KATIBU Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Dk.Bashiru Ally anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku nne
visiwani humu Agosti 17 hadi 20 mwaka huu.
Dk.Bashiru anafanya ziara hiyo
kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo Mei mwaka huu baada ya
aliyekuwa Katibu Mkuu Abdulrahman Omar Kinana kustaafu.
Akitoa taarifa ya ziara hiyo ya
Katibu Mkuu huyo, Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu Taifa(NEC),Idara
ya Itikadi na Uenezi CCM, Zanzibar Catherine Peter Nao, alisema CCM Zanzibar
tayari kimekamilisha maandalizi yote ya mapokezi ya kiongozi huyo.
Catherine alisema katika ziara
yake hiyo pamoja na mambo mengine anatarajia kuzungumza na viongozi mbalimbali
wa CCM na jumuiya zake na makundi ya kutoka taasisi za vijana visiwani humu.
Aliongeza kuwa ziara hiyo ya
Dk.Bashiru itakuwa ni ya kikazi na kujitambulisha kwa wana-CCM ambapo
wanatakiwa kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Katibu Mkuu huyo ambapo
atawahutubia wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla katika uwanja wa Ofisi Kuu
ya CCM Kisiwandui saa 9 alasiri.
“Tunawaomba wanachama wote
tujitokeze kwa wingi kushiriki mapokezi hayo ya kiongozi wetu mpendwa ambaye ni
mara ya kwanza kuja tukitambulisha na kuzungumzia sera na masuala mbalimbali ya
kuimarisha CCM na Jumuiya zake, alisema Catherine.
Akizungumzia ratiba ya ziara
hiyo Katibu huyo wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar,Catherine alisema
siku ya siku ya kesho Agosti 17 mwaka huu katibu Mkuu huyo atakutana na
kuzungumza na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Katibu huyo aliongeza kuwa
Dk.Bashiru anatarajia kukutana na na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa
ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.
Alisema mchana wa siku hiyo ya
ijumaa atazuru Kaburi la Muasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Hayati Mzee
Abeid Karume na kuzungumza na watumishi pamoja na Wazee wa CCM Zanzibar ambapo
jioni atazungumza na Viongozi na wanachama wa Mikoa minne ya CCM Unguja hapo
katika viwanja vya CCM Kisiwandui.
Catherine aliendelea kueleza
kuwa jumamosi ya Agosti 18 mwaka huu Katibu Mkuu huyo atazungumza na Wenyeviti
wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Makatibu wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Kamati za siasa
za Mikoa na Wilaya, Wabunge, Wawakilishi na madiwani katika ukumbi wa Kamati
Maalum Kisiwandui pamoja na kuzungumza na makundi ya vijana katika ukumbi wa
CCM Mkoa wa mjini.
Aliongeza kuwa siku ya Jumapili
Agosti 19, mwaka huu Katibu Mkuu huyo asubuhi atasafiri kuelekea Pemba kwalengo
la kuendelea na ziara yake hiyo ambapo atazungumza na Watumishi wa CCM
na wazee wa Pemba katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Kitengo.
Katibu huyo alisema Dk.Bashiru
anatarajia kuzungumza na viongozi na wanachama wa CCM wa Mikoa miwili katika
ukumbi wa skuli ya Fidel Castro Mkoa wa Kusini Pemba na jioni anatazungumza na
Wenyeviti wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Makatibu wa CCM wa Mikoa na Wilaya, Kamati
za siasa za Mikoa na Wilaya, Wabunge, Wawakilishi,madiwani na maafisa wadhamini
katika ukumbi wa Makonyo Pemba.
Katibu Mkuu huyo atahitimisha
ziara yake hiyo siku ya Juma tatu Agosti 20 mwaka huu, kwa kuzuru kaburi la
Dk.Omar Ali Juma kisiwani Pemba na kumalizia ziara yake kwa kuzungumza
na makundi ya vijana ambapo jioni atasafiri kuelekea Dar es salaam
kuendelea na majukumu mengine.
No comments:
Post a Comment