NA MWINYIMVUA NZUKWI
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa Dk. Hussein Ali Mwinyi wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewahimiza
wadau wa maendeleo nchini kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na
jumuiya ya kiislamu ili kufikia malengo ya kusaidia wananchi katika
masuala mbalimbali likiwemo la afya.
Akizindua kambi ya uchunguzi wa afya na
matibabu katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar iliyoandaliwa kwa pamoja na Jumuiyat
Akhalqul Islamiya (JAI) kwa kushirikana na madaktari wa Jumuiya ya Jamii Bora
Health Services, taasisi MIMI na WEWE, Wizara ya Afya na Ofisi ya Mkuu wa mkoa
wa Mjini Magharibi, Dk. Mwinyi amesema hatua hiyo itasaidia jumuiya hizo katika
kutoa huduma za afya kwa wananchi wengi na kwa wakati.
Amesema kuwa kila mtu anawajibu wa
kutoa sadaka kwa lengo la kuwasidia watu wenye mahitaji na wasiojiweza jambo
ambalo litapelekea kupata nyongeza ya kheri kutoka kwa Mwenyezi Mungu hivyo ipo
haja ya kila mwanajamii kutoa michango yao kwa mujibu wa uwezo alionao kwa
lengo la kujenga jamii yenye amani, upendo na maelewano.
“Jumuiya hii ina malengo makubwa na
bila ya kuungwa mkona na wadau mbali mbali wakiwemo wafanyabiashara, viongozi
wa serikali, balozi za nchi mbali mbali na wadau wengine ni vigumu kuweza
kufikiwa hivyo ninatoa wito kwa kila mmoja wetu kutoa sadaka yake ili kuchangia
kufikiwa kwa malengo ya jumuiya hii”, amesema Dk. Mwinyi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Afya Zanzibar
Hamad Rashid Mohammed amewataka madaktari nchini
pamoja na kufanya kazi katika taasisisi zao kuanzisha utaratibu wa kutoa
huduma za afya bure kila sehemu kwani kufanya hivyo kutasaidia
kuondoa matatizo ya kiafya yanayowakabili wananchi wengi na kupata
watu wenye afya bora.
Waziri Hamad amezipongeza taasisi
zilizoshirikiana kutoa huduma kwa kuamua kufanya jambo hilo katika mkoa wa Mjini
Magharibi kwa kuwa limetoa funzo katika jamii juu ya
umuhimu wa kujitolea kwa ajili ya wananchi katika vita dhidi ya maradhi mbalimbli hapa nchini.
“Hatua ya ndugu zetu hawa ya kufanya
uchunguzi wa maradhi ni somo jipya linalopaswa kuzingatiwa na kiola mmoja wetu
ili tuondokane mna ile tabia ya kwenda hospitali baaya ya kuumwa kwani mtu
anapojua mapema afya yako mapema inasaidia piaserikali kujua ni namna gani ya
kukabiliana na maradhi yanayowakabili zaidi watu wetu”, amesema.
Aidha aliwashauri madaktari wa Zanzibar
kuiga utaratibu ulioanzishwa na madaktari wa Tanzania bara wa kuanzisha jumuiya
na kutoa huduma kwa jamii kwa kujitolea ili kusadia kutanua wigo wa utoaji wa
huduma za matibabu kwa wananchi wa pandew zote mbili za jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mjini
Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud ameziomba jumuiya hizo kuendelea kuisaidia
jamii katika shughuli nyengine za kijamii ili kuondoa changamoto mbali mbali
zinazokabili wananchi wa Tanzania.
Amewapongeza kwa uamuzi wao wa kutoa
huduma hizo kwa wananchi wa mkoa wake na kuwataka wananchi hao kutumia
kikamilifu fursa hiyo ambayo itahusisha uchangiaji wa damu, upimaji na
uchunguzi wa maradhi mbali mbali yakiwemo ya saratani za matiti, tezi dume na
shingo ya kizazi.
“Hakika kulikubali kwetu kwa haraka
jambo hili linaonesha utayari wetu wa kushirikiana na taaasisi za kiraia katika
kustawisha huduma za jamii yetu na niwaombe wennzetu wa JAI pamoja na kuwa hii
ni mara yao ya kwanza kufanya kazi hii hapa Zanzibar, naomba isiwe mara ya
mwisho kwani bila shaka wahitaji wataendelea kuwepo hata baada ya kambi
kufungwa hapo kesho”, amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Kambi hiyo ya siku mbili inaendeshwa
na zaidi ya wataalamu wa afya 60 wakiwemo madaktari bingwa wa maradhi mbali
mbali yakiwemo ya moyo, kina mama na watoto ambapo Dk. Mwinyi aliichangia
jumuiya ya JAI shilingi milioni 5 na Waziri wa Afya
Zanzibar Hamad Rashid alinunua msahafu ulionadiwa katika hadhara hiyo kwa shilingi
milioni 1 kama sadaka yake kwa jumuiya hiyo kwa lengo la kuendeleza
harakati zake.
No comments:
Post a Comment