NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi amewakumbusha Mawaziri wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kukutana kwa
lengo la kubadilishana uzoefu wa kiutendaji ili kuimarisha jukumu la kuwahudumia
wananchi.
Alisema hatua hiyo
muhimu ambayo ilikuwa ikifanyika katika kipindi tofauti itaendelea kujenga
mapenzi zaidi, Umoja na Mshikamano baina ya Watumishi wa Serikali
zote mbili zilizopewa jukumu la kuwatumikia Watanzania wote.
Balozi Seif Ali Iddi
alitoa kumbusho hilo wakati akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki ukiongozwa na Naibu Waziri wake Dr. Suzan
Alphonce Kolimba ulipofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kwa mazungumzo ya
kubadilishana uzoefu.
Alisema Mikutano
vikao vya mara kwa mara vya mazungumzo vitakavyowajumuisha Mawaziri
wa Wizara zinazofanana za pande hizo mbili hasa pale zinapojichomoza hitilafu
ndogo ndogo katika pande mbili za Muungano husaidia kupunguza kero za Muungano.
“Vikao vya mara kwa
mara vya Mawaziri wa Wizara zinazofanana wale wa SMZ na SMT vina uwezo wa
kupunguza au kuondoa kabisa vile vikao vya Watendaji Wakuu wanaokutana kujadili
Kero zilizopo katika Muungano”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe huo wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki kwamba Wananchi wa Zanzibar na Tanzania
Bara Kihistoria ni wamoja kwa Karne kadhaa zilizopita kutokana na
maingiliano yao ya Mila, Kibiashara, Silka na Utamaduni.
Balozi Seif alieleza
kwamba udugu huo ndio uliopelekea Waasisi wa pande hizo mbili kufikia
makubaliano yaliyowezesha kurasimishwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
uliozaa Tanzania mnamo Tarehe 26 Aprili Mwaka 1964.
Akitoa Shukrani kwa
niaba ya Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Naibu Waziri wa Wizara hiyo Dr. Suzan Alphonce Kolimba
alisema kazi inayokabili Viongozi hasa Mawaziri Wapya ni kuendelea kupata
mawazo na fikra za watangulizi wao ili jukumu walilokabidhiwa na Taifa
walitekeleze kwa ufanisi uliotukuka.
Dr. Suzan alisema
licha ya Taaluma waliyokuwa nayo Viongozi wachanga lakini bado busara na hekima
za wale wazoefu zinapaswa kujumishwa pamoja katika utendaji wao kwa lengo la
kuwatumikia vyema Wananchi walio wengi Mjini na Vijijini Tanzania Bara na
Zanzibar kwa ujumla.
Viongozi hao wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wapo Zanzibar kwa
shughuli za Kikazi likiwemo suala la kuratibu masuala ya
Kimataifa yanayojumuisha Serikali zote mbili ile ya SMT na SMZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi (wa pili kushoto) akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioongozwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Dr.
Suzan Alphonce Kolimba (kushoto), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ramadhan
Muombwa (wa tatu kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar
Balozi Mohamed Haji Hamza.
No comments:
Post a Comment