MWINYIMVUA NZUKWI
'Misitu na miji endelevu; tuhifadhi
misitu na miti kwa ustawi wa miji ili tuishi kwa furaha'.
Ni ujumbe wa mwaka huu Kimataifa
katika kuadhinmisha siku ya misitu ulimwenguni ianyoadhimishwa kila mwaka
ifikapo Machi 21.
Pamoja na ukongwe wake toka
ilipoasisiwa na umoja wa mataifa mnamo mwaka 2012, bado siku hii ni ngeni
miongoni mwa wananchi wa Zanzibar ambao kwa kiasi kikubwa ni watumiaji wa
bidhaa za misitu kwa mahitaji mbali mbali ya kijamii kama vile ujenzi, chakula
na dawa.
Uwepo wa siku hii bila shaka kama
zilivyo siku nyerngine za kimataifa zinazoangukia katika sekta mbali mbali,
umelenga katika jambo mahsusi ambalo linahitaji mazingatia na mikakati
madhubuti kwa manufaa ya jamii nzima.
Baada ya miaka 6 toka kuasisiwa kwa
siku hiyo, Idara ya misitu na maliasili zisizorejesheka Zanzibar inatarajia
kuadhimisha kwa shughuli mbali mbali ikiwemo kongamano la wazi kwa wadau wa misitu
na wananchi litakalofanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la wawakilishi Kikwajuni.
Kwa mujubu wa maafisa kutoka idara ya
misitu na rasilimali zisizorejesheka Zanzibar maadhimisho ya mwaka huu yatajumuisha
makundi mbali mbali ya jamii, taasisi za serikali na binafsi kwa lengo la kutoa
elimu juu ya umuhimu wa misitu katika maisha ya viumbe hai.
Mkuu wa kitengo cha misitu ya jamii
Samira Makame Juma, Mkuu wa kitengo cha utafiti Aziza Yunus Nchimbi na Afisa
Msaidizi wa kitengo cha misitu ya jamii Asya Yussuf Khamis wa idara hiyo wamesema
katika kongamano hilo wadau wa sekta ya misitu na wengine watapata fursa ya
kutathmini mafanikio na changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta hiyo nchini.
Walisema pia kongamano hilo limelenga
kuamsha ari na kujenga tabia ya jamii kupanda miti katika maeneo wanayoishi ili
kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na uchafuzi wa hewa jambo ambalo
limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa maradhi.
Maafisa hao walisema kwa muda mrefu
idara yao imekuwa ikiyahamasisha makundi mbali mbali ya jamii na wananchikupanda
miti hasa katika maeneo yaliyoharibiwa na shughuli za kijamii kama vile
shughuli za uchimbaji wa mchanga lakini kupitia kongamano hilo wananchi
watanufaika zaidi kutokana na mada zitakazowasilishwa ambazo zinazohusiana na
ujumbe wa mwaka huu.
“Utafiti unaonesha kuwa mahitaji ya
bidhaa za misitu zinazotumika nchini kwa mwaka ni juu ya wastani wa
uzalishaji unaotokana na eneo la misitu na miti tuliyonayo hivyo upungufu
unaojitokeza huzibwa na bidhaa za misitu zinazoagizwa kutoka nje ya nchi na
kutokana na pengo hilo ndipo kunakopelekea kutokea kwa wimbi kubwa la ukataji
wa misitu na miti kwa mahitaji mbali mbali”, alieleza Aziza yunus nchimbi mkuu
wa kitengo cha utafiti katika idara hiyo.
Alieleza kuwa katika kukabiliana na
wimbi hilo idara yao imekuwa ikiendesha zoezi la kukamata misumeno
ya moto ambayo inayoonekana kuchochea kwa kiasi kikubwa ukataji wa miti na haribifu
wa misitu nchini.
“Hivi karibunu tuanatarajia
kuiangamiza misumeno yote iliyokamatwa katika operesheni zilizofanyika ili
kutekeleza matakwa ya sheria ambayo imeweka zuio la kuingizwa nchini na
kutumika kwa misumeno ya moto lakini pia bado tutaendelea kutoa
elimu kwa jamii kuona umuhimu wa kutunza misitu kwa maisha endelevu ya jamii
yetu”, alieleza Samira.
Nae Asya akizungumzia hatua
zinazochukuliwa na idara hiyo ili kuzuia uharibifu wa misitu alisema
wanaendelea kufanya tafiti mbali mbali ili kubaini ukubwa wa misitu na aina ya
miti, wanyama na wadudu wanaopatikana katika misitu hiyo ili kusaidia kuweka
mikakati madhubuti ya uhifadhi wa misitu nchini.
“Mtazamo wa idara yetu katika
kuendeleza usimamizi wa misitu mijini na vijijini pamoja kwa kusimamia sheria
za uhifadhi wa misitu lakini pia kushirikiana na jamii katika kuitunza miti
inayopandwa ili kuendelea kupata faida inayotokana na miti bila ya kuathiri
mazingira”, alisema afisa huyo.
Katika mwaka uliopita (2017) Shirika la Chakula Duniani (FAO) liliiadhimisha siku hii katika makao makuu ya
shirika hilo mjini Roma, Italia, ambapo Mkurugenzi mkuu, Jose Graziano da Silva, alifungua
maadhimisho hayo yaliyoambatana na uwasilishaji wa ripoti na mada mbali mbali
zilizohusiana na ujumbe wa mwaka huo uliokuwa ‘misitu na nishati’.
Miongoni mwa mada zilizowasilishwa
na kujadiliwa ni pamoja na majukumu ya misitu na nishati ya kijani katika
utekelezaji wa makubaliano ya Paris ya ‘Nationally Determined Contributions –
NDCs’, ambayo ilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Fiji, Jioji Konusi Konrote.
Bila shaka baada ya nmwaka mmoja kupita, ipo haja kwa dunia
na mataifa wanachama wa FAO kutathmini ni kwa kiasi gani jamii hasa za
zinazoishi maeneo ya mijini na vijijini zinaepukana na athari za uharibifu wa
misitu bila ya kuathiri mifumo yao ya maisha.
Kwa mfano jamii nyingi zilizopo mijini, hutegemea mkaa kama
nishati kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, mkaa ambao ili upatikane ni lazima
miti ikatwe hivyo ipo haja ya kuwekwa mipango endelevu ya kuendeleza misitu kwa
kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala.
Miongoni mwa nishati hizo ni pamoja na gesi, umeme asili
unaotokana na nmabaki ya vyakula au vinyesi vya wanyama na kadhalika huku
hamasa ikiendelea kutolewa kwa jamii kupanda miti ya aina mbali mbali
itakayotumika kwa ajili ya nishati yamatumizi ya nyumbani na ujenzi.
Siku ya kimataifa ya misitu ilianzishwa na Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa mwaka 2012 na kuanza kusherehekewa kwa mara ya kwanza ulimwenguni
kote Machi 21, 2013 na kwa Zanzibar siku hiyo itaazimishwa Machi 21, 2018.
.
No comments:
Post a Comment