Na Mwinyimvua
Nzukwi
MKUU wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka
Masheha wa Mkoa huo kuzingatia katiba, sheria, sera, kanuni na miongozo mbali
mbali ya nchi katika utekelezaji wa wajukumu yao ili kuwahudumia wananchi kwa
ufanisi.
Akifungua mafunzo elekekezi ya siku mbili kwa masheha wa hao
kuhusu dhana ya ugatuzi wa madaraka kutoka serikali kuu kwenda serikali za
mitaa yaliyofanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la wawakilishi Kikwajuni mjini
Zanzibar.
Alisema masheha kama watendaji wa awali wa serikali kuu, wana
wajibu wa kisheria wa kuhakikisha wanasimamia mipango ya maendeleo na utowaji
wa huduma bora kwa wananchi bila ya kujali itikadi zao kisiasa, dini, kabila na
rangi kwa maslahi ya shehia zao na taifa kwa ujumla.
Mahmoud alieleza kuwa kupitia mpango wa ugatuzi, masheha wana
nafasi ya kuratibu mipango itakayoandaliwa katika ngazi za serikali za mitaa, wilaya
na Mkoa, hivyo wanatakiwa kutumia mafunzo hayo kuimarisha utendaji na kuhakikisha
mpango huo unafanikiwa.
Akitoa maelezo katika mafunzo hayo Mkurugenzi wa Tawala za
Mikoa na Serikali za mitaa kutoka katika wizara ya nchi ofisi ya rais, tawala
za mikoa, serikali za mitaa na idara maalum za serikali ya mapiduzi ya Zanzibar
Khalid Abdallah Omari alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo masheha kuhusu wajibu na maadili ya
kiongozi wa umma.
Aidha alisema mafunzo hayo yamelenga kukumbushana wajibu wa
utekelezaji wa majukumu yao watendaji hao ili kuepusha mgongano na muingiliano
wa majukumu kati ya serikali kuu na serikali za mitaa.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja Marina Joel Thomas aliwataka
masheha hao kuwashajihisha wananchi katika maeneo yao kushiriki katika uuandaji
na utekelezaji wa wa miradi mbali mbali ya maendeleo ili kustawisha upatikanaji
wa huduma mbali mbali za kijamii.
Mafunzo hayo ya masheha yaliyoandaliwa na wizara ya nchi
ofisi ya Rais tawala za Mikoa Serikali za mitaa na idara maalum ni muendelezo
wa mafunzo yanayotolewa kwa watendaji wa ngazi mbali mbali za uongozi na
utawala ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa mpango wa ugatuzi ulioanza
kutekelezwa rasmi katika sekta ya elimu ya awali na msingi, afya na kilimo
mnamo mwezi julai mwaka huu.
Katika mafunzo hayo viongozi hao walifundishwa mambo mbali
mbali ikiwemo wajibu wa masheha kwa mujibu wa sheria ya Tawala za Mikoa namba 8
ya mwaka 2014 , muelekeo wa mkakati wa upelekaji wa madaraka kwa wananchi, umuhimu
wa kuweka kumbukumbu, kanuni za usuluhishi wa migogoro katika ngazi za shehia
na sheria za usimamizi wa masuala ya ardhi.
Mkuu wa wilaya ya Mjini Marina Joel Thomas (kushoto)
akimuongoza Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud (kulia)
kuondoka katika ukumbi wa zamani wa baraza la wawakilishi baada ya kufungua mafunzo ya
masheha kuhusu ugatuzi wa madaraka kutoka serikali kuu kwenda serikali za
mitaa. Nyuma ya Mahmoud ni mkuu wa wilaya ya Magharibi ‘A’ Capt. Khatib Khamis
Mwadini.
MKUU wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahamoud akitoa hutuba ya ufunguzi wa mafunzo kwa masheha wa shehia za mkoa huo kuhusiana na dhana ya ugatuzi wa madaraka kutoka serikali kuu kwenda katika serikali za mitaa. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mjini Marina Joel Thomas
No comments:
Post a Comment