NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi ameinasihi jamii kuepuka kukata miti ovyo na badala yake irejee katika
utamaduni ya kuotesha miti katika maeneo wanayoishi ili ardhi iendelee kubakia
katika maumbile yake ya kawadia.
Alisema hivi sasa
kiwango cha maji katika ardhi kinaendelea kupungua kutokana na tabia ya wanaadamu
kuchafua mazingira ikiwemo ukataji ovyo wa misitu jambo ambalo ni hatari kwa
maisha ya viumbe.
Balozi Seif Ali Iddi
ambae pia ni Mwakilishi wa jimbo la Mahonda alitoa nasaha hizo wakati wa
sherehe za uzinduzi wa visima viwili vya maji safi na salama vilivyochimbwa
katika kituo cha afya jimbo la Donge na skuli ya msingi na sekondari za Mahonda
jimbo la Mahonda.
Visima hivyo ikiwa
miongoni mwa Visima 15 vitakavyochimbwa ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B” ambapo
Jimbo la Mahonda pekee vitakuwa Visima Vitano ni msaada kutoka Taasisi ya
Kiraia ya ‘Zanzibar Relief and Development Foundation’ - ZARDEF chini ya ufadhili
wa Ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania.
Balozi Seif alisema
shida ya Maji safi na salama katika baadhi ya maeneo visiwani Zanzibar licha ya
kusababisha na ongezeko la idadi ya watu nchini lakini bado
pia huchangiwa na uharibifu wa mazingira unaopaswa kuepukwa kwa
nguvu zote.
Alisema akiwa
msimamizi wa shughuli za serikali atafanya ziara katika maeneo mbali mbali
kuangalia shughuli za mazingira hasa kwa vile taasisi hizo zimeingizwa katika wizara
yake kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Rais wa Zanzibar hivi karibuni
katika taasisi za umma.
Balozi
Seif aliwakumbusha wananchi kwamba ni wajibu wa walimu, wanafunzi na
wananchi wote wa majimbo ya Mahonda na Donge kusimamia utunzaji wa Visiwa hivyo
pamoja na rasilmali zilizomo katika majengo ya huduma za Kijamii kama skuli na vituo
vya afya.
Alifahamisha kwamba visima
vilivyochimbwa ni waji wa wahusika hao kuhakikisha vinaendelea kudumu kwa muda
mrefu kwa vile hauna asiyetambua kwamba maji ni neema kwa wanaadamu pamoja na viumbe
vyote vyenye uhai.
Alisema haitakuwa ni
jambo la busara kwa Viongozi pamoja na Taasisi zinazofadhili Miradi ya Jamii
katika maeneo tofauti Nchini kupata Taarifa ya uwepo wa uharibifu wa Miradi
wanayofadhili.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar aliiahidi Taasisi ya ZARDEF kuipa kila msaada
katika kuona malengo iliyojipangia inayatekeleza kwa ufanisi mkubwa.
Balozi Seif alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini jitihada na Malengo iliyojiwekea
Taasisi hiyo inayokwenda sambamba na serikali katika kuimarisha miradi ya maendeleo
kwa wananchi wote hasa katika sekta za kilimo, uvuvi na biashara.
Akitoa Taarifa ya
Miradi ya Uchimbaji wa Visima katika maeneo mbali mbali nchini Mratibu wa
Taasisi ya ZARDEF Salum Ramadhan Abdulla alisema Taasisi hiyo kwa sasa
imejikita katika uchimbaji wa visima vya maji ikidhamiria kusaidia
kuondoa tatizo la huduma hiyo ifikapo mwaka 2020.
Bwana Salum alisema
utafiti umeonyesha wazi kwamba kundi kubwa linaloendelea kuathirika na ukosefu
wa huduma ya maji safi na salama ni wanawake na watoto wanaolazimika wakati
mwengine kuacha shughuli zao za kujitafutia riziki na Masomo.
Mratibu huyo wa
ZARDEF aliongeza kwamba Taasisi hiyo imejiwekea malengo ya muda mrefu katika
kuimarisha miradi minne mikubwa itakayoelekezwa zaidi kwa kundi kubwa la vijana
katika azma ya kuwaondoshea changamoto ya upatikanaji wa ajira.
Aliitaja miradi hiyo
kuwa ni pamoja na mafunzo ya uzasiriamali, uvuvi wa samaki utakaohusisha boti tatu kubwa
zitakazolenga uvuvi wa bahari kuu, kilimo cha kisasa pamoja na ufugaji wa kuku
na ng’ombe wa kisasa.
Mratibu huyo wa
ZARDEF aliiomba serikali kuu kutoa agizo maalum la kuja kuyataka mahoteli
ya kitalii nchini kununua bidhaa za samaki pamoja na zile za mboga
mboga zitakazotokana na mradi huo.
Akitoa shukrani kwa niaba
ya wananchi wa majimbo ya Mahonda na Donge mwakilishi wa jimbo la Donge ambae
pia ni Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohammed
ameipongeza taasisi ya kiraia ya ZARDEF kwa uharaka wa malengo yake
iliyojipangia.
Dk. Khalid alisema visima
hivyo viwili vilivyochimbwa ndani ya maeneo ya Makundi ya jamii katika huduma
za kitabibu na elimu ni sadaka maalum ya wananchi wawili wa uturuki ambapo
mmoja ni marehemu wenye mapenzi na Zanzibar.
Aliihakikishia
Taasisi ya ZARDEF kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea
kushirikiana na Taasisi hiyo na pale itapobidi itakuwa tayari kusamehe kodi kwa
baadhi ya vifaa vitakavyoletwa nchini kwa kusaidia huduma mbali mbali za kijamii.
Akitoa salamu zake
Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Ali Davutoglu alisema visima hivyo
viwili vilivyozinduliwa ni alama ya ushirikiano kati ya Uturuki na Zanzibar na
Tanzania kwa ujumla.
Alisema Ubalozi wa
Uturuki Nchini utajitahidi katika kuona ushirikiano huo unazidi kuimarika na
kudumu kwa muda mrefu ambapo alisisitiza kwamba Uongozi wa Ubalozi huo uko
tayari kusaidia Miradi ya huduma za Umeme pale itapoonekana yapo mahitaji
katika sekta hiyo mahali popote Nchini Tanzania.
Visima viwili
vilivyochimbwa katika Kituo cha Afya cha Donge Kitaluni na Skuli ya Mahonda msingi
na sekondari na kusimamiwa na Taasisi ya ZARDEF chini ya ubalozi wa Uturuki
Nchini Tanzania vina thamani ya shilingi Milioni 11.3 ambapo kila kimoja kiligharama
shilingi Milioni 5.65.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif (wa pili kulia) akiwa na Balozi wa Uturuki Nchini Tanzania Ali Davutoglu na Mkewe Yetsin Mecco wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa kisima cha maji safi na salama katika Skuli ya Mahonda uliokwenda sambamba na kisima cha Donge Hospitali.
Balozi Seif akifungua pazia kuashiria uzunduzi wa visima vilivyochimbwa na taasisi ya Zanzibar Relief and Development Foundation - ZARDEF chini ya usimamizi wa ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania.
Balozi Seif akimshukuru mke wa Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Yetsin Mecco ambae ndie mfadhili wa visima vilivyochimbwa Donge na Mahonda. (PICHA NA HABARI KWA HISANI YA OMPR).
No comments:
Post a Comment