NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
Zanzibar inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchezesha
michezo Minane ya Kitaifa au Kimataifa kwa siku katika kipindi
kifupi kijacho kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa uwanja wa Michezo
wa Mao Tse Tung uliopo Mperani Mtaa wa Kikwajuni Mjini Zanzibar unaotarajiwa
kuwa na hadhi ya Kimataifa.
Michezo hiyo itaweza
kuchezwa katika Viwanja vya Mao Tse Tung, Amani Stadium pamoja na ule wa
Gombani kisiwani Pemba ambapo michezo hiyo inaweza kuchezeshwa katika vipindi
viwili ndani ya siku moja.
Kauli hiyo imeyolewa
na Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Zanzibar Omar Hassan Omar { Omar King} wakati akimueleza Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefanya ziara fupi ya kuangalia maendeleo
ya ujenzi wa Ujwanja huo.
Omar Hassan alisema
Uwanja wa Mao Tse Tung pekee unaweza kuchezeshwa michezo Sita kwa
wakati Mmoja ikiwemo Miwili wa Mchezo Maafuru wa Soka jambo ambalo limeleta
faraja kwa Wizara, Serikali pamoja na wapenda michezo Nchini.
Alisema hatua za
ujenzi wa uwanja huo hivi sasa zimefikia asilimia 95% ambapo Wahandisi wa
Ujenzi huo kutoka Jamuhuri ya Watu wa China wanatarajiwa kukabidhi Uwanja huo
Mwezi Ujao wa Nane kwa Awamu ya kwanza wakati Awamu ya Pili watakamilisha
kukabidhi rasmi ifikapo Mwezi wa Oktoba Mwaka huu.
Katibu Mkuu huyo wa
Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Zanzibar
alimueleza Balozi Seif kwamba Uwanja huo pia una uwezo wa
kuongeza sehemu za Michezo ya Mpira wa Mikono na Vikapu iwapo
Uongozi wa Taasisi hiyo utahisi upo umuhimu wa kufanya hivyo hapo baadae.
Alieleza kuwa
Wahandisi wa ujenzi huo hivi sasa wanaendelea kukamilisha kazi ndogo ndogo
baada ya kumaliza uwekaji wa Nyasi Bandia katika viwanja vyote viwili wa mchezo
wa soka, Osifi, vyumba vya kubadilishia nguo vya wachezaji pamoja na vyoo 48
vilivyojengwa ndani ya uwanja huo.
Akitoa shukrani zake
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alisema Zanzibar inazidi kupaa kimichezo kutokana na
kuimarika kwa Miundombinu kwenye Sekta ya Michezo hasa Viwanja vya Soka.
Balozi Seif alisema
Serikali Kuu itazingatia mipango maalum itakayosaidia kuimarika kwa upatikanaji
wa vifaa vitavyotumiwa na Wanamichezo wa Michezo tofauti Nchini.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar alielezea masikitiko yake kutokana na kupotea kwa Mchezo wa
Magongo ambao uliiletea sifa kubwa Zanzibar Kimataifa kutokana na umahiri wa
wachezaji wake kipindi hicho.
Hata hivyo Balozi
Seif alionyesha matumaini yake ya kufufuka tena kwa mchezo huo unaochangia pia
ongezeko la Watalii Nchini kutokana na hatua kubwa zinazochukuliwa za
kuimarisha sekta ya Michezo Nchini.
Muonekano wa Uwanja wa Mao Dze Tung unavyoonekana ukiwa katika hatua za mwisho za kumalizika ujenzi wake unaofanywa na Wahandisi kutoka Jamuhuri ya Watu wa China.
Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Zanzibar Omar Hassan Omar ‘King’ (kulia) akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi hatua iliyofikia ya Ujenzi wa Uwanja wa Mao Dze Tung. Wa kwanza kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud.
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi (katikati) akiwa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud (kushoto yake) na Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Zanzibar Omar Hassan Omar ‘King’ (kulia yake) wakikagua baadhi ya sehemu kwenye Uwanja wa Michezo wa Mao Dze Tung unaotarajiwa kukabidhiwa serikalini hivi karibuni baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi wake.
No comments:
Post a Comment