Na Is-Haka Omar, Zanzibar.
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameshauriwa
kuendeleza harakati za kulinda, kutetea na kusimamia misingi ya taasisi hiyo
ili kuenzi kwa vitendo juhudi za waasisi wa ASP na TANU.
Hayo ameyasema Katibu Mwenezi CCM Wilaya ya Dimani
Hassan Suleiman Jaku, katika ziara ya Makatibu uenezi wa CCM
ngazi za matawi hadi Wilaya ya Dimani walipotembelea maeneo ya
historia ya kumbukumbu ya aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Aman
Karume, Kisiwandu Unguja.
Makatibu wenezi wakipata maelezo ndani ya chumba alichouawa muasisi wa mapinduzi ya Zanzibar Sheikh Abeid Aman Karume.
Amesema nguvu za Chama Cha Mapinduzi zinatokana na
wanachama wazalendo wanaolinda na kuthamini urithi wa Chama hicho toka enzi za
vyama vya ASP na TANU.
Katibu huyo Mwenezi amesema lengo la ziara hiyo ni
kuwajengea uwezo watendaji wa Chama hasa wenye dhamana ya masuala ya itikadi na
uenezi wajue uhalisia wa historia ya nchni ili nao wawafundishe wanachama
wengine.
Amesema viongozi hao wamepewa darasa la
itikadi na kujifunza mambo mbali mbali darasani na kwa sasa wamefikia hatua ya
kujifunza kwa vitendo na kwenda katika maeneo mbali mbali ya kihistoria na
kujionea wenyewe maeneo hayo.
Ameeleza kuwa mambo mema yaliyoasisiwa na marehemu
Karume na Wana Mapinduzi wenzake ni urithi wa kudumu unaotakiwa kuthaminiwa na
kila mwananchi.
Makatibu wenezi wakiomba dua mbele ya kaburi la muasisi wa mapinduzi ya Zanzibar Sheikh Abeid Aman Karume.
Pia ameeleza kuwa moja ya mbinu ya kushinda mbinu
chafu za wapinga maendeleo ni kuhakikisha CCM inashinda na kuendelea kushika
dola katika uchaguzi mkuu ujao.
“Tusomeni historia ili tuwe na ujasiri wa kulinda
neema hizi tulizorithiwa na wazee wetu na baadae vizazi vyetu viweze kujifunza
mambo mema kukoka kwetu na kupigania nchi yao ibaki katika mikono ya Serikali
ya CCM.”, amesema Hassan.
Naye Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Dimani,
Abdallah Maulid amesema viongozi, wanachama na watendaji kwa ujumla wanatakiwa
kujifunza historia halisi ya Zanzibar kwa lengo la kukabiliana na changamoto za
upotoshwaji zinazosambazwa na wapinzani.
Amesema vijana wa CCM wanatakiwa kujiunga na
madarasa ya Itikadi kwa lengo la kujifunza masuala mbali mbali ya
historia, Demokrasia na mwenendo wa siasa za visiwa vya Zanzibar.
Katika ziara hiyo wametembelea eneo alilouwawa
marehemu Abeid Aman Karume pamoja na kumuombea dua katika eneo la kaburi
alipozikwa Mwasisi huyo wa Mapinduzi.
No comments:
Post a Comment