Saturday, November 18, 2017

UJUZI MDOGO KATIKA BIASHARA KIKWAZO KWA WAJASIARIAMALI TANZANIA

Na Mwinyimvua Nzukwi
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Tanzania ina idadi kubwa ya Wajasiriamali lakini ni kidogo kati yao ndio wenye ujuzi wa usimamizi wa biashara, taarifa na maarifa  yanayohitajika  kukuza biashara zao.
Alisema hali hiyo hupelekea biashara nyingi kufa kutokana na kushindwa kuendana na mahitaji halisi ya kisekta na kushindwa kuhimili ushindani wa soko.
Balozi Seif alieleza hayo wakati akifungua Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa vijana wajasiriamali yaliyoandaliwa na taasisi ya Fursa Tanzania katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakishi  Kikwajuni Mjini Unguja.
Alisema Serikali ipo tayari kushirikiana na waandaaji wa semina hiyo ili kutengeneza na kutekeleza mikakati itakayojenga mazingira bora na wezeshi kibiashara itakayoweka miundombinu itakayosaidia maendeleo ya wajasiriamali na vijana nchini.
Alisema Tanzania inatekeleza sera ya uchumi wa viwanda azma ambayo katika kufikia hilo, kundi la wajasiriamali lazima lizalishwe kwa wingi ili kuanzisha, kukuza na kuendeleza viwanda hivyo na kutengeneza ajira, kuchochea uvumbuzi na kuhamasisha ushindani wa soko.
 “Fursa imekuwa ikizunguka nchi nzima ili kuzungumza na vijana kuwaonesha namna wanavyoweza kujiendeleza na kuendeleza shughuli zao. Hili ni jambo zuri hasa wakati huu tunapozungumzia uchumi wa viwanda na kuelekea katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025”, alisema balozi Seif.
Mapema Muanzilishi wa Taasisi hiyo ambae pia ni msimamizi wa programu ya mafunzo ya iliyolenga kuwakomboa Vijana na Maisha duni Ruge Mutahaba alisema  kuna haja kwa wajasiriamali nchini kubuni maradi au biashara kwa kuzingatia mahitaji ya jamii yake na fursa zinazomzunguka ili kuongeza thamani na kipato cha bidhaa anazozalisha.
Ruge alieleza kuwa wakati umefika kwa jamii kuondokana na mawazo yanayoviza upeo wa ufikiri na kuelewa ku wa mabadiliko yanaanza na mtu binafsi kwa kuzingatia mahitaji yake na mahitaji ya ndani ya jamii.
“Vijana mnaomaliza masomo na wale mlioko vyuoni ni lazima mjuwe kuwa kutokana na ufinyu wa fursa za ajira kitaifa na kimataifa mnalazimika kujitengenezea ajira nyinyi wenyewe zitakazowaongoza kuendesha maisha yenu kwa amani na furaha hapo baadae”, alisema Ruge ambae pia ni mkurugenzi wa Clouds Media Group.
Akitoa salamu za mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) yanayofanyakazi nchini Tanzania, Mratibu Mkaazi wa umoja huo Alvaro Rodriguez alisema Umoja wa Mataifa kupitia taasisi na mashirika yake utaendelea kutoa taaluma kwa makundi mbali mbali ya jamii wakiwemo wanawake kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujiendesha Kimaisha.
Alisema hakuna taifa lolote ulimwenguni linaloweza kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi bila ya mchango wanawake huvyo ilizitaka serikali za Tanzania kuendelea kutoa msukumo kwa kundi hilo kujiendeleza kiuchumi sambamba na kujengewa mazingira mazuri ya kufikia malengo yao.
“Mashirika ya Umoja wa Mataifa yataendelea kushirikiana na taasisi ya Fursa Tanzania ili kusaidia kupunguza au kuondosha changamoto zinazowakabili vijana na wanawake katika kujikomboa kiuchumi”, alisema Rodriguez.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mahmoud Mohamed aliwakumbusha vijana haja ya kuchangamkia fursa za ajira hasa katika sekta za utalii na uvuvi zinazopatikana kwa wingi katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Alisema serikali ya Zanzibar imetekeleza wajibu wake kwa kuimarisha miundombinu ya kuwawezesha vijana kujiajiri kwa kuweka sera na mipango mbali mbali ili waweze kuendesha maisha yao katika misingi ya amani na utulivu.
“Serikali kazi yake kubwa ni kutengeneza mazingira rafiki ili jamii na wageni waendeshe maisha yao kwa kuzingatia misingi ya amani na Utulivuhivyo niwatie moyo na kuwaomba kuzitumia kikamilifu fursa zilizopo mkatika sekta ya utalii ambayo inachangia karibu asilimia 27 ya pato la Taifa na ambayo imezalisha zaidi ya ajira 88,000 ambazo nyingi zimechukuliwa na wageni kutokana na wazawa kutochangamkia fursa”, alieleza Ayoub.

Semina hiyo ya kiuchumi ni mwendelezo wa majukwaa yaliyofanyika katika mikoa 13 ya Tanzania bara na Zanzibar kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa makundi mbali ya jamii juu ya namna ya kutumia fursa zinazowazunguka kuzalisha ajira a kukuza uchumi wao ambapo kwa mwaka huu imebebe ujumbe wa anzia sokoni.
Baadhi ya washiriki wa Semina ya  Mafunzo ya kuwajenge uwezo vijana wa kupata fursa za ajira wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kufunguliwa kwa semina hiyoiliyofanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Zanzibar.
 Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akihutubia washiriki wa Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa Vijana Wajasiriamali iliyoandaliwa na taasisi ya Fursa Tanzania alipokuwa akiifungua rasmi.
Muanzilishi ambae pia ni msimamizi wa programu ya mafunzo wa taasisi ya Fursa Tanzania Ruge Mutahaba  akitoa darsa kwa Vijana walioshiriki wa Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa Vijana Wajasiriamali Zanzibar.
Mratibu nmkaazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania Alvaro Rodriguez akitoa salamu katika ufunguzi wa Semina ya Mafunzo ya Fursa kwa Vijana Wajasiriamali Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akishikili nembo ya taasisi ya Fursa Tanzania inayotoa ujumbe wa 'Nipo Tayari katika Kampeni ya Kitaifa ya usafi wa Mazingira' mara baada ya kufungua semina ya kutambua fursa za ajira kwa vijana. Kuliakwake ni Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania Alvaro Rudreguez, Mbunge wa Jimbo la Mpendae Salum Turky (mwenye kofia) na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mahmoud Mohamed. (Picha kwa hisani ya OMPR).

No comments:

Post a Comment