NA MWINYIMVUA NZUKWI
Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Ayoub
Mohammed Mahmoud amewataka washiriki wa mbio za baskeli za Afrika Mashariki kutangaza
vivutio vya utalii viliopo na amani ya nchi za afrika mashariki ili kukuza uchumi wan chi hizo unaotegemea
pato la utalii.
Akihutubia wananchi na washiriki wa mbio hizo
katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar, RC Ayoub amesema mbio hizo zikitumika
kusambaza na kueneza ujumbe wa amani zitasaidia kuwashawishi na kuwakumbusha
wananchi juu ya umuhimu wa kulinda amani iliyopo pamoja na uhifadhi wa
mazingira kwa lengo la kuimarisha utalii wa ndani wa Zanzibar na Tanzania bara.
Amewataka washiriki hao wanaotoka katika nchi
mbali mbali za ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini kutumia muda mchache
watakaokuwepo Zanzibar kupitia vivutio vya utalii vilivyopo na kwenda
kuvitangaza katika nchi zao sambamba na kuelezea hali ya amani iliyopo nchini.
Aidha aliishukuru wizara ya Habari, Utamaduni na
Mambo ya Kale kwa kuamua kushirikiana na taasisi ya Afrika Mashariki Festival kwa
kuamua kuanzisha mbio hizo ndani ya mkoa wa Mjini Magharibi mbio ambazo
zinatarajiwa kufanyika pia katika mkoa wa Dar es salam ambazo amesema zitasaidia
kukuza uwekezaji katika sekta mbali mbali ikiwemo ya utalii.
Mapema akitoa taarifa za mbio hizo katibu
mtendaji wa kamisheni ya utalii Zanzibar Dkt. Vuai Idi Lila amezitaja nchi
zilizotoa washiriki wa mbio hizo kuwa Tanzania bara, Kenya, Uganda, Rwanda,
Burundi, Ethiopia, afrika kusini na wenyeji Zanzibar.
Amesema mbio hizo ni sehemu ya mikakati ya
kamisheni yake ya kuimarisha utalii nchini katika majira yote kama moja ya azma
ya serikali ya Zanzibar pamoja na kukuza uhusiano na wadau wengine wa utalii
nchini.
Jumla ya washiriki 72 wakiwemo wanawake wawili
kutoka nchini Kenya walishiriki mbio hizo za umbali wa kilomita 60 zilizoanzia
katika uwanja wa Amaan kupitia Welezo, Mwera, Dunga, Jendele, Unguja Ukuu,
Bungi, Tunguu na kurudia njia ya Mwera
hadi uwanja wa Amaan.
Washiriki wa mbio za baskeli za afrika mashariki wakijiandaa kuanza mbio hizo.
Mkuu wa mkoa wa mjini magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud akipeperusha bendera ya jumuiya ya afrika mashariki kuashiria kuanza kwa mbio za baskeli za Afrika Mashariki
Mmoja kati ya wanawake wawili walioshiriki mbio hizo kutoka nchini Kenya.
No comments:
Post a Comment