Thursday, July 19, 2018

MAONESHO YA UTALII ZANZIBAR YAJA, KAMATI ZAZINDULIWA NA KUANZA KAZI RASMI


NA MWINYIMVUA NZUKWI
WAZIRI wa habari, utalii na mambo ya kale Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo amezindua kamati za maandalizi za maonesho ya utalii yanayotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Akizungumza katika uzinduzi wa maonesho hayo, Kombo alisema maonesho hayo yanatarajiwa kushirikisha zaidi ya mashirika na taasisi mbali mbali zinazojihusisha na sekta ya utalii 300 kutoka ndani na nje ya nchi ya Zanzibar.

Alisema maonesho hayo yatakayofanyika kwa mara ya kwanza yamelenga kuonesha na kutanua wigo wa fursa zinazopatikana katika sekta ya utalii na kukuza uchumi wa Zanzibar.

“Zamani kamisheni ya utalii na mashirika mengine yanayofanya kazi katika sekta ya utalii yalikuwa yakienda nje kuzionesha na kuzitangaza fursa za utalii ziliopo nchini ila kupitia maonesho haya tutaweza kukionesha kwa uhalisia wake na sio kupitiua picha”, alisema waziri Kombo.

Amewaeleza wajumbe hao kuwa wizara yake ina matumaini makubwa ya kufanikisha maonesho hayo ambayo pia yanatarajiwa kuongeza idadi ya watalii na ajira kwa watu mbali mbali waktakaohusika na maonesho hayo kama ilivyo katika maonesho mengine yanayofanyika nchini.

Aliwataja wajumbe wanaounda Kamati kuu ya maonesho hayo kuwa ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya utalii Zanzibar Dk. Vuai Iddi Lila (Mwenyekiti), Mkurugenzi wa kampuni ya ‘Zanzi Promotions’ Javed Jafferji (Makamo Mwenyekiti), Makamo Mwenyekiti wa Jumuiya ya taasisi za utalii Zanzibar - ZATI Julia Bishop anaekuwa Katibu wa kamati hiyo.

Wajumbe katika kamati hiyo ni pamoja na mwenyekiti wa jumuiya ya watembezaji watalii Zanzibar - ZATO Hassan Ali Mzee, meneja mkuu wa hoteli ya Park Hyatt Nicolas Chedro, Mkurugenzi wa uwekezaji katika mamlaka ya ukuzaji wa vitega uchumi Zanzibar – ZIPA Sharif Ali Sharif, naibu mkurugenzi wa iadara ya habari maelezo Dk. Juma Mohammed Salum na Mohamed Mbwana Mkadara kutoka mamlaka ya maonesho ya biashara ya Tanzania – TANTRADE.

Pia katika uzinduzi huo waziri kombo alizindua Kamati ya ufundi ya maonesho hayo inayoundwa na mwenyekiti wa kamisheni ya utalii Zanzibar sabah saleh ali anaekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Meneja uendeshaji wa Kampuni ya ‘Zanzi Promotions’ adnan abass na wajumbe Sabra Juma Nassor kutoka ‘Zanzi Promotions’, Donna Da Silva kutoka ‘Zanzi Promotions’ na Meneja Msaidizi wa hoteli ya Verde Anwar Alex Fernandies.

Katika hatua nyengine waziri Kombo alizinduwa Kamati ya maamuzi ambayo itaamua juu ya washiriki watakaopatiwa zawadi zilizoandaliwa katika maonesho hayo   ambayo itaongozwa na Sabah Saleh Ali, Julia Bishop anaekuwa Makamu Mwenyekiti, Katibu wa jopo hilo Dk. Miraji Ukuti Ussi na wajumbe Ahmed Makame Haji, Andrea Boero, Nicolas Konig, Yves Montel na Omar Mmadi Mwarabu.

Maonesho ya utalii yanatarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 17 – 20 mwaka huu ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinzudi Dk. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi na usiku wa utoaji wa zawadi kwa washindi wa maonesho hayo.


No comments:

Post a Comment