NA MWINYIMVUA NZUKWI
Mkuu wa Mkoa wa Mjini
Magharibi ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kamati ya Uongozi ya Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini TASAF III Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka wajumbe
wa Kamati hiyo kuzidisha mashirikiano na watendaji wa mpango huo ili
utekelezaji wake uoneshe matokeo yanayopimika.
Akizungumza katika Mkutano
wa kutathmini utekelezaji wa mpango huo katika kipindi cha mwaka 2017, uliofanyika
katika ofisi za TASAF Mazizini Unguja, alisema kufanya hivyo kutasaidia
kupunguza changamoto zilizobainika ikiwemo ya kutopatikana kwa matokeo
yaliyotarajiwa katika baadhi ya miradi inayotekelezwa.
Alisema mradi huo
umelenga kupunguza changamoto za kiuchumi na kujenga uwezo wa kaya kumudu
mahitaji muhimu ya kila siku hivyo suala la umakini wakati wa uibuaji wa miradi
lina umuhimu mkubwa hivyo wajumbe wa Kamati hiyo ambao ni Wakuu wa Mikoa, Wakuu
wa Wilaya, Wakurugenzi wa Manispaa na Halmashauri za wilaya na Watendaji wa
kisekta wana jukumu la kusadia utelelezaji wake.
Alisema iwapo viongozi wa
mikoa, wilaya na shehia watayaainisha na kuyatambua maeneo ya vipaumbele,
itarahisisha na kupunguza changamoto mbali mbali zinazoikabili miradi hiyo
ikiwemo ya kutoendelea kwa baadhi ya miradi baada ya mradi kukamilika jambo
linalorudisha nyuma juhudi za serikali za kukuza uchumi na kupambana na
umaskini.
“Suala la kushirikiana
katika hili si la TASAF pekee na ndio maana na sisi tukawa wajumbe wa Kamati hii
hivyo ni lazima tuvitambue vipaumbele vya watu wetu kabla ya kuibua miradi ili
iwe rahisi kupata tija hivyo nashauru watendaji wa tasaf muwe karibu na ofisi
zetu lakini na sisi tuwe wafuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa miradi ya
tasaf katika maeneeo yetu”, alieleza Mahmoud.
Akizungumzia utekelezaji
wa mpango wa malipo kwa njia ya mtandao kwa wanufaika wa mpango huo Mahmoud
aliipongeza TASAF kwa kubuni utaratibu huo ambao licha ya kurahisisha malipo
kwa walengwa pia utasaidia kupunguza mianya ya ubadhirifu, udanganyifu na
ucheleweshaji wa malipo ya wanufaika jambo ambalo alisisitiza liendelezwe huku
taasisi hiyo ikizifanyia kazi changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji
wake.
Mapema akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa mpango huo kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi
Disemba 2017, Mratibu wa TASAF Unguja Makame Ali Haji alisema katika kutekeleza
majukumu yake ya msingi jumla ya shilingi bilioni 3,699,541,933 zililipwa
kwa walengwa wa mpango wa uhaulishaji fedha ambao ni sehemu ya majukumu ya
mpango katika shehia 126 za utekelezaji ndani ya mizunguko 53.
Alieleza kuwa katika
utekelezaji wa miradi ya kutoa ajira za muda kwa walengwa, mpango huo katika
mwaka 2016/2017 ulitekeleza miradi 106 katika shehia 104 iliyohusika katika
sekta za kilimo, misitu na mazingira ambapo shilingi bilioni
2,590,649,700 zilitumika.
Amefafanua kuwa katika
fedha hizo shilingi bilioni 2,006,123,300 zilitumika kulipia
ujira kwa walengwa wakati shilingi milioni 584,526,400 zilitumika
kwa kununulia vifaa vya kutekelezea miradi hiyo
Aliongeza kuwa katika kipindi cha
kuanzia mwezi Julai hadi Novemba 2017 jumla ya miradi 190 iliyohusisha sekta za
kilimo na umwagiliaji iliyokuwa na miradi 82, misitu miradi 91, uvuvi miradi 6
na mazingira 11 iliibuliwa, kusanifiwa na kutekelezwa ikiwa ni utekelezaji wa
mradi huo katika kipindi cha mwaka 2017/2018 kinachoendelea.
Kwa upande wa mpango wa
kuweka akiba na kukuza uchumi wa kaya Makame alieleza kuwa mpango huo umelenga
kujenga msingi wa kaya kuondokana na umaskini kwa njia ya kujiwekea akiba na
kuwekeza katika vikundi vya kumjengea uwezo wa kibiashara, kilimo na kuongeza
thamani ya kipato katika kaya ambapo jumla ya vikundi 970 vimeundwa katika
shehia 126 za utekelezaji wa mpango huo uliohusisha walengwa 13,253, wanawake
12,825 na wanaume 410.
Akielezea mafanikio ya
utekelezaji wa mpango huo katika kipindi hicho Mratibu huyo alieleza kuwa
asilimia 98 ya wanufaika wa mpango huo walipokea ruzuku zao katika vipindi
vyote kwa wakati huku asilimia 94 ya wazazi waliomo katika mpango waliweza
kutimiza masharti ya kumudu gharama za masomo ya watoto wao pamoja na
kuwahamasisha watoto wenye umri wa kwenda skuli kuandikishwa na kuanza elimu ya
msingi.
Hata hivyo Mratibu huyo
alisema katika utekelezaji wa mpango huo katika kipindi hicho walikabiliana na
changamoto mbali mbali ikiwemo ya kuhamahama kwa baadhi ya wanufaika kutoka
shehia moja kwenda nyengine bila ya kutoa taarifa kulipelekea kushindwa
kufanyika kwa uhaulishaji wa fedha na kuibuka kwa dhana ya kuwepo kwa wanufaika
hewa jambo alilosema limeshapatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na masheha
zinazotekeleza mpango huo.
“Mbali na hilo pia
tulikutana na tatizo la upotevu wa vitendea kazi katika baadhi ya shehia
uliotokana na umakini mdogo katika usimamizi wake mara baada ya
mradi kukamilika jambo ambalo linasababisha hoja nyingi kutoka kwa walengwa
ambao walikabidhi vifaa kwa masheha lakini pia elimu ndogo ya ujasiriamali
ilichangia kutoendelea kwa vikundi vya uzalishaji mali vilivyoanzishwa”,
alieleza Makame.
Wakichangia taarifa hiyo
wajumbe wa mkutano huo waliipongeza TASAF III kwa kusimamia vyema utekelezaji
wa miradi iliyomo katika mpango huo na kuitaka kuwa karibu na Kamati za shehia
na kuzijengea uwezo Kamati hizo ili ziweze kuleta ufanisi miradi ianayoibuliwa
na kuleta tija kwa walengwa na jamii kwa ujumla.
Walisema katika
kutekeleza mpango huo ipo haja kwa mpango huo kuibua miradi itakayosaidia
kupunguza umaskini wa kipato cha kaya pamoja na kutafuta masoko ya bidhaa
zinazozalishwa na wanufaika wa mpango huo ili kuwaendeleza kiuchumi.
“Katika kutekeleza hii
dhana ya utalii kwa wote, nadhani tasaf ingeanzisha mpango wa kuwaendeleza
wazalishaji wetu ili waweze kuzalisha bidhaa zinazoweza kukubalika katika soko
la utalii ili waweze kunufaika na mapato yake pamoja na kuwatafutia masoko ya
bidhaa zao ambazo ni bora”, alieleza mkuu wa mkoa wa kaskazini unguja Vuai Mwinyi.
Nae Mratibu wa TASAF
Zanzibar Saida Saleh Adam mbali ya kuwashukuru wajumbe wa Kamati hiyo
aliwaahidi kuyafanyia kazi maoni na mapendekezo waliyoyatoa ili kuongea ufanisi
wa mpango huo ambao toka uanze kutekelezwa umekuwa na matokeo makubwa katika
kukuza uchumi wa kaya na jamii kwa ujumla.
“Katika awamu zote za
utekelezaji kuanzia awamu ya kwanza hadi hii (ya tatu) mpango huu umekuwa na
mafanikio makubwa ukilinganisha na changamoto zinazojitiokeza hivyo ninawaomba
waheshimiwa wakuu wa wilaya na mikoa kuendelea kuunga mkono mpango huu ikiwa ni
pamoja na kupita hasa wakati maafisa wetu wanapokuwa katika maeneo yenu kwa
lengo la kutilia mkazo utekeklezaji wa mpango”, alisema mratibu huyo.
Mpango wa kunusuru kaya
maskini ni mmoja ya mipango ya kitaifa unaotekelezawa Tanzania bara na Zanzibar
ukiwa na lengo la kuziwezesha kaya maskini sana kuongeza kipato, fursa na uwezo
wa kugharamia mahitaji muhimu ya kibinaadamu kama vile chakula, afya na elimu
ambapo hadi sasa kaya 126 kati ya 146 zilizofikiwa na mpango zinaendelea
kunufaika.
No comments:
Post a Comment