Na Mwinyimvua Nzukwi
WASAIDIZI wa sheria – ‘Paralegal’ wa wilaya za
Magharibi ‘A’ na Kaskazini ‘B’ Unguja wametakiwa kufanya kazi zao kwa kufuata
miongozo wanayopatiwa na weledi ili kuongeza tija kwa jamii.
Mwenyekiti wa Umoja wa Watu Wenye ulemavu Zanzibar
(UWZ) Salma Saadat alitoa rai hiyo alipokuwa akifunga mafunzo ya siku 3 ya
kuwajengea uwezo Paralegal wa Unit za wilaya ya Magharibi A na Kaskazini B
Unguja.
Alisema kufanya
hivyo kutasaidia kufikiwa kwa malengo ya kueneza elimu ya sheria na huduma za
kisheria kwa wananchi wengi wa wilaya hizo.
Alisema iwapo elimu na huduma za kisheria
zitapatikana kwa uhakika na wakati stahiki miongoni mwa jamii, kuna uwezekano
mkubwa wa kupungua kwa migogoro ya kisheria na kijamii nchini.
Alisema katika jamii ya Zanzibar kuna migogoro ya
kisheria ambayo inaweza kutatuliwa au kufikia hukumu nzuri iwapo wahusika
wangepatiwa usauri wa kisheria katika hatua za awali kabla ya mashauri hayo
kufikishwa katika vyombo hivyo.
"Siku zote mnapaswa kutambua kuwa jamii yetu
inakabiliwa na mahitaji makubwa ya elimu na huduma za kisheria, hivyo ni vyema
mkafanye kazi hizo kwa jamii yetu kwa kutumia ujuzi mliopatiwa kwa moyo wa
kujitolea, uwajibikaji, uwazi na ushirikiano wa hali ya juu ili kupunguza muda
mwingi unaotumika na watu wetu kufuatilia masdhauri yao katika vyombo vya
sheria", alieleza Mwenyekiti huyo.
Aidha aliwataka wasaidizi hao kutumia mafunzo hayo
kwa lengo la kuziimarisha taasisi zao ili ziweze kujitegemea baada ya
kukamilika kwa mradi uliolenga kuiwezesha jamii ya Zanzibar kuwa na uelewa
mkubwa wa sheria na kupatiwa msaada wa huduma za sheria unaosimamiwa na UWZ
chini ya ufadhili wa shirika la Legal Services Facilities - LSF la Tanzania
bara.
“licha ya mradi huu kulenga katika kuongeza idadi ya
wananchi wanaopatiwa huduma na elimu za sheria katika shehia zenu, pia ipo haja
ya kuutumia kujijengea uwezo ili muweze kuendelea na kazi hiyo hata baada ya
mradi kumaliza muda wake kwa manufaa ya jamii yetu”, alisema Salma.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa UWZ Asya Abdulsalam
alieleza kuwa katika tathmini ya awali ya utekelezaji wa mradi huo, taasisi
wanazosimamia zimeonesha muelekeo mzuri licha ya kutofikiwa kwa malengo ya
wananchi waliotarajiwa kufikiwa katika robo ya kwanza ya utekelezaji wa mradi
huo iliyoanza mwezi Julai mwaka huu.
“Kwa ujumla robo ya kwanza baadhi ya ‘units’
zimeonesha mwelekeo mzuri wa kulifikia lengo la mradi japo kuna changamoto
mbali mbali ikiwemo ya idadi ndogo ya wateja mliowafikia”, alieleza Mkurugenzi
huyo.
Aliongeza kuwa kila ‘Unit’ imewekewa lengo la
kuhakikisha asilimia 35 ya wakaazi wa wilaya husika inapatiwa elimu ya sheria
na asilimia 30 ya wakaazi hao wanapatiwa huduma za sheria ifikapo mwisho wa
mradi hivyo wasaidizi hao wanapaswa kuwa na mikakati imara ya kuyafikia malengo
hayo.
Aidha alieleza umuhimu wa ‘units’ hizo kuzitumia
kamati za ushauri za wilaya (TAGP) zinazoongozwa na wakuu wa wilaya na kamati
za ushauri za viongozi wa kijamii (CAT) zinazowajumuisha masheha ili
kurahisisha utendaji kazi wa wasaidizi hao.
Katibu Mkuu wa ‘unit’ ya wasaidizi wa sheria wa
wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja (NBPU) mwalimu Ali Salim Ali alieleza kuwa
katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita walifanikiwa kuwafikia jumla ya watu
487 kinyume na lengo lililowekwa la kuwafikia watu 1,787 katika kipindi hicho.
“Tulijitahidi kuitisha mikutano katika shehia mbali mbali
kupitia wasaidizi wa sheria wetu, lakini mara nyingi tulipata idadi ndogo
kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo za harakati za maisha na mwamko mdogo
wa jamii katika maswala ya sheria katika maeneo mengi ya wilya zetu”, alieleza
mwalimu Ali.
Nae Katibu Msaidizi wa ‘unit’ ya wasaidizi wa sheria
wa wilaya ya Magharibi ‘A’, Makame Mwadini alieleza kuwa mafunzo hayo
yatasaidia kuimarisha utekelezaji wa kazi zao na kuahidi kuyafanyia kazi
mapungufu yote yaliyoonekana katika tathmini hiyo.
“Kikubwa tulichojifunza ni kwamba tulikuwa tunafanya
kazi bila ya kujiwekea malengo, hivyo tutajitahidi kuyafanyia kazi mapungufu
yaliyoainishwa ili tuwe na matokeo mazuri jambo ambalo ndio madhumuni ya
kuanzisha jumuiya yetu”, alisema mwadini na kuwashukuru wadau wote kwa usaidizi
waliowapatia.
Mafunzo hayo yaliyolenga kutoa tathmini na
kurekebisha makosa yaliyogundulika katika utekelezaji wa mradi huo
unaotekelezwa katika maeneo yanayosimamiwa na umoja huo ambazo ni wilaya za
Kaskazini Unguja ‘A’, Kaskazini ‘B’, Mjini na Magharibi ‘A’ Unguja ili kuleta
ufanisi kwa jamii.
MWISHO.
PICHANI: Katibu Mkuu wa Unit ya Wasaidizi wa sheria (Paralegal) ya wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja Omar Khamis (kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Umoja wa watu wenye ulemavu Zanzibar (UWZ) Salma Saadat (hayupo pichani) alipokuwa akifunga mafunzo kwa Paralegal hao yaliyotolewa na UWZ kwa ufadhili wa Legal Services Facility - LSF.
No comments:
Post a Comment