Saturday, April 14, 2018

WAZEE ZANZIBAR WAMPONGEZA DK. SHEIN KWA KUENDELEZA PENCHENI JAMII, WAMUOMBA KUPUNGUZA UMRI WA WANUFAIKA WANAWAKE



Na Mwinyimvua Nzukwi
Jumuiya ya Wazee Zanzibar (JUWAZA) imeiomba serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kupunguza umri wa wazee wanawake wanaopokea pencheni jamii kutoka  miaka  75 hadi 55 ili kuliwezesha kundi hilo kunufaika na pencheni hiyo.

Wakizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kutimiza miaka miwili toka kuanza kutolewa kwa pencheni hiyo, wazee hao walimshukuru Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuanzisha pensheni hiyo waliyosema imesaidia kuimarisha hali zao na kuondokana na utegemezi.


Walisema kutokana na ukubwa wa kundi hilo katika jamii na kupoteza nguvu kwa haraka ipo haja kwa serikali kuliangalia kundi hilo ili kulisaidia kumudu gharama za maisha.

“Tunapoangalia uwezo wa wanawake wenye umri wa miaka 55 ni tofauti na wanaume wenye zaidi ya umri huo hivyo tunamuomba mheshimiwa Rais (Dk. Shein) kuwaangalia kwa jicho la huruma”, alisema mzee Bamba Ame Haji.

Akizungumzia jinsi anavyonufaika na fedha wanazopokea wazee hao mratibu wa jumuiya hiyo mkoa wa kaskazini unguja nadhar juma alisema ili kuwaendeleza kiuchumi baadhi ya wazee wameamua kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ili kufanya kipato chao kuwa endelevu.

Alisema licha ya kutosita kutolewa kwa pensheni wazee hao walipongeza hatua ya kutolewa mapema fedha hizo ambazo zimewawezesha kujitegemea kutokana na miradi waliyoianzisha.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Khamis Amani alisema idadi ya wanufaika wa pencheni hiyo imeongezeka na kufikia 27,706 kwa Unguja na Pemba.

Aidha alisema pamoja na kunufaika na pencheni hiyo bado kuna changamoto mbalimbali zikiwemo ya uhaba wa wahudumu wanaogawa pensheni hiyo na kusababisha msongamano katika vituo vya kutoa pensheni hizo katika baadhi ya maeneo.

“Pamoja na kuwahi kutolewa kwa pencheni na kuongezwa idadi ya vituo vya kutolea pencheni hiyo bado idadi ya wahudumu katika baadhi ya maeneo yenye wapokeaji wengi tunaomba iongezwe ili kuwapunguzia wazee wetu muda wa kusubiri”, alisema Mwenyekiti.

Pensheni jamii inatolewa kwa wazee waliotimiza umri wa miaka 75 kwa kupatiwa shilingi 20,000 kila mwezi bila ya kujali historia ya utumishi wa mzee husika kwa ajili ya kujikimu kimaisha Zanzibar ikiwa ni nchi pekee inayotoa pencheni hiyo nchi nzima.



No comments:

Post a Comment