NA MWINYIMVUA NZUKWI
WAJASIRIAMALI nchini wametakiwa kuzalisha bidhaa zinazozingatia ubora na viwango ili kukuza mitaji na kuhimili ushindani wa soko la ndani na nje.
Akifungua semina ya udhibiti wa ubora wa viwango kwa wajasiriamali wanaoteneneza sabuni, muda mchachje baada ya kula kiapo cha kuendelea kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya biashara na viwanda Zanzibar Ali Juma Khamis alisema serikali kupitia taasisi ya viawango Zanzibar (ZBS) imeamua kutoa mafunzo hayo kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa.
Alisema pamoja na kuwepo kwa wazalishaji wa bidhaa za sabuni aina mbali mbali bado bidhaa hizo zimeshindwa kuingia katika soko kubwa la utalii kutokana na wingi wa wazaklishaji kutozalisha kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
“Sabuni mnazozalisha ambazo huwa na vionjo vya viungo vya asili ya Zanzibar na kuwavutia watumiaji wengi lakini mara nyingi hukosa kuingia katika soko la kimataifa kutokana na kutozingatiwa kwa ubora na viwango jambo ambalo mnapaswa kulizingatia ili kukuza biashara zenu”, alieleza Khamis.
Aidha aliwataka wazalishaji hao kutumia vyema fursa ya uanzishwaji wa wakala wa viwanda vidogo vidogo (SMIDA) ambayo itawawezesha wajasiriamali wa kila wilaya kupata ujuzi na jmikopo ya kuendeleleza bishara zao.
“Serikali imeanza mchakato wa kuisimamisha hii taasisi ili kuwafanya wajasiriamali wa Zanzibar kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kueneza elimu ya ujasiriamali kwa wale watu ambao bado hawajaanzisha biashara ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kupunguza tatoizo la ajira kwa vijana”, alieleza Khamis.
Mapema akitoa maelezo katika semina hiyo Mkurugenzi Mkuu wa ZBS Mwadini Khatib Mwadini alieleza kuwa semina hiyo ni mwendelezo wa mafunzo yanayotolewa na taaisisi yake kwa wajasiriamali wanaozalisha bidhaa mbali mbali ili kukuza ubora wa bidhaa zao.
“Katika mafunzo haya tumeanza na wazalishaji wa bidhaa za sabuni baada ya kugundua kuwa pamoja na kuwepo kwa uzalishaji mkubwa wa bidhaa hiyo na soko nlake bado bidhaa nyingi hazina alama ya ubora jambo linalochangia kutoingia katika masoko makubwa hasa la utalii ambalo lina firsa nyingi kwa wajasiriamali wetu”, alisema Mwadini.
Akiwasilisha mada katika semina hiyo mkufunzi wa mafunzo hayo George Mang’ala Buchafwe aliwataka wajasiriamali hao mbali ya kuzalisha bidhaa bora kwa kutumia viungo vya asili ya Zanzibar, wafanye kazi kwa kushirikiana ili kuweza kulimudu soko kwa wazalishaji wa bidhaa zinazofanana.
“Wakati mwengine mjifunze kufanya kazi kwa kushirikiana kwani inaweza kutokea mmoja wenu akapata oda ya bidhaa nyingi kuliko uwezo wake sio vibaya kuungana wenzake ili kuweza kulitosheleza soko kuliko kung’ang’ania”, alisisitiza Buchafwe.
Nao washiriki wa semina hiyo waliipongeza taasisi hiyo kwa kuwapatia elimu hiyo na kuitaka kuwa karibu nao ili kuendeleza ujuzi na utaalamu walionao katika utengenezaji wa sabuni.
“Sisi tulizowea kupeleka bidhaa zetu kwa wakala wa chakula, dawa na vipodozi ili kupatiwa ithibati wa ubora wa bidhaa zetu na hatukuelewa kuhusu uwepo wa taasisi hii ambayo ndiyo inayodhibiti ubora wa bidhaa”, alieleza Tatu Suleiman.
Aidha alieleza kuwa mbali ya bidhaa wanazozalisha kuwa na ubora, bado wananchi waliowengi hawapendi kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini jambo waliloiomba serikali kuwasaidia kuwapatia masoko ya bidhaa zao.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanayowashirikiasha wazalishaji wa sabuni 42 kutoka wilaya 7 za unguja pia yamelenga kuwaunganisha wajasiriamali hao kulitambua na kulifikia soko la bidhaa zao kwa kuzingatia viwango vya Zanzibar, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment