Saturday, August 4, 2018

SHEHA ATUMBULIWA KWA KUKIUKA MAADILI


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharib Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud ametengua uteuzi wa sheha wa shehia ya Kisima Majongoo, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi Ali Suleiman Ali baada ya kuthibitika kukiuka maadili ya viongozi wa umma.

Akizungumza na vyombo vya habari, Katibu Tawala wa mkoa wa huo Hamida Mussa Khamis (pichani) amesema shehia hiyo itakuwa wazi hadi atakapoteuliwa sheha mwingine na kuwaonya viongozi hao kuwa makini katika utendaji wao.


Ameeleza kuwa hatua hiyo imekuja kufuatia mamalaka aliyopewa chini ya kifungu namba 9 cha sheria namba 8 ya tawala za mikoa ya mwaka 2014 na kwamba pamoja na hatua hiyo ya kinidhamu, sheha huyo atashughulikiwa hatua za kisheria kulingana na makoasa aliyoyafanya .
"Huyu ni miongoni mwa masheha wapya walioteuliwa mwaka jana, lakini kutokana na uzito wa makosa aliyoyafanya tumeanza na hatua hii kama sheria inavyotuongoza na mamlaka nyengine zinaweza kuendelea kuchukua hatua za kisheria", ameeleza katibu huyo.

Katibu huyo amewakumbusha viongozi wa ngazi mbali mbali ndani ya mkoa huo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyowekwa ili kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa ajili ya wananchi.

Shehia ya Kisima Majongo ni miongoni mwa shehia 121 ziliomo ndani ya mkoa wa Mjini Mgharibi ambapo sheha huyo aliteuliwa mwezi Julai mwaka jana baada ya shehia hiyo kuwa wazi kwa muda kufuatia kifo cha aliekuwa sheha wa shehia hiyo Ali Khamis Makame.

No comments:

Post a Comment