Monday, November 13, 2017

RC AYOUB AWATAKA VIJANA KUTUMIA MAZINGIRA YAO KUZALISHA AJIRA

Na Mwinyimvua Nzukwi
VIJANA nchini wametakiwa kutumia fursa zinazopatikana katika mazingira yao ili kuzalisha ajira kwa lengo la kujiendeleza kimaisha.

Kaimu mkuu wa mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mahmoud Mohammed alitoa kauli hiyo katika vijiji vya Nungwi, Bumbwini na Matemwe wakati wa mwendelezo wa ziara zake mkoani humo kusikiliza kera na changamoto zinazowakabili wananchi iliyoanza Novemba 7 mwaka huu.

Alisema kutokana na nafasi chache za ajira zinazopatikana serikalini, vijana wanatakiwa kujikusanya pamoja na kutumia fursa za uwezeshaji kwa kubuni kazi au miradi itakayowapatia kipato.

Aidha Ayoub ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, aliwataka vijana wachache wanaobahatika kuajiriwa katika sekta mbali mbali  kupenda kufanya kazi badala ya kupenda kuajiriwa ili kuongeza uzalishaji utakaoongeza kipato katika taasisi hizo na kuzijengea uwezo wa kutoa malipo mazuri.

"Tutakapotumia vizuri mazingira na fursa zinazotuzunguka tunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ajira kwani tutakuwa na shughuli nyingi za kufanya za kuzalisha mali na kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ajira hasa kwa vijana na wana nwake badala ya sote kusubiri kuajiriwa katika sekta rasmi ambayo ina uwezo mdogo wa kuajiri", alieleza Ayoub na kuwataka kujiendeleza kielimu na kitaaluma.

Wakitoa malalamiko yao mbele ya Mkuu huyo aliyeambatana na Mkuu wa wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja Hassan Ali Kombo na watendaji mbali mbali wa serikali ya wilaya ya Kaskazini ‘A’ na viongozi wa CCM mkoani humo, wananchi wa maeneo hayo walidai kuwa hawanufaiki na uwepo wa mahoteli mengi ya kitalii kwa mambo mbali mbali ikiwemo ajira.

"Kwa idadi ya hoteli ziliopo katika shehia yetu, hatupaswi kuwa tuna lalamikia ajira kwa vijana wetu kwani kicha ya kuwa baadhi yao hawana sifa za kufanya kazi za kitaalamu lakini basi washindwe kufanya hata  kazi ya kuwa mtunza bustani?", alihoji Mbarawa Sheha Haji mkaazi wa shehia ya Nungwi Banda kuu.

Malalamiko hayo pia yalijitokeza katika mikutano ya Mkuu huyo wa Mkoa iliyofanyika katika shehia za Kiwengwa, Matemwe, Donge Mchangani, Kinyasini na Mahonda hali iliyopelekea Mahmoud kumuagiza Afisa wa idara ya Kazi Mkoani humo kushirikiana na masheha wa shehia za ukanda huo kuwabaini wananchi wanaotoka katika shehia zao ambao wameajiriwa katika hoteli hizo.

Aidha Mahmoud aliagiza kukamatwa kwa wanyama watakaoachiwa bila ya udhibiti baada ya wiki moja kuanzia juzi ili kuuweka mji mdogo wa Nungwi katika haiba nzuri.

"Hili la wanyama, viongozi wenzangu lazima ifike wakati tusimamie sheria ya udhibiti wa wanyama kikamilifu. Hivyo natoa wiki moja kila mwenye mbuzi au ng'ombe wake ajue vya kumdhibiti na baada ta muda huo halmashauri kwa kushirikiana na jeshi la polisi ni lazima mchukue hatua kwa mujibu wa sheria", alisisitiza Mahmoud.

Aidha aliitaka halmashauri ya wilaya ya Kaskazini ‘A’ kufanya kazi kwa mashirikiano na wananchi wa shehia zilizomo ndani ya wilaya hiyo kupitia kwa masheha wanapofanya kazi zinazohitaji nguvu ya ziada ili kuepusha upinzani kama ilivyotokea katika ujenzi wa vibaraza vya kuhifadhia taka taka katika shehia za Nungwi, wilayani humo.

Katika ziara hizo Mkuu huyo amekutana na wananchi ambao walieleza kero na changamoto zinazowakabili ambazo baadhi yao zilipatiwa majibu na utatuzi papo hapo na nyengine kutolewa maelekezo kwa watendaji wa taasisi mbali mbali za serikali na binafsi kuzishughulikia katika muda mfupi jambo lililopongezwa na wananchi walio wengi wa mkoa huo .
Mwisho


No comments:

Post a Comment