Monday, August 13, 2018

UTPC YAANZA KUWANOA WAANDISHI WA HABARI, WANACHAMA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Muungano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC) umeanza kutekeleza mpango wa mafunzo kwa wanachama wa klabu za waandishi wa habari nchini Tanzania kuanzia leo.

Taarifa iliyotolewa na Afisa programu za mafunzo, utafiti na machapisho wa UTPC Victor Maleko kwa klabu za waandishi wa habari Tanzania imeeleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuimarisha uwezo wa kitaaluma wa waandishi wa habari na kuleta mabadiliko katika jamii.

Alisema hatua hiyo inafuatia kukamilika kwa uchambuzi wa maombi ya wanachama wa klabu hizo yaliyofanywa miezi miwili iliyopita na kwamba waandishi hao watapatiwa mafunzo mbali mbali kuanzia mwezi wa Agosti 2018

“Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa UTPC wa 2016 - 2020 ambapo waandishi watapatiwa mafunzo kisha kupatiwa mikataba ya kufanya kazi ili kutathmini ufanisi wa mafunzo yanayotolewa”, alieleza.

Aliongeza kuwa kundi la kwanza la waandishi hao linatarajiwa kuanza kupatiwa mafunzo ya uandishi wa habari za mazingira yatakayofanyika mkoani Morogoro kuanzia Agost13 - 27 mwaka huu wakati kundi la pili litashiriki mafunzo ya uchambuzi wa sera na ufuatiliaji wa bajeti yatakayofanyika mkoani Pwani na kufuatiwa na mafunzo ya habari za uchunguzi kati ya Agosti 14 na 17 mwaka huu.

Maleko alieleza kuwa kwa mwaka 2018 mbali na mafunzo hayo, wanachama wa klabu za waandishi wa habari Tanzania watajengewa uwwzo wa uandika  habari za jinsia, habari za afya, habari za haki za binadamu na utawala bora, misingi na maadili ya uandishi wa na mafunzo ya utangazaji.

Afisa huyo amewataka waandishi waliobahatika kupata nafasi hiyo kuitumia kikamilifu na kujifunza kwa lengo la kubadilisha uandishi wao unaotarajiwa kuleta mabadiliko katika jamii.

Akizungumzia hatua hiyo Katibu Mkuu wa klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC) Faki Mjaka mbali ya kuwapongeza wanachama wa klabu hizo kwa kuteuliwa kuhudhuria mafunzo hayo na kuwataka kuitumia vyema fursa hiyo ili kutimiza ndoto zao za kujiimarisha katika taaluma ya uandishi wa habari.

Alisema iwapo waandishi hao watashiriki na kuzingatia mafunzo hayo kuna uwezekano wa kupatikana mabadiliko makubwa katika tasnia ya habari na taifa kwa ujumla.

Aidha aliipongeza sekretarieti ya UTPC kwa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata mipango iliyoidhinishwa na vikao vya juu vya taasisi hiyo na kuwaomba wakuu wa vyombo vya habari nchini kuwaruhusu waandishi wao ili washiriki mafunzo hayo yatakayosaidia kuimarisha utendaji wa vyombo vyao.

"Kutokana na utaratibu wa UTPC mwandishi anaomba mwnyewe aina ya mafunzo, unaongeza uthubutu, uwajibikaji na kubadililisha mitazamo ya wanachama wetu hivyo ninawaomba wawe wepesi kutumia hizi fursa", alisisitiza Mjaka.

Zaidi ya wanachama 50 wa klabu za waandishi wa habari nchini wakiwemo wanachama 6 wa klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC) wanatarajiwa kushiriki mafunzo ya uandishi wa habari za uchunguzi, habari za mazingira na habari za uchambuzi wa sera na ufuatiliaji wa bajeti kuanzia Agosti 13, 2018 yatakayofanyika katika mikoa Morogoro, Pwani na Dodoma.


No comments:

Post a Comment