NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. Bashiru Ali ameeleza kwamba
CCM imejipanga na kuanza kuchukuwa hatua za kukabiliana na makundi yenye tabia
na nia ya kudhoofisha taasisi hiyo kongwe katika siasa nchini Tanzania.
Alisema Chama hicho kimeumizwa sana na tabia hiyo mbovu
isiyokubalika aliyoifananisha sawa na ugonjwa wa kansa ambayo huchangia pia
kuwachafua viongozi na wanachama wake.
Akijitambulisha rasmi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, katika ofisi za
Makamu wa Pili Vuga Mjini Zanzibar Dk. Bashiru alisema kinachohitajika sasa ni
kuimarishwa kwa chama hicho chenye uwezo wa kuendelea kulinda na kusimamia
Uhuru pamoja na Ukombozi wa Taifa hili.
Dk. Bashiru alieleza kwamba katika muelekeo wa uendelezaji wa CCM imara
iliyoanza kurejesha imani kwa Wananchi walio wengi suala la makundi limefikia
kikomo cha kuepukwa kabisa kwa vile liko sawa na najisi kwa watu
wenye Imani za Kidini.
Katibu Mkuu huyo wa Chama cha Mapinduzi alimueleza Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar kwamba CCM kamwe haitokubali kushindwa na makundi ya Watu
wasiokuwa na muelekeo wa ulinzi wa Ukombozi.
“ Katika utumishi wangu wa Chama katika nafasi ya
utendaji Mkuu sitokubali kuchafuka wala kuchafuliwa, wala kuwachafua Viongozi
wetu Wakuu walioniamini kunipa utumishi huu muhimu katika Chama chetu”.
Alisisitiza Dk. Bashiru.
Aliwataka Viongozi waliopewa fursa za kuwatumikia Wananchi moja kwa moja
hasa Majimboni kuacha tabia ya kupayuka payuka ovyo kwa vile kinachowapa nguvu
ni Heshima ya chama wala si ubinafsi unaoweza kuwavuruga Wananchi wao.
Akigusia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliyopata ridhaa ya
Wananchi ya kuongoza Dola Bara na Zanzibar Katibu Mkuu wa
CCM Dk. Bashiru aliwaagiza Watendaji wa Serikali zote mbili
kuendelea na uratibu wa utekelezaji wa kazi za Ilani ndani ya Serikali hizo.
Alisema Ripoti ya Utekelezaji huo wa Ilani utakaoainishwa kwa pamoja wa
Serikali zote mbili utapaswa kuwasilishwa katika Uongozi wa juu wa Halmashauri
Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi.
Alifahamisha kwamba kitabu kitakachotayarishwa kutokana na Ripoti hiyo
ya Utekelezaji wa Ilani wa Serikali zote mbili kitaweza kusaidia kujua masuala
yote yatakayoibua mafanikio na changamoto zinazowakabili Wananchi katika maeneo
yote Mjini na Vijijini.
Katibu Mkuu huyo wa CCM Taifa alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Braza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa uamuzi na busara zake za
kuiongoza Zanzibar katika mfumo aliyouanzisha wa Kushirikisha Viongozi na
Wananchi moja kwa moja katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.
Dk. Bashiru alisema mfumo huo ambao Tanzania Bara haupo hutoa fursa kwa
Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Watendaji Wakuu wa ngazi zote za Serikali
kuafuatilia changamoto zinazowakabili Wananchi na matokeo yake yamekuwa chachu
ya Maendeleo yanayopatikana kutokana na ushiriki wa kila Mwananchi.
Alisema katika kufanikisha maendeleo hayo Dk. Bashiru alishauri Kamati
Maalum ya CCM Zanzibar iendelee kupewa nafasi yake katika masuala yote ya
Kisiasa yanayoihusu Zanzibar.
Alisema Kamati Maalum iliyoundwa na Chama cha Mapinduzi kwa
kuzingatia mazingira Maalum ya Zanzibar lazima iheshimike kwa vile imeundwa kwa
mujibu wa Katiba na Kanuni za Chama hicho.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
alisema Zanzibar Kisiasa bado iko salama licha ya upinzani mkubwa
unaojitokeza wakati wa chaguzi mbali mbali zinazohusisha Vyama vya CCM na CUF.
Balozi Seif alisema wakati amani hiyo inaendelea kuwapa fursa
Wananchi kuendelea na harakati zao za kimaisha Uongozi wa CCM Zanzibar
unaendelea kujiweka tayari ili ujihakikishie inaendelea kuongoza Dola kwa
upande wa Zanzibar ifikapo Mwaka 2020.
Dk. Bashiru Ali aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM baada ya Halmashauri
Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi kujiridhisha na sifa na uwezo aliyonao na
kupewa jukumu hilo zito la kukisimamia Chama hicho kikiwa miongoni mwa Vyama
vikongwe Barani Afrika.
No comments:
Post a Comment