Sunday, April 15, 2018

'ZANZIBAR OLD STARS' YATAKA WENYE MAMLAKA YA SOKA LA ZANZIBAR WAWATUMIE


Na Salum Vuai, MAELEZO
TIMU ya soka ya wachezaji wa zamani Zanzibar Old Stars, imemuomba Mkuu wa Mkoa wa Mjini  Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud, kusaidia kuwaelimisha wadau  na mamlaka za michezo juu ya umuhimu wa kutunza kumbukumbu zinazohusiana na mchezo huo nchini.

Akizungumza wakati uongozi wa timu hiyo ulipokwenda kumshukuru Mkuu huyo na kumkabidhi kikombe cha ushindi wa mechi ya ‘Karume Day’, Katibu Mkuu wa kikosi hicho Salum Hamduni, alisema inasikitisha kuona wanasoka walioiletea sifa Zanzibar hawathaminiwi hata kwa kutakiwa ushauri.

Alisema tafauti na nchi nyengine, Zanzibar haina utaratibu wa kutunza historia za wanamichezo wake wa zamani ambao waliiwakilisha kimataifa na kuifanya itambuliwe na kuheshimiwa ndani na nje ya nchi.



Hamduni, alimuomba Mkuu wa Mkoa atumie nafasi yake kuhakikisha wanamichezo wa zamani wanapewa hadhi na kushirikishwa katika baadhi ya mambo ya kitaifa, ikiwemo kusikilizwa maoni yao wakati wa kuunda timu za taifa.

“Sisi tumecheza mpira zamani na kwa kiasi kikubwa tulisaidia nchi yetu Zanzibar kufahamika na kuheshimiwa. Kwa vyovyote vile hatukosi kuwa na maarifa yanayoweza kusaidia katika jitihada za kuendeleza michezo kama nchi nyengine zinavyowapa umuhimu maveterani wao na hata kuwaalika kwenye mashindano makubwa,” alifafanua.

Katibu huyo alieleza kusikitishwa kwao na namna watu wanaopewa dhamana ya kuongoza vyama vya michezo hasa mpira wa miguu, wanavyowachukulia wazee kuwa ni maadui badala ya kuwavuta kwa ajili ya kuchota uzoefu na maarifa katika kupeleka mbele sekta ya michezo nchini.


Mapema, Kocha Mkuu wa timu hiyo Abdalla Maulid, alimuomba Mkuu wa Mkoa kuwakutanisha wadau na mamlaka za michezo ili kujadili namna wanavyoweza kunufaika na mchango wa wanamichezo wa zamani kwa lengo la kurejesha hadhi ya michezo nchini.

Alishauri hata wakati wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi, kuandaliwe mchezo maalumu ama siku ya ufunguzi au fainali, utakaowakutanisha wakongwe hao na wenzao wa Tanzania Bara ili kuwafanya vijana wa sasa kuwatambua watangulizi wao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa pamoja na kukubali kuwa mlezi wa Zanzibar Old Stars, aliahidi kufanya kila awezalo kuhakikisha timu hiyo inaimarika na kuwa nembo muhimu ya michezo visiwani Zanzibar.


Alisema, miongoni mwa majukumu yake, ni kuhakikisha agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kurejesha vuguvugu la michezo nchini linatekelezwa na kufanikiwa.
  
Mapema, kaimu nahodha wa timu hiyo Ali Sharif ‘Adolph’, alimkabidhi Mkuu wa Mkoa kikombe walichokipata baada ya kuichapa Young Africans Veterans mabao 2-1 katika mchezo wa maadhimisho ya kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume uliopigwa Aprili 8, 2018 katika uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.


 Mkuu huyo wa Mkoa ndiye  aliyedhamini safari ya timu hiyo iliyoasisiwa mwaka 2009 kwa ajili ya kuwaunganisha wanandinga hao na kuiwekea Zanzibar historia kisoka.


No comments:

Post a Comment