NA MWINYIMVUA NZUKWI
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.
Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amesema CCM taasisi inayothamini juhudi na
mchango wa kuwasadia watoto yatima zinazofanywa na wadau wa maendeleo kutoka ndani
na njue ya nchi.
Hayo aliyasema wakati
alipotembelea Kituo cha kulelea watoto yatima kinachodhaminiwa na shirika la ‘Direct
AID’ la Kuwait kilichopo Mwanakwerekwe uwanja wa Ijitimai ya zamani Unguja.
Dk. Mabodi alieleza kuwa ameridhishwa na juhudi za kituo
kinachowapatia malezi bora watoto yatima wanaolelewa na shirika hilo na
aliliashukuru shirika hilo kwa kufanya kazi ya kuisaidia Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika masuala ya kijamii hususani ya uimarishaji wa huduma za maji
safi na salama na elimu.
Dk. Mabodi alisema kwamba CCM
itaendelea kuwa karibu na mashirika mbali mbali yenye dhamira ya kuendelea
kuunga mkono juhudi za serikali katika kutatua kero na changamoto za
jamii.
Amefafanua kwamba watoto
ambao wazazi wao wamefariki wasipotunzwa na kuhudimiwa vizuri wanaweza kukosa
haki zao za msingi zikiwemo malezi mazuri na elimu bora hivyo ipo haja kwa wananchi
wa maeneo mbali mbali kuwa karibu na watoto hao kwani wengi wao wanakuwa
wakitengwa na kufanyiwa vitendo vya udhalilishwaji vikiwemo vya kutopatiwa
huduma muhimu za kibinadamu.
“CCM tutakuwa karibu zaidi na
Direct AID kwani mmeamua kuisaidia jamii yetu nasi lazima tuonyeshe ungwana
wetu wa kushirikiana nanyi kutatua changamoto zinazowakabili katika upangaji wa
mikakati yenu ya kuisaidia jamii”, alisema Dk. ‘Mabodi’.
Nae Mkurugenzi wa shirika
hilo, Dk. Ayman Mohamed alisema shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kuwapatia
elimu watoto hao ili waweze kujitegemea mara baada ya kumaliza muda wa kuishi
katika kituo hicho.
Alisema kituo hicho kimetoa
vijana wengi wasomi wanaofanyakazi katika sekta mbali mbali za serikali na
binafsi na kuesisitiza kuwa taasisi yake itaendelea kutekeleza malengo yake kwa
kujenga vituo vya kisasa vya kulelea watoto yatima vitakavyokuwa na shule,
vituo vya Afya na vyuo vya masomo ya dini ya kiislamu kwa Unguja na Pemba.
Akizungumza mmoja ya vijana
waliolelewa katika Kituo hicho, Mhandisi Abdullah Salum Kassim alisema
kituo hicho kimemlea akiwa na umri mdogo na kumsomesha hadi ngazi ya elimu ya
juu ambapo hivi sasa ni mtumishi serikalini.
Alikiri kuwa mafanikio hayo
yametokana na utaratibu mzuri uliowekwa na serikali wa kuruhusu shirika la
Direct AID kuwasaidia watoto yatima.
“Shirika hili limenilea
nikiwa mtoto mdogo na kunisomesha mpaka nimekuwa mtu mzima mwenye familia
ambaye pia nawasaidia vijana wenzangu ambao nao wazazi wao walifariki wakiwa
wadogo”, alifafanua Mhandisi Abdulahi.
Nae Diwani wa Wadi ya
Meli nne, Saleh Juma Kinana ambaye pia ni miongoni mwa vijana waliolelewa
katika Kituo hicho, alisema watoto yatima wanatakiwa kulelewa na kuthaminiwa
kama walivyo watoto wengine katika jamii.
Kituo hicho kinafuata malezi
na miongozo ya dini ya Kiislam kina jumla ya watoto 44 ambao ni watoto yatima.
No comments:
Post a Comment