NA MWINYIMVUA NZUKWI, ZANZIBAR
Taasisi za fedha nchini zimetakiwa kuendelea kuzisaidia taasisi za umma
na binafsi kuuweka mifumo mizuri ya matumizi ya fedha ili kusaidia maendeleo ya taasisi
hizo na taifa kwa ujumla.
Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud alitoa
wito huo wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili yaliyoshirikisha wakuu
wa taasisi za serikali, mashirika ya umma, taasisi za kiraia na vyuo vya elimu ya juu yaliyoandaliwa na benki ya NMB Tanzania.
Amesema iwapo taasisi hizo zitajengewa uwezo zitaimarisha mifumo
yao ya mapato na matumizi jambo litakalosaidia kukuza mapato yao na kudhibiti
matumizi kulingana na mageuzi ya kiuchumi kupitia mifumo mipya ya kifedha ya kitaifa na kimataifa.
Amesema serikali ya Zanzibar kupitia Mkakati wa Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA I, II,III) imefanya mabadiliko kadhaa katika sektambali mbali ikiwemo ya sekta ya fedha
yaliyolenga kukuza mapato ya serikali, mashirika ya umma na taasisi zisizo za
kiraia hivyo taasisi hizo zinapaswa kuhakikisha zinatumia huduma za kibenki
zinazotolewa na benki hiyo ili kujiendeleza.
“Nchi haiwezi kuendelea kama hakutokuwepo na mifumo mizuri ya
kifedha nah ii ndio maana serikali ikaamua kufanya marekebisho katika sheria
zake ili kuruhusu sekta za fedha zuiweze kutoa huduma bora zitakazosaidia
makundi mbali yaweze kunufaika nazo”, amesema Mahmoud.
Nao washiriki wa mafunzo hayo walisema kuwa yamewasiadia kujua
huduma mbali mbali za kifedha zinazotolewa na benki hiyo sambamba na kuwajengea
uwezo ambao watautumia katika kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kudhibiti
matumizi yao kwa manufaa ya wanachama wa taasisi hizo na jamii kwa ujumla.
Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa bodi ya chama cha wanasheria
wanawake Zanzibar ZAFELA Fatma Gharib ameeleza kuwa mafunzo hayo
yamewashajihisha kutumia huduma mbali mbali za kifedha kama vile kupata ushauri
na mikopo inayotolewa kwa taasisi zisizozalisha faida jambo ambalo litasaidia
kuziimarisha taasisi hizo kuwa na maendeleo endelevu.
“Taasisi zetu (za kiraia) kimsingi huwa zinategemea ruzuku au
misaada na kujua kuwa wajibu wetu katika matumizi ya benki ni kutunziwa fedha
jambao ambalo kupitia semina hii nimeiona fursa pana zaidi ya hiyo ambayo
taasisi zetu inaweza kuitumia kupitia benki hii”, aamesema Fatma.
Akitoa maelezo kuhusu mafunzo hayo mkuu wa biashara za kitaasisi
kutoka makao makuu ya benhi ya NMB William Makoresho amesema mafunzo hayo
yalilenga kuonesha shughuli zinazofanywa na benki yake kwa baadhi ya wateja
wake ili waweze kuzitumia kwa lengo la kuimarisha utendaji wa taaisisi hizo.
“Watu wengi wanafikiria benki yetu inafanya kazi ya kutunza fedha
au kutoa mikopo kwa wateja wetu pekee lakini kupitia semina hii tumeweza
kuwaelezea washiriki ukubwa huduma na faida zinazoweza kupatikana na sisi kuweza
kujua mahitaji ya wateja wetu hivyo ningependa kuwaalika waendelee kutumia
huduma za benki na kifedha zinazotolewa na benki yetu”, amesema Makoresho.
Nae Meneja wa benki hiyo tawi la Zanzibar Abdallah Duchi amesema
mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kuyafikia makundi mbali ya
kijamii ili kuwaelezea umuhimu wa kutumia huduma za kifedha katika kukuza
uchumi wa taasisi na kwamba katika mafunzo benki hiyo iliwafikia Wakurugenzi wa
taasisi na mashiriika ya serikali, Wakurugenzi wa taasisi za kiraia na Wakuu wa
taasisi za elimu ya juu ili kuwajengea uwezo juu ya namna bora ya kuongeza
mapato na tija ya taasisi zao.
Meneja wa tawi la NMB Zanzibar Abdallah Duchi (wa pili kutoka kushoto) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud (wa pili kulia) kuhusu semina ya watendaji wakuu wa taasisi za serikali, mashirika ya umma na asasi za kiraia kabla ya Mkuu huyo kufunga rasmi mafunzo hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud (kushoto) akihutubia washiriki wa semina ya wakuu wa taasisi za serikali, mashirika ya umma na asasi za kiraia yaliyoandliwa na benki ya NMB. Kulia ni Mkuu wa huduma za Biashara za Taasisi wa benki ya NMB William Makoshero.
Baadhi ya washiriki wa semina ya wakuu wa taasisi za serikali, mashirika ya umma, taasisi zisizo za kiserikali na vyuo vya elimu ya juu (waliosimama) wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud (wa pili kulia waliokaa) mara baada ya kufunga semina hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud (wa tatu kulia) akijadiliana jambo na Meneja wa NMB Zanzibar Abdallah Duchi (wa pili) na mkuu wa biashara za kitaasisi William Makoshero.
No comments:
Post a Comment