Sunday, August 19, 2018

"HATUKURUPUKI KUWEKEZA KATIKA MIRADI YA MAENDELEO" - DK. SHEIN


NA MWINYIMVUA NZUKWI, ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa uwekezaji unaofanywa katika maeneo mbali mbali unalenga kukuza uchumi na kunguza tatizo la ajira kwa wananchi wa Zanzibar.

Akizindua biashara katika mji mdogo wa Fumba unaojengwa na kampuni ya CPS-lives katika shehia ya Nyamanzi wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, Dk. Shein alisema hatua hiyo inachukuliwa na kutekelezwa kwa umakini kati ya serikali na sekta binafsi.

Alisema katika kuekeleza dhana ya uhusiano kati ya serikali na sekta binafsi (PPP), serikali yake imeweka miundombinu rafiki ya kuiwezesha sekta binafsi kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo ya makaazi badala ya serikali kutekeleza miradi hiyo.



Alisema miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuanzisha ukanda wa maeneo huru ya kiuchumi na kuipa juklumu mamlaka ya ukuzaji vitega uchumi Zanzibar (ZIPA) inatekeleza mipango mbali mbali na ilani ya uchaguzi wa CCM ili kuongeza kasi ya maendeleo ya jamii.

Aliitaja mipango hiyo kuwa ni dira ya Maendeleo 2020, mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini Zanzibar (MKUZA III) na ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo ilirithi ilani ya chama cha Afro Shiraz Party (ASP) iliyoitumia wakati wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 1961 na 1962.

 “ASP iliweka ahadi ya kujenga na kuyaendeleza makaazi ya wananchi wa Zanzibar ambao wengi wao walikuwa na makazi duni azma ambayo inaendelezwa na CCM (Chama Cha Mapinduzi) baada ya mapinduzi ya 1964 na hadi sasa kupitia ilani ya uchaguzi ambayo zinaelekeza serikali zake kwa kushirikiana na sekta binafsi”, alieleza Dk. Shein.

Alisema licha ya uwezo mdigo ilionao serikali yake itaendelea kujenga na kuiiimarisha miji midogo na mji mikongwe wa Zanzibar na kutoa ushirikiano na wawekezaji sambamba na kuzingatia usafi ili kuwavutia wageni na kujikinga na maradhi.



Aidha Dk. Shein aliipongeza kampuni ya CPS-Lives kwa kufanikisha ujenzi wa mradi kwa kasi na kiasi cha kukamilisha nyumba hizo katika kipindi kifupi na kwa kutumia teknolojia inayozingatia uhifadhi wa mazingira.

“Tulipokuja kuuwekea jiwe la msingi mwezi Januari mwaka huu hali haikuwa hivi. Hivyo sina budi kuwapongeza wawekezaji wa mradi huu kwa kutimiza ahadi waliyoiweka wakati ule kuwa wangekabidhi sehamu ya nyumba hizi kwa wateja wao na leo tumeshuhudia wateja 60 waliokamilisha malipo wamekabidhiwa nyumb zao”, alisema Rais Dk. Shein.

Mapema akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohammed alisema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya uwekezaji inayotekelezwa  kwa faida nchini kutokana kodi inayolipwa serikalini na faida nyengine ikiwemo ya upatikanaji wa ujuzi.

Alisema mradi huo una lenga kuweka haiba ya Zanzibar na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, utasaidia kupunguza msongamano katika maeneo ya mji wa Zanzibar.

“Wawekezaji katika mradi huu ni walipa kodi wazuri na wametoa ajira za kudumu 250 na ajira za muda zaidi ya 500 sambamba na fursa za mafunzo ya utunzaji wa mazingira jambo ambalo limesaidia kutimiza malengo ya kuhimiza uwekezaji nchini mwetu”, alisema Dk. Khalid.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya CPS-Lives Sebastian Dietzold alimshukuru Dk. Shein kwa kuendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kuwa kampuni yake itaendelea kushirikiana na serikali ya mapinduzi Zanzibar.

Amesema toka kuasisiwa kwa mradi huon jumla ya nyumba 400 za awamu ya kwanza zimeshauzwa na 60 katin ya hizo zimekabidhiwa kwa wenyewe katika uzinduzi huo kazi ambayo inatarajiwa kufanyika kila mwezi.

“Mradi wetu umekuwa na manufaa makubwa sio kwetu bali pia kwa vijiji vya karibu yetu vya nyamanzi na dimani kwa kusaidia upatikanaji wa huduma za jamii i pamoja na kuwapatia ajira watu kutoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar”, alieleza.


Aliongeza kuwa baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi huo baadae mwaka huu, awamu ya tatu ya utekelezaji wa mradi huo utaanza ambao utahusisha ujenzi wa majengo ya huduma za jamii na viwanda.

Awali Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya ukuzaji vitega uchumi Zanzibar (ZIPA) Salum Khamis Nassor alieleza kuwa uendelezaji wa eneo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango ulioasisiwa na serikali ya awamu ya 5 iliyoyatangaza maeneo ya Fumba na Micheweni kuwa ni maeneo huru ya uchumi mwaka 1992.

Alieleza kuwa uamuzi huo ulilenga kuimarisha uchumi wa Zanzibar kwa kushirikiana na sekta binafsi kazi ambayo inaendelea kutekelezwa na mamlaka yake kwa kuzingatia sera na sheria za nchi.

Makabidhiano ya nyumba hizo umekuja baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi huo ambapo nyumba 400 za awali kati ya 2000 zilizokusudiwa kujengwa katika awamu hiyo inayotarajiwa kukamilika baadae mwaka huu.
Mwisho.
    


No comments:

Post a Comment