Tuesday, November 14, 2017

RC MAHMOUD AHITIMISHA ZIARA YAKE KWA KUHIMIZA UWAJIBIKAJI

Na Mwinyimvua Nzukwi
WATENDEJI na viongozi wa Mkoa wa Kaskazini wametakiwa kubadilika na kutumia falsafa za ‘hapa kazi tu’ na ‘kutofanya kazi kwa mazowea’ ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma za jamii mkoani humo.

Akizungumza na wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama, watendaji wa serikali za wilaya, mkoa na halmashauri za wilaya za mkoa huo baada ya ziara yake ya  siku 5 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mahmoud Mohammed alisema ipo haja kwa watendaji hao kutumia ziara hiyo kutathmini utendaji wao na mahitaji ya wananchi wa mkoa huo.

Alisema ili kuongeza imani ya wananchi kwao, hawana budi kuzingatia muda, wajibu na majukumu yao kwa umma ili kupunguza malalamiko ya jamii jamboa alilisema litaongeza imani ya wananchi kwa serikali yao.

Alisema katika ziara hiyo amegundua kuwa kero nyingi zilizokuwa zikitolewa na wananchi dhidi ya serikali na sekta binafsi mkoani humo ni matokeo ya upungufu wa uwajibikaji jambo ambalo lilipunguza imani ya wananchi kutumia huduma zinazotolewa na taasisi hizo kiasi cha kuibua kwa malalamiko miongoni mwa wananchi.

Alisema wananchi wengi waliopata nafasi ya kueleza kero zao walionesha kutoridhishwa na huduma zinazotolewa na watendajiwa serikali za wuilaya, halmashauri na shehia  hivyo kwa pamoja wamekubaliana kubadilika na kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na kujituma.

“Ninawaomba tubadilike, kwani wananchi walio wengi na kwa muda mrefu walikosa imani na sisi (serikali) kwa kudhani kuwa hata wakija hatutoweza kuwahudumia ima kwa tofauti zao za kimaeneo au kikanda au kisiasa au kidini jambo ambalo sio dhamira ya serikali zote mbili ambazo zipo kwa ajili ya mkoa ni kuwahudumia wananchi”, alisema RC Ayoub.

Aidha aliawakata kuwa na ujasiri wa kuamua na kutekeleza wajibu waonda watasaidia kuongeza kasi ya maendeleo na kupunguza kiwango cha umaskini wa wananchi wa mkoa huo.

Kabla ya kikao hicho, Mkuu huyo wa Mkoa alikutana na na kamati za ulinzi na usalama za Wilaya na mkoa huo na kukubaliana kuundwa kwa kamati maalum ya kufuatilia maagizo na maelekezo yaliyotolewa wakati wa ziara ambayo yalielekezwa katika maeneo mbali mbali ya kiutendaji.

Baadhi ya maeneo hayo  ni pamoja na kuendelezwa kwa vita dhidi ya dawa za kulevya katika maeneo yote ya mkoa huo, kushughulikiwa kikamilifu kwa migogoro ya ardhi, kufuatiliwa na kuwekewa mkakati wa ajira za wakaazi wa maeneo ya jirani na hoteli za kitalii, udhalilisha wa kijinsia na kudhibitiwa kwa watembeza watalii wasio rasmi katika fukwe za mkoa huo.

Mambo hayo ni miongoni mwa kero zilizotolewa na wananchi wa maeneo mbali mbali ya mkoa huo katika mikutano 11 ya hadhara iliyofanyika katika shehia za Bumbwini Makoba, Mahonda, Nungwi, Kivunge, Kiwengwa, Kinyasini, Upenja, Donge Pwani, Matemwe na Tumbatu uvuvini ambayo ilijumuisha wananchi wa shehia nyengine za jirani nazo.

Ziara ya RC Ayoub ilianza Novemba 7 mwaka huu katika shehia ya Bumbwini Makoba wilaya ya Kaskazini ‘B’ na kuhitimishwa katika shehia ya Tumbatu Uvuvini  wilaya ndogo ya Tumbatu Novemba 12 mwaka huu ambapo wananchi zaidi ya 100 walipata nafasi ya kueleza kero na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao zilizohusiana na utendaji wa serikali na sekta binafsi na kupatiwa ufumbuzi wa papo kwa papo na mengine kuelekezwa taasisi husiuka kuzishughulikia.

MAELEZO YA PICHA: Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mahmod Mohammed (katikati) akisisitiza jambo katika mkutano wa majumuisho baada ya ziara yake ya siku 5 mkoani humo. kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja.

No comments:

Post a Comment