Na Is-haka Omar,.
KAIMU Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM
Zanzibar, Abdulghafar Idrissa Juma amewataka viongozi wa Baraza kuu la UVCCM
Wilaya ya Mfenesi kuwa sehemu muhimu ya kuwaunganisha vijana na sio kuwagawa
katika makundi yatakayoweza kuleta migogoro ndani ya Umoja huo.
Rai hiyo ameitoa leo wakati akifungua
Kikao cha kwanza cha Baraza hilo tangu kumalizika kwa Uchaguzi wa ngazi ya
Wilaya hiyo kilichofanyika katika Ofisi za UVCCM Mfenesini zilizopo
Bububu Unguja.
Alisema wajumbe wa Baraza hilo
wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kushughulikia matatizo yanayotokea kwa Vijana
ili waendelee kuishi katika misingi ya malezi bora ya Chama cha Mapinduzi.
“Viongozi mliochaguliwa kupitia
Uchaguzi wa Umoja wetu msipofanya vizuri mtakuwa mmeharibu mfumo wa maisha yenu
ya kisiasa, lakini mkifanya vizuri itakuwa ni njia ya kupata fursa mbali mbali
za kiungozi na kiutendaji ndani ya Chama na Jumuiya ”, alisema
Abdulghafar.
Aliwambia kuwa matarajio ya UVCCM ni
kuona Baraza hilo linakuwa ni shamba darasa la kuwapata viongozi imara wenye uwezo
wa kujenga hoja zenye nguvu ya kuleta mabadiliko ya kimaendeleo nchini.
Abdulighafar alisisitiza kuwa wajibu
wa kila kiongozi ndani ya umoja huo ni kuongoza vizuri sambamba na kuzisoma kwa
kina kanuni ya UVCCM na Katiba ya CCM ili maamuzi yoyote yatakayofanyika yaweze
kuzingatia matakwa ya Kikatiba.
Aidha Kaimu Katibu Mkuu huyo,
Abdulghafar umefika wakati wa kuwa na UVCCM huru yenye nguvu kiuchumi na
kiutendaji hivyo viongozi wa umoja huo wanatakiwa kubuni miradi endelevu
itakayosaidia vijana kujiajiri wenyewe.
“Vijana tutakapokuwa na uhakika wa
kipato kupitia miradi tunayoisimamia wenyewe basi hata hao baadhi ya wanasiasa
wenye fedha waliozoea kututumia kwa maslahi yao watakuwa hawana nafasi hiyo
tena bali tutasimama wenyewe kutetea maslahi ya chama na jumuiya kwa ujumla.”,
alieleza Kaimu Katibu Mkuu huyo.
Mapema Katibu wa Hamasa na
Chipukizi wa Wilaya hiyo aliyemaliza muda wake, Mussa Khamis Mzee
alijiuzulu wadhifa wake ili kupisha kikao hicho kutekeleza utaratibu wa
kikanuni wa kumdhibitisha Katibu atakayeshika nafasi hiyo kwa miaka mitano
ijayo.
MAELEZO YA PICHA:
Picha
no.9- Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Abdulghafar Idrissa Juma akifungua
Kikao cha Baraza Kuu la UVCCM Wilaya ya Mfenesini Unguja.
Picha
no.11 na 14 Baadhi ya Wajumbe walioudhuria kikao hicho kilichofanyika
katika Ofisi za UVCCM Wilaya ya Mfenesini zilizopo Bububu Unguja.
No comments:
Post a Comment