Saturday, July 28, 2018

TUMIENI FURSA KUENDELEZA MIRADI YENU - HAMIDA


NA MWINYIMVUA NZUKWI
Katibu Tawala wa Mkoa Mjini Magharibi  Hamida Mussa Khamis amewataka wajumbe wa shirikisho la vikundi vya ushirika na maendeleo vya mkoa huo kuwahimiza wananchi juu ya umuhimu wa uchimbaji na matumizi sahihi ya vyoo ili kuijiepusha na maradhi ya mripuko.
Akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa shirikisho hilo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa mjini magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud alisema wana vikundi hao wana wajibu wa kueneza elimu hiyo kwa wananchi wenzao wa shehia zilimo ndani ya mkoa huo.
“Umefika wakati kwa wananchi kujenga utamaduni wa kujenga vyoo na kuvitumia ili kuondokana na maradhi mbali mbali yanayosababishwa na uchafu yakiwemo ya kipindupindu”, alisema Katibu huyo.
Alieleza kuwa baadhi ya maeneo ya mkoa huo mazingira yake hayaridhishi kutokana na kukosa vyoo vya kisasa hivyo ni vyema wanachama wa shirikisho hilo wakawa mabalozi wazuri kwa wananchi waliowazunguka ndani ya wilaya za mkoa huo.
Aidha aliwaasa wanaushirika hao kuendelea kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya vikundi vyao ili viweze kuondokana na umasikini uliokithiri nchini unaochangiwa na ukosefu wa ajira.
“Kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo za ongezeko la watu, serekali haina uwezo wa kuwaajiri wananchi wote hivyo ni vyema mkajikusanya katika vikundi na kuanzisha miradi ya maendeleo ili  muweze kusaidiwa kupitia mfuko wa uwezeshaji ulioanzishwa na serikali kwa madhuimuni hayo”, alisema Hamida na kuahidi kuwa serikali ya mkoa huo itaendelea kuwasaidia ili wafikie malengo waliyojiwekea.
Akitoa maelezo kabla ya ufunguzi wa mafunzo hayo Mratibu wa Shirikisho la vikundi hivyo Sadfa Othman Kaswela ameeleza kuwa lengo la kuazishwa shirikisho hilo ni kuwasaidia wananchi kujikwamua kimaisha kupitia miradi ya maendeleo wanayoiendeha.
Alisema katika kukabiliana na umaskini wananchi wa maeneo mbali mbali ya mkoa huo wameanzisha vikundi vya ushirika kwa lengo la kukabiliana na changamoto za maisha hivyo shirikisho hilo linakusudia kuviunganisha vikundi hivyo ili kupata nguvu ya pamoja.
“Vikundi vyetu huwa vianakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo za uwezo mdogo wa kujiendeleza hivyo kupitia shirikisho hili tunaamini tutaweza kukabiliana na changamoto hizo na kuimarisha utekelezaji wa kazi zetu”, alieleza.
Nao baadhi ya viongozi wa shirikisho hilo kutoka katika wiliya za mkoa huo waliwahimiza wanawake wa mkoa wa Mjini Magharibi kujitokeza na kujiunga katika vikundi vya maendeleo ili kupata mafunzo yatakayowajengea uwezo wa kujitegemea na kuepukana na utengemezi katika jamii zao.
Walisema panmoja na idadi kubwa ya vikundi hivyo kuundwa na wananwake, bado kundi hilo la jamii linapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha ushirika kama njia mojawapo ya kupambana na umaskini wa kipato ndani ya familia zao.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa skuli ya sekondari ya Haile Selassie yaliandaliwa na shirikisho hilo kwa lengo la kujengeana uwezo ili kuvisaidia vikundi hivyo kuwa endelevu kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya jamii.

No comments:

Post a Comment