Na Mwinyimvua Nzukwi
WADAU wa sekta ya elimu na wananchi wa Zanzibar, wametakiwa
kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali ili kuimarisha elimu nchini kwa
kiwango kilicho bora.
Akizungumza baada ya kupokea kompyuta 96 aina ya laptop kutoka
kampuni ya ROM Solutions, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud,
amesema kufanya hivyo kutatanua wigo wa mafanikio katika sekta hiyo.
Amesema serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,
imekuwa ikitekeleza shughuli mbalimbali zikiwemo za ujenzi wa madarasa na
kuondoa michango kwa wanafunzi wa ngazi zote ili kuondoa changamoto
zinazoikabili sekta ya elimu ambazo huchangia kupatikana matokeo yasiyoridhisha.
Ameipongeza kampuni hiyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia
maendeleo ya Zanzibar kielimu na sekta nyengine, akisema zawadi hizo zitaongeza
hamasa ya wanafunzi na kuwawezesha kufanya vyema katika mitihani yao.
Amesema kompyuta hizo zitakazotolewa kwa wanafunzi wote waliofaulu
kwa kiwango cha daraja la kwanza kwenye mitihani ya kidato cha sita mwaka 2018
ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati alipokutana nao wakati
wakijiandaa kufanya mitihani hiyo mapema mwaka huu.
Aidha amewapongeza wanafunzi, walimu na wazazi kwa
kushirikiana na kamati ya maendeleo ya elimu ya mkoa, hatua aliyosema iliwezesha
kupatikana kwa matokeo mazuri ya mitihani hiyo.
Mapema, Mkurugenzi wa kampuni ya ROM Solutions Bi. Viorica
Enescu, aliwapongeza wanafunzi kwa matokeo hayo na kusema kampuni yake itaendelea
kushirikiana na serikali ya mkoa huo katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Alisema ufaulu huo wa kiwango cha juu unaihakikishia nchi kupata
wataalamu watakaosaidia kukuza uchumi na ustawi wa jamii.
Alitumia fursa hiyo kuwataka wanafunzi hao kuongeza bidii katika
masomo yao watakapokuwa vyuoni.
Akitoa taarifa katika mkutano huo, Katibu Tawala wa mkoa huo Hamida
Mussa Khamis, alisema mbali na zawadi hizo, ofisi ya mkuu wa mkoa ilichukua
hatua ya kudhamini kambi za wanafunzi hao pamoja na upatikanaji wa vitabu.
Alisema shughuli hizo zilidhaminiwa na taasisi ya Mimi na
Wewe, ambapo wanafunzi wa skuli zote za mkoa huo zilizokuwa na wanafunzi wa
kidatu cha sita zilihusika na mpango huo.
Alieleza kuwa, mpango huo ulisaidia kupatikana kwa ufaulu wa
daraja la kwanza kwa wanafunzi 96 na kupunguza idadi ya wanafunzi waliopata daraja
sifuri kutoka 96 hadi 15.
Zaidi ya shilingi milioni 115 zimetumika kununulia kompyuta
hizo zilizotolewa na kampuni ya ROM Solutions ambazo zitakabidhiwa kwa wanafunzi
hao ili ziwasaidie katika maandalizi ya elimu ya juu.
MAELEZO YA PICHA:
MKUU wa mkoa wa Mjini Magharibi ayoub mohammed Mahmoud (kushoto)
akipokea moja ya kompyuta mpakato (compyuta) 96 kutoka kwa mkurugenzi wa
kampuni ya ROM Solution Viorica Enescu (kulia). Kompyuta hizo zitakabidhiwa kwa
wanafunzi waliopata daraja la A wa skuli za mkoa wa Mjini Magharibi.
No comments:
Post a Comment