Wednesday, August 15, 2018

KZU WADHIBITI MOTO MKUNAZINI, RC AYOUB AWATAKA WANANCHI KUCHUKUA TAHADHARI


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar (KZU) Agosti 15, 2018 kimefanikiwa kuuzima moto uliozuka majira ya saa moja usiku katika moja ya majengo yaliyopo nyuma ya soko kuu la kuku shehia ya Mkunanizi, mjini Unguja.



Jengo hilo linalotumika kwa biashara na makaazi ya binadamu, linamilikiwa na Haroub Suleiman Nassor ambae amelikodisha kwa hoteli ya Marumaru linatumika kwa makaazi ya wanafunzi wanaofanya mafunzo ya vitendo katika hoteli hiyo pamoja na walimu wao.


Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud (katikati) akizungumza na wanahabari wakati wa shughuli ya uzimaji wa moto. kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Hamida Mussa Khamis.

Akizungumza katika eneo la tukio Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Ayoub Mohammmed Mahamoud amewataka wamiliki wa majumba ya mji mkongwe zanzibar kutochanganya matumizi ya nyumba hizo ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea pindi majanga ya moto yanapotokea.

Amesema katika jengo hilo lenye maduka ya kawaida na makaazi ya watu, wafanyabiashara wameweka majokofu wanayoyatumia kuhifadhia samaki na vitoweo vyengine jambo lililochangia kutokea kwa moto huo.

Aidha amewashukuru wakaazi wa shehia hiyo kwa hatua za awali walizochukua kuudhibiti moto huo kabla ya kikosi cha Zimamoto na uokozi Zanzibar kufanikiwa kuuzima bila ya kuleta madhara kwa maisha ya waakaazi wa nyumba hiyo.

Akizungumzia tukio hilo mkuu wa kikosi cha zimamoto na uokozi wilaya ya Mjini SSF Suleiman Ahmada Suleiman ameleza chanzo cha moto huo ni kutomika bila kupumzishwa kwa majokofu hayo na kupelekea kutokea kwa hitilafu ya umeme.

SSF Suleiman amesema hali hiyo inasababisha uchakavu na kuwataka watumiaji wa vifaa vya umeme kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa hivyo.

Aidha amewatoa hofu wakaazi wa jengo hilo kuwa moto huo umedhibitiwa na kwamba eneo hilo lipo salama kwa matumizi huku akiwataka wananchi kutoa taarifa mapema katika kikosi chao ili kupunguza madhara ya moto au majanga mengine yanapotokea.

Nae sheha wa shehia ya Mkunazini Fuad Mohammed Hussein ameeleza kuwa jengo hilo la ghorofa mbili pamoja na maduka yaliyopo katika eneo la chini, linatumiwa kwa makaazi na wanafunzi wa chuo cha Sillas College waliopo katika mafunzo ya vitendo katika hoteli ya Marumaru iliyopo mjini Zanzibar.

Amesema awali alipewa taarifa ya kutokea kwa moto huo majira ya saa moja usiku na kuanza kutumia vifaa vya kuzimia moto walivyopatiwa na Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Mjini hivi karibuni ili kupunguza kasi ya moto huo pamoja na kutoa taarifa polisi na kikosi cha zimamoto na uokozi kwa msaada zaidi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi (ACP) Tobias Sedoyeka aliyefika katika eneo la tukio wakati shughuli za uzimaji zikiendelea aliwapongeza wananchi wa eneo hilo kwa ushirikiano waliouonesha na kuwapa pole watu walioathiriwa na moto huo.

akizungumza kwa niaba ya wenzake mmoja ya wanafunzi hao ambae hakutaka kutajwa jina amesema moto huo ulianzia katika eneo la chini la jengo hilo na kufanikiwa kutoa taarifa kwa watu waliokuwepo maeneo ya jirani na jengo hilo baada ya kuona moshi mkubwa.

"Mimi nilikuwa ndio narudi kutoka kazini ila wenzetu waliokuwepo walisema waliona moshi mwingi ukiingia vymbani huku watu wengine wakipiga kelele za moto ndipo walipotoka ili kupisha watu wa zimamoto lakini tunashukuru sote tupo salama", amesema.

Aidha amewahakikishia wananchi hao kuwa jeshi lake litaendelea kuweka ulinzi katika eneo ili kulinda wananchi hao na mali zao.

No comments:

Post a Comment