa upya lakini pia na muda wa kuanza kwa zoezi hili ili kuwapa muda wadau kujiandaa na kulielewa kwa kina hii dhana ili kuwasaidia kuja kulitekeleza bila ya vikwazo”, alisema Dk. Hafidh kutoka ZCAA   

Semina hiyo iliyolenga kutoa elimu kwa wafanyabiasha wa matairi nchini iliandaliwa na ZBS kwa lengo kujenga uelewa wa pamoja juu ya aina na viwango vya matairi yanayoingizwa nchini ili kupunguza ajali na athari za kimazingira zinazochangiwa na bidhaa zilizo chini ya ubora na viwango.
Mwisho.     
  


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Ali Khamis Juma akifungua semia ya kujenga uelewa wa wafanyabiashara ya matairi ya magari na vyombo vya moto iliyoandaliwa na taasisi ya viwango Zanzibar.



Washiriki wa semina ya semia ya kujenga uelewa wa wafanyabiashara ya matairi ya magari na vyombo vya moto iliyoandaliwa na taasisi ya viwango Zanzibar (ZBS) kuhusu utaratibu wa ukaguzi wa viwango vya bidhaa hizo unaotarajiwa kuanza mwezi April mwaka huu.


Saturday, February 24, 2018

ZANZIBAR HEROES WAKABIDHIWA VIWANJA WALIVYOAHIDIWA

NA MWINYIMVUA NZUKWI
Serikali ya Zanzibar imekabidhi viwanja 33 kwa wachezaji na viongozi wa makamo bingwa wa mashindano ya chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes) ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein aliyoitoa Disemba 24 mwaka jana.

Hafla hiyo iliyoshuhudiwa na waziri wa habari, utamaduni, utalii na michezo Rashid ali juma, iliongozwa na waziri wa ardhi, maji, nishati na mazingira salama adoud talib katika eneo la Tunguu plan wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Akikabidhi hati na maeneo ya viwanja hivyo, waziri salama aliwataka wachezaji hao kuzingatia usia uliotolewa na Dk. Shein wa kuvienzi kwa kuvijenga viwanja hivyo ili kufaidi matunda ya jasho lao.

“Serikali inathamini michezo na nguvu mlizotumia wakati mnapigania heshima ya nchi yetu, hivyo nawakumbusha kuwa Rais (Dk. Ali Mohamed Shein) hatofurahi atakaposikia mmeviuza na hamkuvijenga”, alisema Waziri huyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, waziri juma alisema anashukuru kuona historia nyengine inaandikwa katika medani ya soka na kuwataka wachezaji hao kuendelea kujituma na kulinda viwango vyao katika timu zao wanazozitumikia.

“ninashukuru kuona kuwa serikali imetimiza ahadi yake kama ilivyoiweka. Sasa ni jukumu na wajibu wetu kuendelea kutumia vyema nguvu na akili zetu katika kuendeleza michezo nchini”, alisema Rashid.

Kocha mkuu wa Zanzibar heroes Hemed Suleiman ‘Morocco’ akitioa shukrani kwa niaba ya viongozi na wachezaji wa timu hiyo alimshukuru Rais Dk. Shein na viongozi wengine wa serikali kwa kutimiza ahadi hiyo na kuahidi kuendelea kuikumbuka siku hiyo miaka mingi ijayo.

“Hiki tunachokishuhudia hapa ni deni ambalo linaweza kuchukua muda mrefu kulilipa lakini tunaomba mumfikishie salam zetu za shukrani na ahadi ya kwamba tutaitunza zawadi hii na kuithamini siku zote”, alisema Morocco.


Viwanja hivyo ni zawadi ya 4 kwa wachezaji hao kutoka kwa Dk. Shein baada ya chakula cha mchana, hafla maalum katika taarab rasmi na fedha taslim shilingi milioni 3 kwa kila mmoja baada ya timu hiyo kushika nafasi ya pili katika mashindano hayo baada ya kutolewa na wenyeji Kenya kwa penalti 3 – 2 baada ya timu hizo kutoka sare ya magoli 2 – 2 ndani ya dakika 120.


Mlinda mlango wa timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ Ahmed Salula (wa pili kulia) akipokea hati ya kiwanja chake kutoka kwa Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Abod Talib (kushoto). Anaeshuhudia ni waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Rashid Ali Jumba (wa pili kushoto).

Kikosi cha timu ya Zanzibar Heroes kilichoshiriki fainali za challenji ya wakubwa ya CECAFA mwaka 2017 na kumaliza ya pili nyuma ya Harambee Stars ya Kenya.

'SAND HEROES' USO KWA USO NA WA-AFRIKA KUSINI UFUKWENI KESHO

Na Mwinyimvua Nzukwi
Kocha mkuu wa Mabingwa wa mashindano ya Copa Dar es salam katika soka la ufukweni timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Sand Heroes’ Ali Sharif Adolf  ameeleza kuwa kikosi chake kipo imara kukikabili kikosi cha timu ya taifa ya afrika kusini katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaochezwa Februari 25 mwaka huu katika fukwe za Bububu nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Mchezo huo ambao ni sehemu ya maandalizi ya timu ya Afrika Kusini kwenye changamoto ya kuwania kufuzu katika mashindano ya kombe la dunia, yatatumiwa na  ‘Sand Heroes’ kama maandalizi ya tamasha la mchezo huo linalotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu kama ilivyoshauriwa na rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein alipokuwa akipokea kombe lililochukuliwa na timu ya Zanzibar mwaka uliopita.

Adolf ambae pia ni mwenyekiti wa kamati ya soka la ufukweni Zanzibar alisema lengo la tamasha hilo litakaloshirikisha nchi mbali mbali za ndani na nje ya afrika ni kuitangaza Zanzibar kupitia mchezo huo na kujiimarisha katika viwango vya FIFA.

alisema maandalizi yote yanayohusiana na mchezo huo yamekamilika na Kwamba ameridhishwa na viwango vya wachezaji wake ambao anaamini wataonesha mchezo wa urafiki kwa lengo la kukuza mahusiano kati ya nchi mbili hizo.

“Mchezo huu ni mchezo wa bahati na fursa kwa wale ambao wamekosa bahati ya kushiriki katika soka la kawaida, nadhani tukiitumia vyema fursa hii itasaidia kuitangaza nchi na wachezaji wake na ndio maana tunamtaka kila mmoja wetu aje kushuhudia mchezo huo”, alisema.

Akizungumzia mchezo huo, kocha wa afrika kusini Ntokozo Bhengu alisema wachezaji wake wapo fiti na wana ari kubwa ya mchezo huo.

 “Mbali ya kuamini kuwa tutapata ushindani wakati wa mchezo, lakini tunapaswa kujua kuwa nchi zetu ni marafiki na sisi tumekuja kujifunza utamatuni wa mchezo huu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki baada ya kuwa na uzoefu mkubwa katika mashindano ya ukanda ya COSAFA”, alisema kocha Bhengu.

Alisema amevutiwa na mwaliko waliopewa na kukutana na Zanzibar kutokana na kuwa Zanzibar inashika nafasi ya karibu na nchi yake katika viwango vya FIFA, hivyo anaamini mchezo huo utakuwa na ushindani utakaomsaidia kuimarisha kikosi chake.

Nae Mkuu wa msafara wa timu ya taifa ya Afrika Kusini Ngwenya Kwezakwakhe alielezea kufurahishwa kwa mapokezi na huduma walizopatiwa toka walipowasili na kutoa mwaliko kwa timu ya Zanzibar kufanya ziara kama hiyo nchini kwao.

“Tumehudumiwa vyema toka tulipowasili na kushuhudia sehemu kubwa ya ukarimu wenu kwa wageni na ninaamini hata kama tukipoteza mchezo huu itakuwa ni kwasababu za ushindani na sio mambo mengine”, alisema Kwezakwakhe.


Timu ya Afrika Kusini iliwasili Zanzibar Ijumaa ikiwa na wachezaji 11 na viongozi 7 kwa ajili ya mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya wenyeji wao ‘Sand Heroes’ baada ya timu ya mchezo huo ya Oman kushindwa kujibu mwaliko uliotolewa na Kamati inayosimamia mchezo huo visiwani humu.


Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Zanzibar Ali Shari ‘Adolf’ (kulia) na kocha mkuu wa timu ya taifa ya afrika kusini Ntokozo Bhengu (kushoto) wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya timu hizo utakaochezwa Jumapili Februari 25, 2018 katika ufukwe wa bahari ya Bububu, Zanzibar. 

Thursday, February 22, 2018

VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA - VYOMBO VYATAKIWA KUACHA UTASHI

NA MIZA KONA MAELEZO – ZANZIBAR
Wasimamizi wa sheria na vikosi vya ulinzi na usalama wametakiwa kuacha utashi na kufanya kazi kwa uzalendo ili kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Mkurugenzi mtendaji Tume ya Taifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar Kheriyangu Mgeni Khamis alitoa rai hiyo katika kikao cha pamoja kati ya taasisi hizo kilichofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkokotoni.
amewataka watendaji hao wawe waadlilifu katika ngazi zote za utendaji ili kuweza kudhibiti uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya nchini.
Kikao hicho kiliitishwa na tume hiyo kwa lengo la kujadili namna ya kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya katika mkoa huo kutokana na uwepo wa bandari ndogo ndogo zinazohusishwa kuwa njia zinazotumiwa kuingizwa kwa dawa hizo.
Alisema kuna baadhi ya ya vyombo vya kusimamia sheria havitekelezi vyema majukumu yao na kupelekea kufutwa kwa baadhi ya kesi na hivyo kurudisha nyuma juhudi za serikali za kutokomeza dawa hizo.
Alieleza kuwa wasimamizi wa sheria wakiwa makini na waadilifu pamoja na kushirikiana na jamii, wanaweza kufanya kazi bila ya migogoro na kuwafichua wahalifu wanaofanya biashara haramu ya dawa za kulevya katika mkoa huo.
Mkurugenzi huyo alieleza kwa Mkoa wa Kaskazini umekuwa ukiongoza kwa kesi za dawa za kulevya kutokana na wimbi kubwa la uingizaji na utumiaji wa dawa hizo.
“Ni vyema kuzisimamia ipasavyo sheria ili kuweza kuzuia na kudhibiti uhalifu huu usiingie nchini na kuinusuru na nguvu kazi ya taifa isiathirike na matumizi ya dawa za kulevya”, alisema na kueleza kuwa tume yake imejipanga kuimarisha mfumo utakaodhibiti uingiaji wa dawa hizo nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Vuai Mwinyi Mohammed, akizungumza katika kikao hicho alitaka kubadilishwa kwa sera na sheria zilizopo ili ziendane na mazingira ya sasa pamoja na kuondoa muhali na kudhibiti tatizo hilo nchini.
Wakichangia majadiliano hayo, washiriki wa kikao hicho wameitaka Tume hiyo kuweka maofisa katika ofisi za mikoa watakaoweza kuratibu na kushughulikia suala hilo.
Aidha walitaka hatua kali na za haraka zichukuliwa kwa wanaobainika kujihusisha na biashara hiyo ili kuepukana na usumbufu katika ufuatiliaji wa kesi hizo wanaoupata wasimamizi wa sheria.
Aidha walieleza kuwa ukosefu wa vifaa vya kisasa unapelekea kukosa taarifa za haraka na hivyo kusababisha kuongezeka kwa uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya katika mkoa huo.

Wednesday, February 14, 2018

ASKARI POLISI WATAKIWA KUBAINI VYANZO KUDHIBITI UDHALILISHAJI


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka watendaji wa taasisi za serikali na jeshi la polisi kufanya utafiti wa kina ili kubaini vyanzo vya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia wa wanawake na watoto.

Akifungua mafunzo maalum ya siku kumi
Kwa watendaji wanaoshughulikia makosa ya udhalilishaji wa kijinsia na ukatili wa watoto yaliyoandaliwa na jeshi la polisi, katika makao makuu ya jeshi la polisi Zanzibar alisema endapo jeshi hilo litafanikiwa kubaini chanzo na
viashiria vya matendo ya udhalilishaji itasaidia kupunguza kasi ya matendo hayo yanayoharibu jina la nchi.

Alisema hatua zinazochukuliwa ili kudhibiti kasi ya vitendo hivyo zitafanikiwa iwapo elimu ya kutambua viashiria vyake na kupelekea kupungua na kudhibitiwa katika jamii.

“Wakati tukitafuta njia za kutambua viashiria vya matukio haya ninawaomba muendeleze
Nidhamu na kufanya kazi hii kwa kuzingatia maadili, uzalendo na uwajibikaji katika kutumia nafasi zenu za kutimiza malengo ya kupambana na vitendo hivi pamoja na changamoto zinazowakabili”, alisema RC Ayoub.

Wakizungumza katika mafunzo hayo baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema changamoto wanazokumbana nazo wanaposhughulikia aina hiyo ya uhalifu huo uchache wa elimu na ujuzi unaohusiana na masuala ya udhalilishaji kwa wananchi.

Hata hivyo walisema tatizo la muhali miongoni mwa jamii kunakopelekea jamii kumaliza kesi hizo mitaani jambo linalorudisha nyuma juhudi za serikali na wadau mbali mbali katika kuondosha vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto.

Akizungumza katika mafunzo hayo Kamishna wa kamisheni ya polisi jamii Tanzania, Kamishna Mussa Ali Mussa alisema jeshi la polisi halitamvumilia askari yeyote atabainika kujihusisha na uharibifu wa kesi na ushahidi unaohusiana na kesi hizo.

Aliongeza kuwa jeshi hilo limendaa mikakati mbali
mbali ukiwemo wa uundaji wa madawati ya jinsia ili kuhakikisha kesi za udhalilishaji zinafanyiwa upelelezi wa kina na kuchukuliwa hatua za kisheri na kuwataka watendeji hao kuwa karibu na jamii.




Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud akifungua mafunzo kwa askari polisi na maafisa wa ustawi wa jamii kuhusiana na kudhibiti vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na watoto.


MKATABA HUDUMA KWA WATEJA KUBADILI UTENDAJI WA WATUMISHI WIZARA YA HUUM


NA MWINYIMVUA NZUKWI
WIZARA ya Habari, Utamaduni, Utalii na michezo imesema kutekelezwa kwa mkataba wa utoaji wa huduma kwa wateja utasaidia kuimarisha utendaji na utawawala bora ndani ya wizara hiyo.

Akiwasilisha rasimu ya mkataba huo kwa wadau wa wizara hiyo, watendaji wa idara na wakuu wa vitengo Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji na Utumishi Joseph Kilangi alisema lengo la mkataba huo pia ni utekelezaji wa programu ya kuimarisha utumishi wa umma yam waka 2000.

Alisema programu hiyo inazitaka taasisi za umma kuweka kwa uwazi misingi ya huduma zinazotoa na kuweka viwango vya utoaji wa huduma na kuwataka wadau hao kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo.

Alisema kukamilika kwa mkatàba huo kutawasaidia wadau wa wizara hiyo kukuza kupata huduma bora na kuwa tayari kupeleka malalamiko yao kwa katibu mkuu wa Wizara hiyo pale wanapokosa huduma wanazostahiki.

“Wapokea huduma kutoka katika taasisi zilizomo katika wizara yetu wanatakiwa kwa mujibu wa mkataba huu kuwasilisha malalamiko yao juu ya kutoridhishwa na huduma zinazotolewa ili kuzipatia ufumbuzi lakini pia watendaji wanatakiwa kuutekeleza mkataba huu kikamilifu”, alieleza Kilangi.

Alisema chini ya mkataba huo, mteja atakuwa na haki ya kupatiwa mrejesho wa malalamiko atakayoyawasilisha, kupatiwa huduma kwa haraka na katika muda mfupi na kupatiwa huduma anayoihitaji bila ya ushawishi au kutoa rushwa na zawadi.

 Wakiichangia rasimu hiyo wadau hao waliitaka wizara hiyo kuwa na vipimo vya muda katika majukumu waliyojipangia kuyatekeleza ili iwe rahisi wadau kujua namna ya kupata au kudai huduma zinazotolewa na taasisi za wizara hiyo.

Walisema pamoja na mkataba huo kuwa na maelezo ya jumla katika majukumu ya idara na vitengo vya wizara hiyo ni vyema vitengo hivyo vingeanishiwa majukumu mahsusi ili iwe rahisi kuwajibika juu yake.

“wizara ina majukumu makubwa na ingekuwa vyema kama kila kitengo kingeeleza mambo yatakayoyafanya na kuwa ni ahadi ili mwisho wa siku iweze kupimwa kutokana na mipango hiyo”, alisema usi mohammed usi kutoka wizara ya nchi ofisi ya rais, tawala za mikoa, serikali za mitaa na idara maalum za SMZ.

Aidha wadau hao waliitaka wizara hiyo kuzingatia kwa kina majukumu ya kila idara na kuhakikisha zinaweshwa kwa kupatiwa mafunzo na bajeti ya kutosha ili wawe na uwezo wa kutekeleza mkataba huo kikamilifu.

Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za wajumbne wa kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano ya wizara hiyo kikwajuni, afisa utumishi kutoka tume ya utumishi Zanzibar maulid sheha alisema uanzishwaji wa mikataba hiyo ni sehemu ya utekelezaji katika sekta ya utumishi wa umma na kwamba maoni yaliyotolewa na wadau hao yatazingatiwa.

“Tafiti mbali mbali zimebainisha uwepo wa ufanisi katika utumishi wa umma mahali ambapo kuna mikataba ya utoaji huduma kwa wateja kwani watumishi wote huwa wamejifungamanisha na mikataba hiyo na wateja huwa na nafasi ya kulalamika pale wanapoona hawajatendewa haki”, alisema ofisa huyo.



Mkurugenzi wa idara ya uendeshaji na utumishi katika wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Joseph Kilangi akiwasilisha rasimu ya mkataba wa utoaji huduma kwa wateja wa wizara yake kwa wadau wa wizara hiyo.


Afisa utumishi wa idara ya utumishi serikalini Maulid Shehe akitolea ufafanuzi baadhi ya hoja zilizotolewa na wajumbe waliohudhuria kikao cha kupitia rasimu ya mkataba wa utoaji wa huduma kwa wateja wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo (WHUUM).





Baadhi ya wajumbe walioshiriki kikao cha kupitia rasimu ya mkataba wa utoaji wa huduma kwa wateja wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo (WHUUM) Zanzibar.


Tuesday, February 13, 2018

"MABARAZA YA WADI NA KAMATI ZA MASHAURIANO YATAPUNGUZA URASIMU, KUCHOCHEA KASI YA MAENDELEO YA JAMII" - WAZIRI KHERI



NA MWINYIMVUA NZUKWI
Imeelezwa kuwa kuanzishwa kwa mabaraza ya wadi na kamati kwa za mashauriano za shehia kutachochea kasi ya maendeleo, demokrasia na kupunguza urasimu katika utekelezaji wa shughuli za serikali.

Waziri wa nchi ofisi ya rais, tawala za mikoa, serikali za mitaa na idara maalum za SMZ Haji Omar Kheri ameeleza hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Zanzibar akieleza kuwa kufanya hivyi pia ni utekelezaji wa katiba ya Zanzibar ya 1984.

Alisema katiba ya Zanzibar inatambua uwepo wa serikali za mitaa ambazo uchaguzi wa viongozi wake, madaraka na kazi zake zitakuwa kama zinavyoelekezwa na sheria za mamlaka ya serikali za mitaa namba 7 ya mwaka 2014.

Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo serikali za mitaa zina ngazi mbili ambazo ni mabaraza ya manispaa au miji kwa maeneo ya mijini na halmashauri za wilaya katika maeneo ya vijijini.

Alisema mabaraza ya wadi na kamati za ushirikiano za shehia ni vyombo vya kiutendaji vitakavyokasimiwa madaraka ya kutoa huduma bora na endelevu kwa wananchi jkw kuzingatia misingi ya utawala bora.

“Misingi mikuu ya utawala bora ni pamoja na kuwepo kwa dhana ya ushirikishwaji, wa wananchi katika kubuni, kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo katika maeneo yao kwa kuzingatiwa uwazi na uwajibikaji”, alisema waziri Kheri.

Alisema ili kuyaweka mabaraza hayo kuwa na ufanisi ofisi yake imeandaa miongozo iliyozinduliwa Februari 13, 2018 ambayo inatoa taaluma kwa masheha na madiwani wote ambao kwa mujibu wa sheria wanapewa jukumu la kuwa viongozi wakuu wa vyombo hivyo.

“Ushiriki wa wananchi wote katika mabaraza haya ni haki ya kila mwananchi na hatutarajii wananachi kubabaishwa katika kupata haki yao hii kwa sababu yeyote ile isiyokubalika kwa kuwa miongozo hii imeandaliwa kwa lugha nyepesi kwa kila anaetaka ufafanuzi”, alisisitiza.

Aidha alieleza kuwa wizara yake itaendelea kutoa miongozo na elimu kwa watendaji mbali mbali watakaohusika katika uundwaji wa vyombo hivyo na kuwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika michakato ya uundwaji wake.

Akizungumzia utekelezaji wa mpango wa ugatuzi wa madaraka ulioanza kutekelezwa mwezi Julai 1, 2017, waziri kheri alisema tathmini iliyofanywa imebainika kuwepo kwa mafanikio makubwa katika sekta zilizogatuliwa kutokana na kuwepo kwa usimamizi wa karibu ulioleta ufanisi.
“Kuna tofauti kubwa ya kiutekelezaji na kiusimamizi wa majukumu ya maafisa wa sekta zilizogatuliwa kutoka serikali kuu jambo ambalo linatupa moyo kuwa tuanaweza kuwa na ufanisi mkubwa katika maeneo mengine”, alisema.

Dhana ya ugatuzi wa madaraka kutoka serikali kuu kwenda katika serikali za mitaa Zanzibar imeanza katika sekta za afya ya msingi, elimu ya maandalizi na msingi pamoja na kilimo ambazo zipo chini ya usimamizi wa wakurugenzi wa manispaa na halmashauri za wilaya.


Kwa mujibu wa sheria namba 7/2014 ya serikali za mitaa vyombo hivyo vitaundwa na watu wa kada mbali mbali wanaoishi katika maeneo husika kwa ya kuteuliwa na wakuu wa wilaya baada ya kuomba nafasi hizo miongoni mwa watu wenye sifa za kitaaluma na kuheshimika na jamii husika.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri akifafanua jambo wakati alipokuwa akijibu maswali katika kutoka kwa Waandishi wa Habari baada ya kutoa taarifa kuhusiana na kuanzishwa Mabaraza ya Wadi na Kamati za Mashauriano za Shehia.



Mwandishi wa Habari wa kituo cha ITV - Zanzibar Farouk Karim akimuuliza maswali Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir mara baada ya kutoa taarifa kuhusu uanzishwaji wa  Mabaraza ya Wadi na Kamati za Mashauriano za Shehia katikas mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Kikwajuni Mjini Zanzibar.


Afisa  wa Habari wa idara ya Habari Maelezo zanzibar Salum Vuai Issa akiuliza swali kutaka ufafanuzi juu ya taarifa ya uanzishwaji wa Mabaraza ya Wadi na Kamati za ushauri za shehia iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Haji Omar Kheri.



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Haji Omar Kheir akizungumza na Waandishi wa Habari  kuhusiana na  kuanzishwa Mabaraza ya Wadi na Kamati za Mashauriano za Shehia.