Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema
Zanzibar na Oman zitaendelea kufanya kazi pamoja katika lengo la kudumisha uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kwa maslahi na maendeleo
ya wananchi wa nchi mbili hizo.
Alisema Ushirikiano huo
umeimarika zaidi kwa Zanzibar kupokea ufadhili wa Vijana wake wanaopata
fursa za kujiunga na Masomo ya juu Nchini Oman katika fani mbali mbali za
mafunzo ikiwemo Udaktari, Uhandisi, Kompyuta pamoja na Lugha.
Balozi Seif Ali Iddi alisema
hayo wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania Bwana Ali
Abdulla – Al Mahrouq aliyefika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar
kujitambulisha rasmi akiambatana pia na Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar
Dr. Ahmed Hamood Al - Habsi.
Alisema Zanzibar inafurahia
kuendelea kuwepo kwa uhusiano huo wa kipekee na wa kupigiwa mfano ambao umekuwa
ukileta faraja na matunda mazuri yanayotowa fursa zaidi kwa Zanzibar kutanua
wigo wa Kimaendeleo na kuongeza maeneo mengine ya ushirikiano wa Kisiasa,
Kiuchumi na Kiutamaduni.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alimueleza Balozi Ali Abdulla – Al
Mahrouq kwamba uungaji mkono wa Oman kwa Zanzibar hasa
katika utanuzi wa Chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni umeleta faraja kwa Wananchi
walio wengi kwenye huduma za Afya zinazotarajiwa kuenea katika masafa
yasiyozidi Kilomita Tano.
Balozi Seif aliipongeza Serikali
ya Oman kwa msaada wake mkubwa inayoendelea kutoa kwa Zanzibar hasa
kwa kukubali kugharamia matengenezo makubwa ya Majengo ya Kihistoria ya Beit el
ajab na Jumba la Makumbusho ya Kifalme yaliyopo Forodhani Mjini Zanzibar.
Alisema msaada huo wa Majengo
hayo muhimu umekuja wakati muwafaka kwa vile utasaidia kuhifadhi Historia ya
Kiutamaduni na Kiutawala ya Visiwa vya Zanzibar inayohusisha pia
mafungamano ya Majengo hayo na Oman.
Akigusia ujio wa Meli ya
Kifalme ya Fulk Al Salamah kutoka Nchini Oman Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif alieleza wazi kwamba Zanzibar imepata
faraja kubwa ya ziara ya Ujumbe wa Serikali ya Oman uliowasili
Zanzibar na Meli hiyo ya Kifahari.
Alisema Wananchi wa
Zanzibar wamepata kujifunza mambo mbali mbali kufuatia ujio wa Meli hiyo kwa
kupata taaluma ya kuepuka masuala mazima yanayotokana na Sekta ya mafuta ambayo
kwa sasa Visiwa vya Zanzibar vimo katika matayarisho ya awali ya kuendesha
Miradi inayotokana na Sekta hiyo.
Akigusia suala la Majanga Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameishukuru Serikali ya Oman
kwa msaada wake wa kuwawezesha Viongozi Wanne Waandamizi wa Zanzibar kupata
fursa ya kujifunza mbinu na Taaluma ya jinsi ya kujikinga na
Majanga.
Balozi Seif alisema mafunzo
hayo yameleta faida kubwa kiasi kwamba Oman ingefikiria tena kutoa nafasi
nyengine kama hizo kwa watendaji wengine wa Taasisi za Majanga
Zanzibar kupata fursa kama hizo katika kipindi chengine kijacho.
Mapema Balozi Mpya wa Oman
Nchini Tanzania Bwana Ali Abdulla – Al Mahrouq alisema
udugu uliopo wa Viongozi pamoja na hata Wananchi wa kawaida wa Oman
na Zanzibar ni vyema ukaongezeka zaidi katika uhusiano wa masuala ya
Kibiashara.
Balozi Al –
Mahrouq alisema pande hizo mbili zimekuwa na historia ndefu ya Kiutamaduni
na Kisiasa kiasi kwamba kwa sasa nguvu zikaongezwa katika uimarishaji zaidi wa
Kibiashara jambo ambalo linaweza kustawisha kuongeza ukaribu wa
Wananchi wa pande hizo mbili unaoweza kudumu milele.
Balozi huyo wa Oman Nchini
Tanzania alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Serikali ya Oman
itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha harakati za Maendeleo na
Ustawi wa Jamii wa Wananchi wa Zanzibar unazidi kukua.
Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania Bwana Ali Abdulla – Al Mahrouq (kushoto) akijitambulisha rasmi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (katikati) alipofika katika Ofisi za Makamu huyo wa Vuga Mjini Zanzibar. Wengine ni Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Hamood Al – Habsi (wa kwanza kulia) na Naibu Waziri Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mihayo Juma Nhunga.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (kulia) akimkabidhi zawadi ya Mlango wa Zanzibar (Zanzibar door) Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania Bwana Ali Abdulla Al-Mahrouq kama ishara ya kufungulia Milango ya uwepo wake nchini.
.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (kulia) akiagana na Balozi Mpya wa Oman Nchini Tanzania Bwana Ali Abdulla Al - Mahrouq (kushoto) mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ofisi za balozi Seif Vuga Zanzibar. (Picha na OMPR).
No comments:
Post a Comment