Saturday, November 18, 2017

UJENZI WA JENGO LA ABIRIA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA ZANZIBAR KUENDELEA MWEZI UJAO

Na Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
UJENZI wa jengo jipya la abiria  katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar unatarajiwa kuendelea mwezi ujao baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati ya serikali ya Zanzibar na serikali ya China ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za usafiri wa anga  kwa abiria  wanaotumia  uwanja huo.
Akitoa taarifa ya serikali kwa Waandishi wa Habari mjini Unguja, Waziri wa Fedha na Mipango zsanzibar Dk. Khalid Salum Mohammed amesema ujenzi huo ambao ulisisima kwa muda mrefu, unatarajiwa kuendelea kuanzia katikati ya mwezi Disemba kufuatia serikali ya watu wa china kutoa dhamana ya mkopo wa ziada kwa serikali ya Zanzibar kugharamia ujenzi huo kutoka katika benki ya Benki ya Exim ya China.
Alisema kusimama kwa mradi ambao ni miongoni mwa miradi ya uimarishaji wa uwanja huo, ulitoakana na kubadilika kwa muundo wa ujenzi wa jengo hilo uliozingatia mahitaji mapya ya shirika la usafiri wa anga dulinani (ICAO) hali iliyopelekea kuongezeka kwa gharama za ujenzi zilizopangwa awali.
Alisema awali mradi huo ulipangwa kutumia dola milioni 70.4 za marekani ambazo ni mkopo wa masharti nafuu ambazo ziliongezeka na kufikia dola million 128.7 ambazo serikali ya Cina ilishauri zitafutwe mahali pengine na kupelekea kusimama kwa ujenzi huo uliohusisha ujenzi wa jengo hilo, upanuzi wa eneo la maegesho kwa zaidi ya mita za mraba 38,000 na maegesho ya magari ya watumiaji wa uwanja huo.
“Tatizo kubwa lililojitokeza ni upatikanaji wa huizo fedha za ziada, lakini baada ya mashauriano ya muda mrefu kati ya SMZ (Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar), SMT (Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na serikali ya jamhuri ya watu wa china yaliyochukua muda mrefu hatimae benki ya exim imekubali kudhamini mkopo wote wa kugharamia ujenzi huo kwa taratibu za mkopo wa masharti nafuu badala ya masharti ya kibiashara kama ilivyopendekeza awali”, alieleza Dk. Khalid na kuwashukuru wadau wote waliofanikisha kutatua changamoto hizo.
Alisema serikali imepigania kutatua changamoto zilizojitokeza kwa kuamini kuwa kukamilika kwa ujenzi huo utapelekea kuimarika kwa  huduma za kusafirisha abiria na mizigo sanjari na kuzihudumia ndege zitakazotua uwanjani hapo kwa kuzingatia viango vya kimataifa.
“Katika miradi iliyotangulia, tuliimarisha huduma za kiusalama kwa kununua magari mapya ya zimamoto pamoja na kuweka vifaa vya ulinzi na usalama  ili kuimarisha  hali ya usalama katika  eneo hilo  hususani watalii  ambao wana mchango muhimu  katika uchumi wa Zanzibar”, alisisitiza wazir Khalid.
Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Balozi Ali Abeid Karume alisema Wizara yake itahakikisha inasimamia kikamilifu ujenzi huo ili uweze kumalizika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa kwa lengo la kukuza uchumi wa Zanzibar.
Alisema ili kufanikisha hilo imeanza mawasiliano na wizara nyengine ili kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa rasimilali za ujenzi na kwamba wameshapatiwa maeneo yatakayotumika kwa ajili ya upatikanaji wa mchanga na kifusi ili kuharakisha ujenzi huo.
“Kwa mujibu wa makubaliano mapya, wizara yangu ndiyo itakuwa mwajiri katika mradi huu na tumeshajipanga kuona ni kwa namna gani mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa kwa kuweka wasimamizi wa kazi mbali ya mshauri elekezi, hivyo hakuna kazi itakayotekelezwa na mkandasi au kukubaliwa kabla na sisi kujiridhisha”, alieleza balozi karume.
Aidha alieleza kuwa uwanja huo utakapokamilika unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia abiria  million 1.6 kwa mwaka na  kukabiliana kwa kiasi kikubwa na tatizo la kuchelewa kuhudumiwa kwa abiria wanaowasili au kuondoka kutokana na jengo linalotumika sasa kuwa na uwezo wa kuhudumia watu laki 5 kwa mwaka.
Akifafanua baadhi ya hoja za waandishi, katibu mkuu wa wizara ya fedha na mipango Zanzibar khamis mussa khamis alisema kuendelea kwa ujenzi huo kutapelekea uwanja huo kuweza kupokea ndege za aina zote isipokuwa air bus 3 na kwamba hadi sasa mkandarasi kampuni ya Beijing Construction & Engineering Group ameshalipwa kiasi cha dola 35.2 milioni kwa kazi alizofanya awali.
“Sisi (serikali ya Zanzibar) tulisita kukubali kuingia katika mkopo wenye masharti ya kibishara kwa kujua kuwa usingekuwa na nafuu kama huu ambao ndani yake una ruzuku lakini pia una riba ya asilimia 2 lakini pia una muda mrefu wa malipo ambao ni miaka 25 baada ya kumalizika kwa kipindi cha kujizuia kulipa ambacho kinadhaminiwa na serikali ya china”, alifafanua Katibu Mkuu huyo.

Mradi huo unatarajiwa  kugharimu  Jumla ya Dola za marekani Million 128 utakamilika baada ya kipindi cha miezi 18 kuanzia mwezi ujao, unatarajiwa kuanza majaribio ya awali mnamo mwezi agosti 2019 kabla ya kukabidhiwa rasmi serikalini mwezi disemba mwaka huo.
Waziri wa fedha na Mipanzo Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohamed

No comments:

Post a Comment